Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA – MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MASUALA YA UKIMWI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuhitimisha hoja yangu.

Kwanza kabisa napenda kuwashukuru Wabunge wote kwa michango yenu mizuri ambayo imelenga kuboresha katika vita hii ya kupambana na masuala ya UKIMWI, dawa ya kulevya lakini pia na kifua kikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nawapongeza sana Mawaziri kwa kufafanua. Suala la UKIMWI ni suala mtambuka kwa hiyo, liko katika sekta zote, kwa hiyo basi Wizara kama ya Michezo ikiboresha mambo yake Wizara ya Elimu ikiboresha mambo yake, hata changamoto zile ambazo zinasababisha watu kupata UKIMWI zinapungua. Kwa hiyo, tunawashukuru Mawaziri kwa juhudi zenu katika kuboresha mambo ya kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani za pekee zimwendee Mheshimiwa Waziri, Ummy Mwalimu kwa kutufafanulia kutupatia data ya hivi karibuni ya kuhusu suala la 90, 90 ambalo watu wengi wamezungumzia. Kwa hiyo, tunashukuru, lakini tunaomba juhudi hizi ziendelee kufanyika ili kwa sababu mwaka huu 2020 ndio mwaka ambao tunatakiwa tufikie 90, 90 zote tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Wabunge ambao wamechangia hoja walikuwa sita, kwa sababu ni wachache naomba kuwataja majina; Mheshimiwa Susan Lyimo, Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mheshimiwa Mboni Mhita, Mheshimiwa Amina Mollel, Mheshimiwa Edward Mwalongo na Mheshimiwa Sikudhani Chikambo, lakini na Waheshimiwa wengine wakati wanaanza pia waliipongeza Kamati yetu kwa kazi nzuri ambayo tumeifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, michango ya Wabunge ambao wameonesha hoja zao mingi kabisa ilikuwa imejikita kwenye maeneo yafuatayo; suala la 90-90-90 limezungumzwa, suala la kuhakikisha kwamba Serikali inatafuta vyanzo vya uhakika ambayo Kamati pia imezungumza, imejitokeza. Pia imejitokeza wamechangia kwamba watu waweze kupima ili waweze kutumia dawa ili tuweze kufikia 90-90; lakini pia jambo lingine lilizongumzwa na wachangiaji ni kuharakisha utekelezaji wa Sheria ya Mtoto ya miaka 15 ambayo inamruhusu sasa kupima bila ridhaa ya mzazi ili hasa tuweze kufikia 90 ya kwanza ile ambayo ni muhimu sana kwa 90 pili na ya tatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mchango mwingine ulijikita kwamba elimu zaidi sasa iendelee kutolewa ili watu waelewe zaidi masuala ya UKIMWI, TB na madawa ya kulevya. Pia kuna mchangiaji mwingine ambaye amesema basi Serikali iangalie namna ya kutoa msamaha wa kodi kwa NGOs zinazojishughulisha na masuala ya UKIMWI, TB na madawa ya kulevya ingawa wakati tumekutana na Mheshimiwa Waziri wa Fedha alitufafanulia kuhusu jambo hili. Zipo NGOs kwa kufuata utaratibu maalum wanaweza wakapata huo msamaha wa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema Waheshimiwa wengine Wajumbe wamepongeza Kamati kwa kazi nzuri. Kwa hiyo, hakukuwa na mambo mengi sana ambayo yamejitokeza, sana sana wachangiaji wengi wamepongeza Kamati kwa kazi nzuri na issues ambazo zimetokea wamezizungumza zote ziko kwenye Kamati. Niwashukuru kwamba na wenyewe wameona na wanapongeza juhudi ya Serikali katika kupambana na suala hili la UKIMWI, madawa ya kulevya pamoja na TB. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, labda niseme tu kwa kuhitimisha kwamba magonjwa haya kwa kweli ni hatari hasa upande wa UKIMWI kwa sababu hata kama Serikali itaweka trilioni za fedha kama hatutabadili tabia zetu bado ugonjwa huu hatutaweza kufikia lengo la 2030. Kwa hiyo tubadili tabia tuweze kulindana ili kuweza kufanikisha kutatua changamoto hii ambayo inatukumba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nashukuru sana kwa kunipa nafasi, baada ya kusema haya nahitimisha hoja yangu na naomba kutoa hoja. Ahsante. (Makofi)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.