Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Dr. Haji Hussein Mponda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DKT. HADJI H. MPONDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunipa wingi wa afya ambayo inaniwezesha leo kusimama hapa na kutoa mchango katika mada ambayo tunaizungumzia. Vile vile naomba nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi leo ya upendeleo ili nami nitoe mchango wangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze na pongezi za dhati kabisa, nimpongeze Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako na timu yako, mmeanza vizuri. Mmeanza vizuri wala msitikisike, mikakati mnayoweka tuna imani mnaweza mkatutoa hapa tulipo. Pia, niipongeze Kamati mahiri, Kamati ya Huduma za Jamii; Kamati hii mchango wao na upembuzi waliofanya kwa kweli umesaidia, pengine utaboresha zaidi hii sekta ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wengi wamelalamika, wametoa maoni yao na ushauri; kwa kifupi picha iliyojitokeza hapa, hali ya elimu sio nzuri. Mchango wangu utajikita huko huko na kutoa mfano wa hali halisi. Mheshimiwa Waziri matokeo ya mwaka jana ya vijana wetu wa Kidato cha IV, Wilaya yangu ya Malinyi ni miongoni mwa zile shule 10 ambazo hazikufanya vizuri, Wilaya yangu imetoa shule tatu, zile shule ambazo zimeshika mkia. Matokeo haya yalitusikitisha, yalitushtua, kama wadau wa elimu tulirudi tukakaa chini, kulikoni? Tulijua, lakini imebidi kama wanasayansi twende kwa kina zaidi. Tumeongea na Bodi za shule, tumeongea na Walimu, tumeongea na wananchi, baadaye tumebaini yafuatayo ambayo yanalinganalingana na wenzangu, lakini yangu ni mabaya zaidi na ndiyo maana yamekuja kutokea matokeo yale. Tuna upungufu mkubwa wa Walimu, hususan Walimu wa Masomo ya Sayansi. Tunahitaji Walimu 72, lakini hali ilivyo sasa hivi kule hata kama walimu hawa wakija changamoto nyingine nitazieleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni suala la mabweni; hizi Shule za Sekondari za Kata ambazo ndiyo nyingi katika Jimbo langu, katika Wilaya hii Mpya ya Malinyi zinachachukua wanafunzi kutoka vijiji mbalimbali. Shule nyingine ya Kata kati ya vijiji vitano mpaka kumi, lakini vijiji hivi viko mbali na hizo shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, Shule ya Sekondari Ngoeranga, wanafunzi wengine wanatoka Kijiji cha Kilosampepo, kilometa 22! Kwenda na kurudi mtoto huyu maana yake kwa siku atembee kilometa 44! Kwa hiyo, kulikuwa na dhana pale na ingeweza kuleta jibu hilo, mabweni. Hata hivyo, nimeona azimio la Mheshimiwa Waziri la uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na mazingira ya kujifundishia, lakini mmeelekeza mboreshe hizo shule kongwe.
Nashauri waanze kule kwenye matatizo kweli kweli ambapo kama wanaweza wakayarekebisha matatizo haya, hizo shule kongwe tayari wako pazuri! Mheshimiwa Waziri tumeongea, ameonesha dhamira, naomba asirudi nyuma kwamba, baada ya Bunge hili, pamoja na Mkurugenzi wa TEA watakwenda Wilaya ya Malinyi, waje wayaone haya mambo ambayo mtayazungumza, yamechangia sisi kuwa wa mwisho katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana. Hawa walimu niliosema hata kama wakiletwa, nyumba ni changamoto. Shule nyingine hazina kabisa nyumba ya Mwalimu na shule hizi ziko vijijini wakati mwingine hata hizo nyumba za kupanga, aghalabu, hazipatikani kirahisi. Shule hizi kwa mazingira yalivyo kule tunapakana na mito mingi, tunahitaji madaraja, tunahitaji na barabara, navyo ni kikwazo, Walimu na wanafunzi hawa kufika kwa wakati hasa kipindi cha masika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliliona tena tatizo lingine, mfumo wetu huu wa elimu, mtoto huyu anaanza darasa la kwanza mpaka la saba anajifunza Kiswahili, anapoingia form one Kiingereza, hapo ndio shughuli. Masomo yote ni ya Kiingereza, kwa hiyo ukiangalia ufaulu wao form two wanakwenda vizuri lakini wanapoingia form three, form four ni hatari.
