Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

Hon. Peter Joseph Serukamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigoma Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii

MHE. PETER J. SERUKAMBA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA HUDUMA NA MAENDELEO YA JAMII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wamejadili vizuri ripoti yetu, wamechangia Wabunge 22 na wajumbe watano wameandika kwa maandishi, kwa sababu ya muda nitaomba nisiweze kuwataja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na Wizara ya Afya; nimewasikiliza Waheshimiwa Wabunge wote jambo moja ambalo nadhani Serikali mtakubaliana na Waheshimiwa Wabunge moja, ni kuhusu watumishi wa afya. Umefika wakati, tumewekeza fedha nyingi sana kwenye vituo vya afya, kwenye zahanati, hospitali za mikoa, hospitali za wilaya na hospitali za kikanda. Uwekezaji huu ili uweze kuwa na maana ni muhimu sana kuwa na wafanyakazi, niwaombe Serikali mpo hapa tujitahidi sana tupate wafanyakazi kwenye Idara ya Afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo wengi wamelisema na sisi kwenye mapendekezo yetu tumeliweka ni jambo la bima ya afya. Mimi nawaomba sana Serikali kama kuna jambo, na Mheshimiwa Spika alisema tutakuwa tumeleta ukombozi kwa Watanzania ni kuleta Sheria ya Bima ya Afya kwa wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hili naomba sana watu wa Serikali tusipate kigugumizi kuleta sheria hii. Kamati yangu ilikwenda Rwanda, Rwanda kila Mnyarwanda ana bima ya afya, lakini kwa sababu wanajua kuna watu maskini wameweka social stratification, wamewagawa watu. Katika wote kuna asilimia karibu nne hawana uwezo kabisa, hao Serikali inawalipia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu ukilipiwa na Serikali hutakiwi hata kuwa na bank account, so lazima wajue kweli wewe ni maskini kweli kweli. Kwa hiyo, mimi naomba sana Serikali suala hili la bima kwa wote, na mimi nasema siyo suala la NHIF, ni suala la bima ya afya kwa wote. Ukiipata kwenye private sector sawa, ukiwa nayo kwenye Mfumo wa Serikali sawa, cha msingi kila Mtanzania awe na bima ya afya.

Mimi naomba sana Serikali mlete, na hii mtakuja jambo la misamaha, kuna Wabunge wamesema habari ya maiti kukataliwa, lakini jamani gharama za matibabu ni kubwa sana. Ni kweli wanasamehewa watu wengi, ni kweli Serikali haipeleki ruzuku, kwa hiyo kinachotokea sasa hizi hospitali hazitoweza kutoa huduma bora katika mazingira ambayo bajeti yake haifai. Kwa hiyo niwaombe wenzangu Serikalini jitahidini sana ili kupambana hili la misamaha lazima tulete bima ya afya kwa wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya pia kuna suala la kinga na lishe, nadhani imefika wakati tuwekeze fedha nyingi kwenye kinga pamoja na lishe, tutaokoa magonjwa mengi sana. Ili tuweze kuwekeza kinga lazima turudi kwenye drawing board, tuajiri watu wa social workers waende huko vijijini, hawa ndiyo watasaidia katika haya mambo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo wamechangia watu wengi ni kwenye elimu, mimi nataka niseme kidogo kwenye elimu na nina mambo makubwa mawili/matatu; moja, leo dunia inaenda kwa kasi sana, yuko mwanazuoni mmoja anasema; “we stand on the blink of technological revolution will fundamentally alter the way we live, work and relate to one another”.

Kwa nini nimesema hivyo, leo tunakwenda kwenye fourth industrial revolution, tunakwenda kwenye dunia ya teknolojia, kwa hiyo, lazima Wizara ya Elimu turudi tuangalie elimu tunayotoa inaweza kwenda kupambana na mabadiliko haya makubwa ya kiteknolojia?

Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikia Mheshimiwa Naibu Waziri hapa anasema wanatafuta utaratibu kuowesha mitaala, kuangalia mambo ya, jamani! Bado mimi kama Mwenyekiti na Kamati yangu tunaomba Serikali muendelee kutafakari umuhimu mkubwa kuhakikisha tunapitia mfumo upya wa elimu. Tuje na mfumo ambao kuanzia kindergarten mpaka university, tuangalie je, elimu tunayofundisha, mitaala, uwekezaji, fedha vinajibu matakwa ya sasa? Kama hatuhangaiki na hilo tutapata taabu sana huko tuendako.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna suala la kuboresha elimu, mimi ningeomba sana watu wa Wizara ya Elimu ili kuboresha elimu kunaendana, unaposema tunaboresha elimu lazima hiyo kazi ifanywe na shule za umma na shule za private. Lazima watu binafsi watusaidie kwenye kuboresha elimu yetu, lakini naomba sana Serikali mtafakari, umefika wakati suala la shule za binafsi, kwamba usimamizi wa shule zote liwe chini ya Wizara ya Elimu, tuondoe TAMISEMI. Kwa sababu TAMISEMI naye ana shule kwa hiyo TAMISEMI kuna conflict of interest, kwa hiyo, kuna maamuzi atafanya TAMISEMI kwa sababu anajua anapendelea shule zake. Kwa hiyo, ili kuondokana na hilo jambo mambo yote ya usimamizi wa elimu Tanzania yarudi Wizara ya Elimu, lakini watoa elimu watakuwepo wa binafsi, itakuwepo TAMISEMI kwa maana ya shule za umma. Mimi nadhani hii itatusaidia sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nia nyingine ni kuhakikisha kuwa tuna quality na access, lakini hayo yote yatapatikana kama hatutafanya vurugu kwenye shule hizi za binafsi, lakini pia tuangalie uwezekano wa kutoa kodi kwenye shule za binafsi ili tuweze kuzisaidia.

Pia kuna suala la walimu wa sayansi ni jambo kubwa limesemwa na Wabunge wote, tuangalie pia mitaala ya vyuo vya ufundi na mMimi nasema jamani tumesema tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda unahitaji ….. education so lazima tuangalie upya; je, mitaala yetu ya ufundi inajibu huko tunakotaka kwenda? Kuna shule zinapoteza hawa walimu?

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho ni suala la TBC. TBC ni muhimu sana, lazima tuendelee kuwekeza ili TBC ndiyo pride ya Tanzania, ndiyo pride ya Serikali. Kwa hiyo, lazima tuwekeze kwenye chombo hiki cha kwetu cha Watanzania. Pia na vyombo vya binafsi lazima tuendelee kuvisaidia ili vitusaidie kutoa elimu kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo sana naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.