Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, sijui kama nitazimaliza kwa sababu nina mambo machache tu ya kuchangia, nashukuru sana kwa kunipa hizo dakika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niko hapa na mimi ntoka kwenye eneo la Selous, lakini kwa mujibu wa hii ramani nachanganyikiwa sijui ndio ipi, kama ni hifadhi, kipande fulani kinahifadhiwa? Sasa najiuliza je, kule Mlimba ambako kula wale puku hawapatikani mahali popote isipokuwa kwenye lile pori, ndio eneo ambalo linaenda kuhifadhiwa? Kwa sababu, hii kwenye ramani imenichanganya kidogo, sielewi ni eneo lipi?

Mheshimiwa Spika, hata mimi nilikuwa na mawazo kwamba labda lote sasa linahifadhiwa na hi itasaidia kwanza wananchi tunaoishi pembeni ya hilo pori sasa TANAPA wakiingia na sisi tutaanza kupata mapato ukiachilia mpaka…

SPIKA: Kinachohifadhiwa ni ile mipaka inayoitwa Selous hivi sasa vilevile ilivyo. Vilevile ilivyo Selous kwa mipaka yake ya sasa, endelea Mheshimiwa.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa hiyo, mimi naungana na wenzangu waliosema bora tulinyanyue lote kwa sababu itatusaidia, kwa nini nasema hivi?

Mheshimiwa Spika, sasa hivi kinachoendelea huko kwenye maeneo ambayo sio mipaka ya Selous watu wanaingia wanalima, yaani kunakuwa na ugomvi, mara zimewekwa beacon, mara zinaondolewa, watu wanalima, watu wanafuga, lakini huko huko kuna mhanganyiko na wanyama. Kwa mfano kwenye lile eneo lile kuna puku wanapatikana duniani ndio kule tu, sasa hivi wanaisha, wanaitwa sheshe, kitaalamu wanaita puku, sheshe.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, huyu sheshe ni mnyama fulani kama swala pala, lakini mdogo kama mbuzi hivi, lakini mkubwa kidogo kuliko mbuzi, lakini yeye characteristic yake ni kwamba badala ya kwato kukaa kama kawaida zile za mbuzi au nini kwato zake yeye zinakuwa ziko wima namna hii. Anapenda kukaa kwenye maeneo ya mafuriko, halafu panapokuwa na kamuinuko hivi basi anakaa hapo juu hivi. Ni mnyama anapatikana eneo hilo peke yake.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

SPIKA: Ahsante.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, sasa kuna vivutio kama hivi tunafanyaje? Hiyo mipaka ya Selous kwanza mimi siijui vizuri eeh! Basi kama ndiyo hivyo? Tupandishe lote ili kuondoa muingiliano wa wanadamu katika hili eneo ambalo tunaita la hifadhi urithi wa dunia. Wakati tunapanga kupandisha hivyo na tunaita hiyo hifadhi Mwalimu Nyerere tuone namna gani wananchi katika maeneo hayo vijiji vinavyozunguka haya maeneo wapewe elimu watafaidika vipi na uhifadhi huo, bila hivyo kutakuwa na ugomvi.

Mheshimiwa Spika, hapa tunasema tu tunapandisha, lakini je wananchi kule wameenda katika maeneo hayo? Je, wamepewa elimu? Mimi naona tutumie nguvu ya ziada tuende tukatoe elimu katika maeneo hayo lakini ushauri wangu naomba tupandishe hilo pori lote hadhi ili tuhifadhi urithi wa dunia ulioko ndani yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Itete wale Swala Energy wameenda kuchoronga choronga visima pale vya gesi kama sikosei ndani ya Selous lakini pale Itete wanakwenda kuchoronga vile visima vya gesi ndiyo wanyama wako pale, wale wachorongaji wako pale na wanyama wako pale na Swala hao aina ya Puku ninaosema ndiyo walikuwepo kwenye maeneo hayo. Kwa sababu ya mwingiliano na watu sasa hivi wamekimbia wamejificha kule Utengule sijui unakujua? Kule Utengule kule ndiyo waliko wanahangaika hawajui waende wapi. Je tunahifadhi nini? Hamuoni kama hiyo ni rasilimali kubwa ya Taifa? Tunafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wale watu ambao bado wanapendelea pendelea bado kula nyama za porini wanawawinda wale wanawala. Mimi ni-declare hapa interest kwamba zamani nilivyokuwa mdogo tulikuwa tunakula nyama ya Sheshe ni tatu balaa lainii! Lakini siku hizi hatuli tena kwa sababu hamna, sasa hawa waliopo mnawalindaje? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, hebu tuone namna ya kulinda hizo hifadhi, huo urithi wa dunia ambao uko Tanzania tuone kwamba na wananchi watapata mafanikio.