Mheshimwa Naibu Spika, sasa mimi nashauri, kwa nini sasa kama hizi shule binafsi wanaweka pre-form one mwaka mzima ni bora tuchelewe lakini tufike. Kwa hiyo, vyema watoto hawa kabla hawajaendelea kuanza form one walio-pass darasa la saba waanze pre-form one kwa mwaka mzima, wawezeshwe masomo ambayo yanawasumbua, masoma haya ni kiingereza masomo ya hisabati na sayansi. Baada ya hapo ndio waingie kidato cha kwanza mpaka la nne. Hili linawezekana, nimeongea na Mheshimiwa Waziri ukawa unasitasita ukasema sijui kama itawezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba Wabunge wenzangu tukubaliane, ndio maana nimesema chelewa lakini ufike, hawa tunawawahisha wa miaka minne matokeo yake wanakuja kuishia wengi wao asilimia karibu 30 ya watoto wetu mitihani ya form four wanapata division zero.
Mheshimwia Naibu Spika, haya tuliweza kuwezesha sasa tunapitisha hii bajeti, naona wengine mtakwenda mtafika hatua hii mtaigomea, hamtaki kupitisha hii bajeti. Lakini mimi nawashauri na kwanza naomba nishauri Kamati ya Bajeti hii fedha iliyotengwa ni ndogo sana katika Wizara hii, hii sekta ya elimu ni nyeti, ni muhimu sana, tunaomba ile wiki ya kujadili na Serikali Kamati ya Bajeti makae muongeze fedha hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia bajeti hii muundo wake yaani ile structure asilimia 17 ndio inazungumzia elimu ya msingi na elimu ya sekondari, asilimia 48 elimu ya vyuo vikuu, wapi na wapi! Kama kweli tunataka twende uchumi huu wa viwanda wafanyakazi wengi watatakiwa ni hawa wa elimu ya kawaida, elimu hii ya form four, kwa hiyo ingekuwa vyema zaidi tungeboresha hii bajeti, hiyostructure tuweke fedha nyingi zaidi tuziwekeze kwenye elimu ya misingi na elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamelalamikia, wamechangia wameonesha hoja yao, na mimi naungana nao sula la maslahi ya walimu. Wala nisitafune tafune kwa kwali walimu wanaonewa, mafao yao yanasua sua.
Kwa nini wafanyakazi wengine malipo yao pamoja na sisi Wabunge yanaenda chapu chapu kwa nini hawa walimu bado kilia siku sauti ni hiyo hiyo, kila siku wanalalamika lakini kama ni kusikilizwa kidogo kidogo.
Mheshimwa Naibu Spika, naomba nimalizie kuhusu COSTECH (Taasisi ya Sayansi na Teknolojia). Tunasema tunataka tuipeleke nchi hii kuwa ya viwanda, uchumi wa kati, kuwa nchi ya teknolojia ya kisasa, lakini hatufiki huko kama hatuwezi tukawezesha taasisi hii kufanya kazi zake kikamilifu. Maana wao ndio wanatengeneza, wanasimamia suala zima la utafiti na utafiti majibu yake ndio yanatoa ushuhuda au evidence, ushuhuda huu ndio unaotufanya sisi watunga sera, sisi wasimamizi wa hii Serikali namna gani unaweza kuishauri vizuri kwa kutegemea matokeo ya utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyowekwa hapa ni 0.04% ni kidogo mno na mimi nakumbuka utaratibu wetu tulikubaliana COSTECH itengewe bajeti ya asilimia moja ya bajeti ya Serikali. Sasa leo kiko wapi? Tunawashauri Serikali na Kamati hii ya Bajeti mrudi mpitie bajeti ya COSTECH kama kwa fedha hii hawawzi wakafanya chochote matokeo yake tunalaumu ndio tunaruka ruka kwa sababu wakati mwingine tunakosa vigezo, ushahidi kwenye mipango yetu na sera tunazozipanga. Nakushukuru kwa kunipa nafasi tena na naunga mkono hoja asate.