Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Amina Nassoro Makilagi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. AMINA N. MAKILAGI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe na kumshukuru Mwenyezi Mungu aliye juu Mbinguni kwa kunipa nafasi ya kusimama na kuweza kuchangia hoja hii muhimu ya Sekta ya Huduma za Jamii na Masuala ya UKIMWI ambayo mimi Amina Nassoro Makilagi ni Mjumbe wa Kamati zote hizi mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mara baada ya shukrani, naomba nianze kwa kuleta salamu za wanawake na wananchi wa Tanzania walionipigia kura za kishindo wakanileta hapa Bungeni. Wamenituma nije niseme yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, wanamshukuru Mheshimiwa Rais na Serikali yake ya Chama cha Mapinduzi kwa kuboresha huduma za afya, kwa kutenga fedha za kutosha za kuhakikisha tunapata dawa, vifaa tiba na vilevile tunaboresha miundombinu. Wenzangu wameshasema, sitataka kurudia; na kama alivyosema Mbunge wa Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Vedastus Mathayo, kwa miaka hii ya hivi karibuni tunashuhudia Hospitali za Rufaa zaidi ya 10 zinajengwa katika nchi hii. Mkoa wa Mara peke yake tumepata zaidi ya shilingi bilioni
15. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nianzie hapo kuleta salamu za wananchi wa Simiyu, wanashukuru sana kwa Hospitali ya Rufaa na pia ninaleta salamu za wananchi wa Geita, wanashukuru sana na ninaleta salamu za wananchi wa Katavi, wanashukuru sana, wananchi wa Songwe na wananchi wa Geita na Mkoa wa Mara wanashukuru sana na hata Mkoa wa Mtwara. Wanaomba Serikali iendelee kuleta fedha za kutosha ili Hospitali za Rufaa ziweze kukamilika, hasa kwa kuzingatia kwamba Kanda ya Ziwa mfano Hospitali ya Rufaa ya Bugando imezidiwa, Hospitali ya Mwalimu Nyerere Memorial Centre itasaidia kukabiliana na ile changamoto ya watu (population) ya zaidi 15,000 ambao wanahudumiwa katika Hospitali ya Bugando.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ule Ukanda wa Mtwara hapakuwa na Hospitali ya Rufaa, kwa hiyo, wamekuwa wakipata adha ya kuja Muhimbili. Nina imani sasa changamoto inaenda kutatuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali na wanawake wa Tanzania wamenituma nije kuleta ahsante kwa kujenga hospitali 67. Wanawake wanasema ahsante sana, Mungu amjalie Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, aendelee kutenga fedha kwa zile Halmashauri ambazo hazijafikia mpango huu kwa mwaka wa fedha ujao 2020/2021, nao waweze kupata fedha na hospitali zijengwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala zima la kupunguza vifo vya wanawake na watoto; wanawake wamenituma, wanasema wanaishukuru sana Serikali ya CCM kwa kujenga vituo zaidi ya 350 jambo ambalo limepunguza kasi ya vifo vya wanawake na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninayezungumza, nimetembea ziara kabla ya kuja hapa, kwenye Mkoa wa Mara nimetembelea vituo vyote na mikoa ya jirani nimekwenda, kwa kweli hali ni nzuri, tunashukuru sana na wanawake wamenituma nije niseme ahsante. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa ushauri ninaoutoa kwa Mheshimiwa Spika, tumefanya kazi nzuri ya kujenga vituo, tumefanya vizuri kuboresha huduma, lakini naungana na wachangiaji wenzangu kwamba Serikali itafute fedha kwa ajili ya kuajiri wataalam. Maana tusipoangalia, tumejenga vituo, lakini havifanyi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niwashauri pia kwamba ni vizuri Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na TAMISEMI, wafanye hizo tathmini kuona tangu tumejenga hivi Vituo vya Afya ni vingapi vinafanya kazi? Kwa sababu, mfano nimetembelea Kituo cha Kinesi, Kituo kimeshajengwa, kimekamilika lakini pale hakuna Mtaalam wa Usingizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetembelea Kituo cha Nata Isenye Serengeti Kituo kiko vizuri na