Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Musoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, nipende kuchukua nafasi hii kwanza kukushukuru kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hizi hoja zetu mbili za Kamati ya Afya pamoja na Huduma za Jamii. Mimi binafsi naendelea kuipongeza sana Serikali ya Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo wameendelea kuboresha katika haya maeneo mawili. Nilishazungumzia maeneo mengine lakini leo kwa sababu tuko kwenye elimu pamoja na afya naomba nijikite upande huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninakumbuka katika mafanikio mengi tuliyoyapata, na naomba nijielekeze zaidi katika Jimbo langu la Musoma. Hata kwenye upande wa elimu peke yake nakumbuka hata kwa mwaka jana tu tumepata shilingi milioni 700 kwa ajili ya Shule ya Msingi Mwisenge, shule aliyosoma Hayati Baba wa Taifa. Shule hii haikuwa kwenye bajeti lakini kwa sababu Mheshimiwa Rais alikuja kule basi akaitembelea na akaweza kutupatia fedha hizo, kwa hiyo pongezi hizo ziweze kumfikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile hata kwenye zile shule zetu kongwe tulipata 1.2 bilioni kwenye shule yetu ya Musoma Teki. Tumeendelea kupata mafanikio mengi katika nyanja mbalimbali kwenye upande wa elimu. Walimu wameongezeka pamoja na kwamba bado kuna upungufu mkubwa wa walimu kutokana na wingi wa wanafunzi; maana ukiangalia kwenye taarifa ya Kamati wamesema wanafunzi tu wameongezeka kwa asilimia 27.7, kwa hiyo inaonesha dhahiri kwamba baada ya kuwa tumepata mfumo wa elimu bure au elimu bila malipo sasa haya haya ndiyo matokeo yake, kwamba wanafunzi wengi zaidi wameendelea kujiunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ungeangalia kwenye elimu ya juu bado kwa mwaka huu peke yake imetolewa mikopo ya thamani zaidi ya bilioni 49. Hii ni kwa sababu ya wale watoto, wale watoto wasiokuwa na uwezo waweze kuwa na uhakika wa kusoma. Kwa hiyo naipongeza sana Serikali kwa kazi hiyo nzuri
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi hata ukizungumzia kwenye idara ya afya yako mambo mengi ambayo yemefanyika. Uilinganisha sasa na kipindi cha nyuma utakubaliana na mimi kwamba hata upungufu wa dawa katika vituo vyetu vya afya pamoja na kwenye zahanati umepungua ukilinganisha na kipindi cha nyuma. Kwa pale Musoma Mjini kwa mwaka jana peke yake tuliweza kupata fedha isiyopungua milioni 400 kwa ajili ya kituo chetu cha afya cha Makoko naipongeza sana SerikaliPamoja na fedha za bajeti jambo ambalo limetufurahisha sana wananchi wa Musoma na wananchi wa Mkoa wa Mara tumekuwa na hospitali ya Rufaa ambayo tumehangaika nayo kwa zaidi ya miaka 20. Kwa mwaka huu peke yake tumepata bilioni 15 kwa ajili ya ile hospitali na tunategemea wakati wowote ule ile hospitali itaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya si maendeleo ya kubeza, ni maendeleo ambayo ni maendeleo makubwa ambayo tunadhani kwamba kwa kadri tunavyoenda hivi basi kusema kweli tunaenda vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe tu kusema kwamba pamoja na hayo maendeleo ambayo yameendelea kupatikana; lakini liko suala moja ambalo bado ninategemea Kamati iweze kuli-address, kwamba kutokana na ongezeko kubwa la watu mimi nilitegemea Kamati ya Huduma za Afya iweze kulizungumzia hili suala la uzazi wa mpango. Maana kama hatuwezi kulizungumza kila leo huduma zitakuwa zinaongezeka lakini baada ya miaka miwili, mitatu zile huduma zinaonekana tena hazitoshi kwa sababu ongezeko letu la watu bado ni kubwa sana. Sasa hilo nalitegemea, kama hatuwezi kulizungumza na tunaendelea kulikalia kimya kwa hiyo tuendelee kutambua kwamba kazi kubwa ambayo itakuwa inafanyika bado tutakuwa tunaonekana tu bado tuko nyuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mbali na hayo ningependa kufahamu Kamati ilivyojipanga hasa kwenye mapungufu ya kuondoa tatizo la ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, tuna upungufu mkubwa wa walimu wa sayansi katika shule zetu. Hii hata kwenye vile vyuo vyetu vya ufundi, VETA; kati ya matatizo mengine tuliyonayo, mfano tuna Chuo cha VETA pale kinachukua wanafunzi 280. Ukiangalia kile ni chuo ambacho mwanafunzi wa Darasa la Saba anaweza kwenda, wa Kidato cha Nne anaweza kwenda, wa Kidato cha Sita anaenda. Sasa kwa sababu wanachukuliwa wachache, matokeo yake ni kwamba tunapeleka wanafunzi wengi mpaka Vyuo Vikuu, lakini wakifika kule matokeo yake ni kwamba wanakosa ajira. Kumbe tungeweza kuboresha na kuongeza zaidi kwenye hivi vyuo vya ufundi kama VETA vingeweza kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka Serikali ilianza na utaratibu wa kupeleka wanafunzi JKT na wengine wamekaa huko miaka mpaka mitatu. Nadhani ilikuwa ni nafasi nzuri ya kutumia mafunzo ya JKT katika kuwafundisha vijana wetu stadi mbalimbali. Mambo ya kilimo wangeweza kujifunza kule, mambo ya ufundi wangeweza kujifunza kule. Kwa sababu JKT ni mahali pekee ambapo mwanafunzi anaweza kuishi kwa gharama nafuu, lakini akajifunza mambo mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea kwamba baada ya kuwa wamejifunza kule, badala ya kuwaacha tu kwamba sasa hebu rudini majumbani, nilitegemea kabisa kwamba ni mahali ambapo wangeweza kujifunza stadi mbalimbali, mafunzo mbalimbali na baada ya hapo, wale vijana wakapewa mitaji wakaingia wakaja huku kwenye ujasiriamali wakaweza kujiajiri katika ajira mbalimbali. Kile kitendo cha kuwaweka pale halafu baada ya muda tukawaondoa, kusema kweli sioni kama inawasaidia sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)