Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii nzuri.

Mheshimiwa Spika, kimsingi ukiangalia alipowakilisha Mwenyekiti wa Kamati na Kambi Rasmi ya Upinzani ni kama wamekubaliana. Rafiki yangu Mchungaji amezungumza mambo mengi lakini ametoa na majibu. Mchungaji anapoizungumzia UNESCO ni kama vile kuna kachombo fulani hivi ka nchi kanapodhibiti mambo fulani hivi ya nchi fulani. UNESCO imeanzishwa mwaka 1945 inaitwa United Nation Education, Scientific and Cultural Organization. Mwaka 2014, UNESCO ilikuja kwenye Pori la Selous kuweka tahadhari ya Pori la Selous kwa ajili ya mauaji ya tembo. UNESCO ilikuja kuangalia mauaji ya tembo yanayofanyika kwenye Pori la Selous. UNESCO kazi yake ni kuangalia usalama wa maeneo maalum katika nchi mbalimbali kwa vizazi vilivyopo na vijavyo kama alivyosema Mheshimiwa Msigwa hapa sustainable development.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho UNESCO wanafanya kwa sasa ni kumpa kumzawadia Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kutunza mazingira ambayo sasa wameiondoa Selous kwenye hatari wameiweka kwenye usalama. Sasa leo nashangaa unaposema UNESCO kwamba itaondoa miradi, yaani umeitengenezea miradi ambayo unaitunza kwa vizazi vya sasa na vijavyo halafu waondoe mradi, sijawahi kuona. Kwa hiyo, UNESCO ipo pale kuangalia usalama wa maisha ya maeneo mbalimbali kwa vizazi vya sasa na vinavyokuja.

Mheshimiwa Spika, nafikiri wote waliotoa ripoti hapa, Kambi ya Upinzani waliposoma, Mwenyekiti wa Kamati alivyosoma wamefanya sawa. Mheshimiwa Msigwa amesema sasa kwa kuwa Pori la Akiba Selous lilikuwa linasaidia TAWA kwenye mapato na sasa limekwenda TANAPA, kwa hiyo, Serikali ifanye jitihada kwa sababu TAWA na TANAPA ni mali ya Serikali, hakuna nchi zinazojitegemea hapa, hakuna kusema TAWA ina hela zake na TANAPA ina hela zake, ni mali za Serikali. Kwa hiyo, sasa kwa sababu TANAPA inapungukiwa mapato mengine ya kusaidia maeneo mengine kwa hiyo Serikali isaidie TAWA kwa kuwapa hela za kuisaidia kwenye maeneo mengine. Tuna mapori ya akiba 23 yanatosha kuifanya TAWA ipate fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilichokiona hapa na ambacho kwa kweli tunatakiwa kukifanya ni kwamba katika Pori la Selous kuna wafanyakazi 700 wa TAWA na wafanyakazi wa TAWA na TANAPA wanalipwa tofauti. Wafanyakazi wa TAWA wanalipwa mshahara wa laki nne na zaidi wakati wafanyakazi wa TANAPA wanalipwa shilingi milioni moja na laki tano. Sasa inakuja hoja, wafanyakazi wa TAWA ambao wametunza hilo pori toka likiwa bovu, wameliwekea miundombinu, wengine wamezeeka wamebakiza miaka 3, 4 kustaafu, sasa leo kwa mujibu wa sheria zilizopo mtawaondoa wote waende TAWA halafu wataajiriwa wa TANAPA kufanya kazi ile.

Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge wafanyakazi 700 walio kwenye Pori la Selous wabaki pale pale na wenyewe wafaidi hizo hela za TANAPA ambazo zitawekwa mule ndani na wenyewe wapate hiyo mishahara. Naomba tusiwaondoe mule ndani ili mishahara itakayokuja iwakute mle ndani na wenyewe wafaidi. Wamefanya kazi kwa muda mrefu wa kutunza lile pori tusiwaondoe wakaenda kusononeka huko, ni kama vile umetengeneza kitu halafu wewe unanyang’anywa. Kwa hiyo, niombe Serikali na niombe tuliunge mkono ili wafanyakazi 700 wa Selous waliopo pale wabaki kwenye maeneo yao wapandishwe vyeo, wahamishwe waende TANAPA ili na wenyewe wapate kilichoko mule ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine kilichopo ni kwamba TAWA nayo imetumika sana kutengeneza yale maeneo, imeweka miundombinu na vitu vingi. Kwa hiyo, kama kuna uwezekano kama tulivyosema wengine basi Serikali sasa kupitia TANAPA ione namna gani kwenye mapori ya akiba yaliyobaki kuimarisha namna ya kutengeneza kitega uchumi ambacho kitawasaidia kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Spika, kusema kweli hakuna jipya, mambo yote yameenda vizuri. Namshukuru Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii amehangaika sana na habari ya kusema wadau, habari ya kusema nani, lile ni pori la akiba, wadau walishasikilizwa muda mrefu na ni mali ya Serikali. Kwa hiyo, Serikali imefanya uhifadhi kwa kulitoa kwenye pori la akiba na kupeleka kwenye national park.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi sioni kama kuna tatizo ambalo liko hapa. Mimi naipongeza Serikali, nampongeza Mheshimiwa Rais ametuwekea ule mradi pale na watu wengine wajue jamani kuweka Pori la Akiba Selous kuwa hifadhi maana yake ni kama tunatunza kiota chetu, tuna mradi wa Stiegler’s Gorge mkubwa, Mradi wa Nyerere ambao umeanzishwa pale, tunatakiwa tuuwekee mazingira mazuri na waliosema eneo lote liwe hifadhi mimi nakubaliananao ili eneo lile lilindwe vizuri ili tuweze kuutunza ule mradi wetu vizuri kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja, lakini naona hoja hii imeisha, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)