Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nami napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu aliyenijalia kusimama katika Bunge lako hili na kupata fursa ya kuchangia taarifa mbalimbali kutoka kwenye Kamati ambazo zimewasilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuingia Bungeni, Kamati yangu ya kwanza ilikuwa Kamati ya UKIMWI, lakini baadaye nilienda kuwa Mjumbe katika Huduma za Maendeleo ya Jamii. Kwa hiyo, mimi ni kama Mjumbe Mstaafu kwenye hizo Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kupongeza sana sana kwa kazi nzuri ambazo zinafanyika. Nimeanza kusema kwamba nilikuwa Mjumbe kwenye hizi Kamati, niliona kule mwanzo jinsi tulivyokuwa tunapata shida kwenye baadhi ya mambo, lakini naona baada ya kupitia taarifa hizi, kwa kweli kwa sasa yako maeneo ambayo tunafanya vizuri sana, sina budi kupongeza kwa Wenyeviti wa Kamati, Wajumbe wa Kamati na hata Wizara husika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na suala la ujenzi wa Vituo vya Afya. Binafsi naomba sana nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anazofanya. Wako Wajumbe wamesema tuna tabia ya kupongeza sana halafu baadaye tunalaumu sana. Kama binadamu, kunapokuwa na jambo zuri ni lazima usime, lakini hakuna mazuri yasiyekuwa na changamoto. Tunaeleza changamoto kwa ajili ya kuishauri Serikali ili iendelee kufanya vizuri vile ambavyo imekusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kama mwanamke, lakini siyo tu mwanamke, ni mwanamke ambaye nimeshawahi kuingia leba, nimeona matatizo ambayo tumekumbana nayo huko nyuma kupita maeneo ya uzazi na leo jinsi mambo yanavyokwenda vizuri. Kwa kweli naomba nipongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Serikali imeweza kujenga Vituo vya Afya 350. Katika Vituo vya Afya hivyo, katika Mkoa wangu wa Ruvuma tumepata Vituo vya Afya saba. Vituo hivyo saba ni pamoja na vilivyopo katika Wilaya ya Tunduru, Kituo cha Afya Matemanga, Mkasale na Mchoteka. Ninashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie Kituo cha Afya Matemanga ambacho kwa sasa tayari kimeanza kutoa huduma ya upasuaji, nafikiri ndiyo lengo la Serikali kukaribisha huduma ili akina mama wanapopata dharura ya upasuaji, waweze kupata hiyo huduma kwa haraka sana. Naomba sana niipongeze Serikali kwa hiki ninachokisema.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitawapongeza viongozi ambao wameshiriki kwa namna moja au nyingine, akiwepo Diwani wa Kata ile ya Matemanga; amejitahidi sana kufuatilia kwa Serikali, amepiga kelele na hatimaye tumefanikwa, tuna uwezo sasa katika kituo kile kufanya upasuaji wa akina mama wajawazito. Vile vile wanapasuliwa akina baba wenye matatizo ya ngiri na huduma nyingine. Kwa kweli nawapongeza sana na ninawatakia kila heri kwa namna moja au nyingine wale ambao wamehusika katika kufanikisha zoezi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine naomba nizungumze suala la mikopo ya asilimia 10. Ni kweli kupitia Halmashauri zetu na kupitia mapato ya ndani, zipo Halmashauri ambao zinafanya vizuri lakini zipo ambazo mpaka sasa bado zinatekeleza jambo hili kwa kusuasua. Naomba nitumie nafasi hii kupongeza Halmashauri ambazo zinafanya vizuri kupitia hii asilimia 10
kwa lengo la kukopesha akina mama, vijana na walemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukiwasaidia akina mama wajasiriamali wadogo wadogo kuweza kuinua mitaji yao. Kwa kweli jambo hili ni jema. Naiomba Serikali, kwa zile Halmashauri ambazo hazitekelezi vile ambavyo inakusudiwa, ni lazima kuchukua hatua kuona kwamba kila Halmashauri inatekeleza ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo la walemavu. Katika kutekeleza hili jambo kuna miongozo ambayo inatolewa na Wizara, wanapeleka kwenye Halmshauri kwa ajili ya kuziagiza Halmashauri zitoe pesa kwa kufuata miongozo hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie kwenye suala la walemavu. Naomba niishauri Serikali kwenye suala la walemavu ambalo lina shida kidogo. Katika kupitia ile miongozo, inawataka pia walemavu nao wapate ile mikopo kupitia vikundi vya watu watano watano. Ninaamini kabisa kwamba tunapozungumza vikundi, viwe ni vya watu walioshibana ili waweze kuchukua mkopo na kulipa, lakini yapo maeneo mengine walemavu wanashindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kupitia maelekezo yanayotolewa, lingetolewa kabisa eneo maalum la kumtaka hata mlemavu mmoja mmoja aweze kupata mikopo. Kwa sababu maeneo mengine wanashindwa. Unaweza kwenda kwenye kijiji pengine wanatakiwa watano watano, lakini wakakosekana idadi inayotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kupitia Serikali yangu na sina shaka ni Serikali sikivu; kwa kuwa tuna lengo la kuwasidia walemavu, basi kuna vitu ambavyo tunatakiwa tuviangalie upya ili tulegeze masharti tuweze kuwasaidia, tuhakikishe na wale walemavu wananufaika na hii huduma na mikopo ili iweze kuwaendeleza katika maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambao naomba nilizungumze ni suala la ikama ya watumishi. Tunafahamu kwamba tuna tatizo la ikama ya watumishi katika idara mbalimbali, lakini naomba nizungumze kwenye suala la Maafisa Maendeleo ya Jamii wa ngazi ya Kata. Kwenye Halmashauri zangu nane zilizopo katika Mkoa wa Ruvuma, naomba nitolee mfano kwenye Halmashauri moja ambao wana uhitaji wa Maafisa wa Maendeleo ya Jamii 39, lakini mpaka sasa wapo 13. Hata wale 13, wengine wamepelekwa kwenye Idara nyingine kufanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Maendeleo ya Jamii wana kazi kubwa sana. Kazi mojawapo ni kuhakikisha miradi ile ya maendeleo inayokwenda kwenye maeneo wanatoa ushauri mbalimbali. Hata hii mikopo tunayozungumza, Maafisa Maendeleo ya Jamii wa ngazi ya Kata ndio wanaotakiwa waifanye hii kazi ya kuleta uhamasishaji kwa vikundi hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu hii mikopo inanapotolewa wakati mwingine, vikundi vingine vinashindwa, vinasuasua katika kufanya marejesho; na dhamira ya Serikali itoe mikopo na hatimaye watu weweze kurejesha mikopo. Kwa hiyo, wenye kuweza kuleta hamasa ni wale Maafisa Maendeleo ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Utumishi alitembelea katika Halmashauri yetu, aliona mazingira yaliyopo kuhusiana na suala la watumishi. Naomba sana nisisitize kwenye eneo hili kwamba watumishi waliopo ni wachache. Unaweza ukaona na pia Wizara husika inaweza ikaona. Kama wanatakiwa 39 halafu unakuta kuna 13, lakini bado hata 13 wenyewe wameenda katika Idara nyingine katika kusaidia kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niipongeze sana Serikali yangu na Wizara kwa kazi nzuri inayofanyika. Tunawatakia kila heri, wafanye kazi vizuri ili CCM iendelee kushinda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)