Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Mchinga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Wabunge wenzangu wa Chama cha CUF, naomba niseme kwamba sisi tunaliunga mkono Azimio hili. Tunaliunga mkono sehemu hii ya Selous kuchukuliwa kufanywa kuwa ni hifadhi na kiukweli yapo mafanikio ama faida ambazo zitaonekana hapo baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mimi ni Mbunge ninayetoka Mkoa wa Lindi, naomba nieleze machache ambayo Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha hoja anaweza akawa na majibu. Kwanza, ifahamike mbuga ya Selous inachukua asilimia 38 ya Mkoa wa Lindi. Mkoa wenye ukubwa wa square kilometer 67,000 asilimia 38, zaidi ya square kilometer 24,000 ni Msitu wa Hifadhi wa Selous.
Mheshimiwa Spika, jambo la kupandisha hadhi sisi kama Mkoa wa Lindi utaathiri moja kwa moja, inawezekana athari zikawa za faida (positive) ama negative. Nataka nihoji mambo kadhaa, sasa hivi ukiwa unatembea unatoka Nangurukuru Kilwa unaelekea Liwale hasa muda wa asubuhi, ajabu sana utakutana na malori yanabeba magogo yanayotoka kwenye Selous, tena malori yenyewe hata plate number hayana, yaani yale malori ya zamani, yaliyochakaa na ni mengi. Mimi nimefanya ziara hivi karibuni nimekutana na malori mengi yanakata miti nikastaajabu hii ni kwa mujibu wa vibali ambavyo vimetolewa ama imekuwaje.
Mheshimiwa Spika, pia wafugaji sasa, ukitoka eneo linalopakana kati ya Kilwa na Liwale, maeneo ya Zinga unaelekea Liwale kumekuwa na uvamizi mkubwa wa wafugaji, ng’ombe wako wengi, kule msituni kuna ng’ombe wengi na kuna ukataji hovyo wa miti katika eneo lile. Sasa tunakupandisha hadhi swali linakuja hawa wafugaji ambao wamevamia kwa kiwango kikubwa, wafugaji wengi Mkoa wa Lindi wako Liwale na unapozungumza Selous Mkoa wa Lindi unazungumzia Wilaya za Liwale na Kilwa na Halmashauri ya Lindi Vijijini ya kwetu sisi, hawa wafugaji mtawapeleka wapi, ni wengi mno na wana mifugo mingi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Lindi ambayo ina eneo kubwa la Selous na nimeangalia ramani ya eneo ambalo linachukuliwa kupelekwa Selous, tuna vivutio vingi kabisa ambavyo kupandishwa hadhi kwa pori hili kunaweza kukaunganisha utalii wa Kusini especially utalii wa Lindi. Mfano, tunao mji mzuri wenye historia, Mji wa Kilwa Kisiwani ambao ni kivutio kizuri kabisa cha watalii na inafanya vizuri sasa hivi ukiangalia ile channel yetu ya Tanzania Safari huwezi kuangalia siku mbili kama hujaona inaonyeshwa Kilwa Kisiwani. Nadhani upandishaji wa hadhi wa pori hili unaweza ukaunganisha sasa utalii ukaenda moja kwa moja kwenye Mji wa Kilwa Kisiwani na fukwe nzuri zilizopo katika Pwani ya Kusini maeneo ya Lindi mpaka Mtwara hasa eneo la Mikindani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia mimi nina hakika kwamba jambo hili ili liwe jema sana hizi fedha za REGROW ambazo zinataja Southern Circuit ya utalii ziguse na Mkoa wa Lindi, hazitugusi. Hili ni swali Mheshimiwa Waziri kwako. Fedha za Southern Circuit zinakwenda Mkoa wa Morogoro, Iringa na Njombe, ni fedha zilizosababishwa na Selous, sisi ambao tunachangia kilometa za mraba 24,000 kwa nini fedha hizi hazitugusi? Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha ajibu na swali hili fedha za REGROW sisi watu wa Lindi tunazikosaje? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesema tunaunga mkono jambo hili lakini liendane na uboreshaji wa miundombinu ya barabara. Barabara ya kutoka Nangurukuru kwenda Liwale zile kilometa 230 ni ya vumbi. Kwa hiyo, watalii watakwendaje ikiwa ile barabara haipitiki? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mnaweza mkastaajabu, Lindi tumepakana na Mkoa wa Morogoro kule kwa Mheshimiwa Mlinga, watu wanatoka Liwale wanakwenda Mahenge wanatembea kwa miguu wanatumia zaidi ya siku 5, 6 na wanasindikizwa na wale askari wanyamapori. Naomba upandishaji wa hadhi wa msitu huu uendane na ujenzi wa miundombinu ili na sisi watu wa Lindi tuweze kunufaika na hifadhi ya Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya wenzangu wote na mimi tunaunga mkono Azimio hili. (Makofi)