Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Kufuta Hasara itokanayo na Maduhuli ya Madeni ya Nyuma ya Ada na Leseni za Magari, Riba na Adhabu kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2019

Hon. Stanslaus Shingoma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Kufuta Hasara itokanayo na Maduhuli ya Madeni ya Nyuma ya Ada na Leseni za Magari, Riba na Adhabu kwa kipindi kinachoishia tarehe 30 Juni, 2019

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia walau kidogo. Kwanza naunga mkono Azimio la kufuta na kusamehe hasara ya maduhuli ambayo Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Waziri wa Fedha mwaka 2017/2018, wakati Waziri wa Fedha anakuja hapa kuwasilisha bajeti yake, moja ya jambo kubwa lilikuwa ni kufuta leseni za magari ambazo zimekuwa na usumbufu mkubwa na kero kubwa sana kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ni jambo ambalo kila mmoja ndani ya nyumba hii alipiga makofi na kulishangilia kwa sababu siyo tu liliwahusu watu walioko nje ya nyumba hii, lakini hata sisi miongoni mwa Wabunge tuliopo ndani ya jengo hili tulifaidika na msamaha wa huu kodi na maduhuli haya mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni jambo tu la kushangaza na ndipo huku tunapoanza kufahamiana siku zote kwamba sio kila jambo linastahili kupingwa. Tunaongelea kodi ya shilingi milioni 398, wadaiwa waliokuwa wanadaiwa fedha hizi ni zaidi 365,600. Kwa hiyo, hata ukifanya hesabu ya kawaida sio zaidi ya shilingi milioni moja walikuwa wanadiwa kila mtu ambaye amesamehewa deni hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni lazima tufike sehemu tukubali, mimi nikiri kazi nzuri iliyofanywa na Serikali, maelekezo mazuri yaliyofanywa na Wizara ya Fedha kwa kuleta hoja Bungeni na sisi kama Wabunge tukaipokea na kuifanyia kazi. Kazi kubwa iliyofanywa na Kamati kwa niaba ya Bunge ni kupitia na kujiridhisha Mkaguzi wetu ambaye ni jicho amefanya kazi yake sawasawa? Kama kamati yako imejiridhisha bila shaka kwa maelekezo na maandishi ya Mheshimiwa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) tena wakati huo Mheshimiwa Peter Serukamba amesema vizuri dokezo hili limesainiwa na Ndugu Profesa Assad mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa lazima tukubaliane hoja hii tunayoiongea mimi nitoe pongezi kwa Serikali nikupngeze sana Waziri wa Fedha na timu yako kwa kuamua kutuonesha Watanzania huu ndio mfumo wa utawala bora tunaouzungumza katika kujenga na kutetea maslahi ya Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine tukubaliane, Mwenyekiti wangu pengine ameteleza, sote tunafahamu hakuna gari la Serikali ambalo linalipiwa kodi. Kodi tunayozungumza hapa ni kodi ambazo sisi kama wananchi tunapoingiza magari tunafanya utaratibu wa kulipa leseni na baadaye tumekuwa tukiendelea hivyo. Lakini mimi niseme ni lazima tujifunze kushukuru hata ambapo hatutamani kushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kusema jambo hili ni kubwa na mimi niombe jambo moja Mheshimiwa Waziri huko mbele tunakoenda hizi hoja ambazo zinachafua vitabu kwenye mahesabu, hoja za muda mrefu tuangalie pia mbali na kwenye Halmashauri zetu zipo hoja za muda mrefu zaidi miaka kumi. Sasa tuangalie utaratibu mzuri, CAG awe anazifuta kwa utaratibu huu hii nchi tutaijenga tena tutaijenga sana sana na tutendelea kuwepo sana kwa style hii kama ndio hali yenyewe hii Mungu akubariki sana Mzee Mipango pamoja na msaidizi wako kazi nzuri sana. Ahsante sana. (Makofi)