huduma zimetolewa lakini yupo daktari mmoja; nimekwenda kule Butiama hakuna mtaalamu wa mionzi lakini pia hakuna x-ray. Kwa kweli tunaweza tukajenga baadaye tukabaki na Majengo nilikuwa naomba sasa Mheshimiwa Waziri na timu yake hebu sasa tujielekeze kwenye wataalamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa ushauri ninaoutoa kama alivyosema Mheshimiwa Tendega ambaye ni mjumbe mwenzangu wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii tumekuwa tukitoa ushauri chini ya Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Peter Serukamba; kwamba sasa ifike wakati Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iwatambue wataalamu wa sekta ya afya iongee nao, izungumze nao iwaombe wajitolee. Sisi wenzenu tulianza kujitolea; hata mimi hapa nilipo sikufika hapa leo nikawa Mbunge, sikufika hapa nikawa Katibu Mkuu, nilianza kujitolea. Mimi nilijitolea miaka mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wataalamu ambao wako tayari wanasubiri ajira, wapo wataalamu ambao wanasubiri kupewa ajira Serikalini ni vizuri tukazungumza nao halafu kupitia vyanzo vya ndani wakalipwa fedha kidogo kwa ajili ya kujikimu ili waweze kutoa mchango wao katika taifa. Vilevile kuna watu waliostaafu kazi, wako huko wamestaafu na bado wana nguvu kabisa; miaka 60, miaka 55, ni wataalamu wetu wanaweza wakashirikishwa ili waweze kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoshauri tena katika mwaka wa fedha ujao 2020/2021 tuje na bajeti nzuri itakayotoa fursa kwa Serikali kuweza kuajiri Wataalamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu naleta shukrani nyingi sana kwa wananchi na wanawake wa Tanzania kwa kazi nzuri sana inayoendelea ya kuhakikisha vijana wetu waliopata fursa ya kupata elimu ya juu wanapata mikopo. Ni ukweli usiopingika kwanza kwa kipindi hiki kifupi zaidi ya shilingi bilioni mia nne zimeweza kutoka kwaajili ya vijana wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kwenye sekta hii ya kutoa mikopo kwa elimu ya juu hebu tufanye uwiano ulio sawa kwa upande wa vijana wa kike ili na nao waende sambasamba kwa sababu takwimu zinaonesha kwamba watoto wa kike wamebaki nyuma kidogo. Vilevile nataka nitoe tena ushauri kwenye kupeleka watoto wa elimu ya juu katika vyuo vikuu; hata ukiangalia takwimu pia uwiano hauendi kati ya wanawake na wanaume bado wanawake wako chini. Nilikuwa nashauri hebu tupandishe hii na wanawake wapate hii fursa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niache salamu za wananchi; wanashukuru sana jinsi ambavyo Serikali imeendelea kutoka mikopo. Ni hivi karibuni tu kupitia takwimu tulizozipata kupitia huduma za jamii ni zaidi ya shilingi milioni mia nne na themanini zimetolewa kwa ajili ya mikopo. Tumetoka mbali kazi ni nzuri tunaomba fedha ziendelee kutengwa ili akina mama vijana wetu waendelee kupata mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa elimu ya dekondari tumefanya kazi nzuri, vijana wetu sasa wanakwenda wengi, na hata kwenye shule za awali wanakwenda, wenzangu wamezungumza, nisirudie. Hata hivyo hapa ushauri wangu, tujitahidi sasa kwenye walimu wa sayansi. Kusema ukweli kuna changamoto ya sayansi katika elimu ya sekondari na msingi. Kama nilivyoshauri kwenye sekta ya afya, tutafute fedha ili tuwapate na walimu wa sayansi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la. Kadri tunavyoongeza watoto; majengo ni yale yale; na bahati nzuri wananchi wanafanya kazi nzuri ya kujenga maboma. Nitatolea Mkoa wa Mara ninakotoka; sisi Mkoa wa Mara hatusubiri Serikali ijenge kuanzia msingi, sisi tunajenga mpaka renta. Wananchi wanahitaji haya maboma sasa yatengewe fedha kwa ajili ya kukamilika. Tunashukuru sana Serikali kwa kutuletea fedha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya Chuo cha VETA.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mungu awabariki, naunga Mkono hoja. (Makofi)