Mheshimiwa Spika, pia hapo hapo sijui Selous labda Mheshimiwa Dkt. Kigwangwala ataniambia pale Kilombelo North Safari Kitalu cha Uwindaji nasema kila siku, yule jamaa mipaka yake haijulikani, mara anachoma nyumba za watu, mara anachoma vyakula, mara ukienda Polisi havieleweki na nimeomba mara nyingi mje muangalie pale, kwa sababu lile eneo ni kero kubwa.

Mheshimiwa Spika, kingine tukihifadhiwa hilo eneo lote, Serikali ione haja sasa ya kuweka uzio kwasababu ninavyosema mpaka leo tembo wanashinda kwenye kijiji cha Iduindembo kule Utengule, wanatoka kwenye haya maeneo ya hifadhi, wanakuja vijijini wanakesha vijijini yaani watu wako hoi. Kibaya zaidi Wilaya ya Kilombero ni kubwa sana kuanzia Kidatu mpaka huko mpakani mwa Njombe, hata huyo Afisa wa Maliasili aliyepo pale hata ukimpigia anahangaika tu tembo wanakatiza mara Mkula hapo wanatoka Selous wanaingia Udzungwa, nadhani mnaelewa, wanaingia huko kila mahali sasa huyu mtu mmoja, gari moja hana uwezo, hivi atasaidia vipi kwahiyo wananchi wanataabika na tembo. Kwa hiyo mapendekezo yangu ni bora sasa tukatoa elimu kwa wananchi tukahifadhi hili eneo lote ili tutenganishe.(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Susan kule Zanzibar wanaitwa ndovu.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ndovu! Sasa hapa siyo Zanzibar hapa ni Tanzania Bara hawa wa Zanzibar watajua wenyewe huko, tukienda Zanzibar tutabadilisha Kiswahili. Kwa hiyo, mimi najua ni tembo na wananchi wangu kule wakisikia tembo ndiyo wataelewa mambo ya ndovu wanajua zile pembe tu sijui unayo habari? Ukisikia ndovu kwetu ni zile pembe tu lakini lile ‘limnyama’ lenyewe linaitwa tembo, lile linaenda kusumbua kule vijijini. Kwahiyo, ningependekezo pamoja na mambo hayo naomba muwaongezee nguvu watu wa Maliasili walioko kule Wilaya ya Kilombero ya magari na wafanyakazi ili watusaidie katika kudhibiti tembo wanaokuja katika vijiji vyetu.

Mheshimiwa Spika, maeneo yote kuanzia huku Mkula, Magombela wapi kote ni shida tupu, Sanje tunaopakana na Udzungwa tunashida sana, tembo wanakatiza wanaenda Udzungwa wanarudi Selous, kwa hiyo wanapita katika majumba ya watu.(Makofi)

SPIKA: Ahsante sana dakika tano zimeisha.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, dakika tano ulinipa dakika 10 nilisema sijui kama nitamaliza.

SPIKA: Mheshimiwa Susan mwenyewe ukazipunguza.

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, nikajipunguzia Saba siyo Tano.

SPIKA: Haya malizia Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba Kurudia tena hebu mtusaidie mpandishe hilo pori lote, kwa sababu kuna mwingiliano, ng’ombe kule ndiyo usiseme! Kila siku ninasema wale ng’ombe walioko kule wako Tanzania, nyama tunakula, maziwa tunakunywa na ngozi tunazihitaji, kwa nini msiweke miundombinu badala ya kuwaswaga swaga wale wanyama mara waende Rufiji mara wapi, kwa nini msiwatafutie maeneo na hifadhi ziko nyingi? Kwa mfano, hapa Kongwa kwako hivi tunashindwa nini hiyo hifadhi ya Kongwa, kuwaleta wafugaji ambao wana uwezo wao kuwapatia block, kuwawekea miundombinu ya kuotesha nyasi za kisasa, kuweka malambo Madaktari, viwanda vya maziwa, viwanda vya ngozi ili tufurahie urithi wa Tanzania na hao ng’ombe wetu hivi mnashindwa nini? Hapa Kongwa hakuna ng’ombe kula nguchilo tu hili pori, kwa nini msiwalete hawa wafugaji.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mnapopandisha hadhi wale ng’ombe watakwenda wapi? nasi wakulima kwa sababu kule hatulimi tena mtuwekee miundombinu katika vijiji vyetu, kutuchimbia mabwawa kutuwekea kilimo cha umwagiliaji, uvuvi wa samaki kwa sababu Kilombero tutakuwa hatuvui tena. Ninyi mna matatizo gani Serikali? Kwa nini hamyaoni hayo? (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumekuja hapa kushauri hayo ndiyo wanayosema wananchi, huo ni ushauri wangu ndiyo maana wakati wa maliasili tulivyopendekeza Wizara zitumbuliwe hapa na mtu wa mifugo tulimtumbua kwa sababu haisaidii Serikali kuwapa miundombinu ni namna gani kuwalea hawa wafugaji ili watupatie uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na Mungu atubariki sana. (Makofi)