Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na mimi niweze kuchangia hoja iliyo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi hakuna mtu anayeweza kupinga maendeleo ya Kitaifa ikiwepo kutunza hifadhi zetu na kuweza kutambua maeneo mbalimbali yakafanyika kuwa hifadhi, mimi mwenyewe mmoja wapo ninapongeza Wizara ikiendelea kufanya hivyo, lakini ikifuata kanuni na sheria za Kikatiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzungumzaji aliyepita ametoka kuzungumza mahali hapa kwamba watu wa lile Pori la Ugalla walikuwepo siku zote na Serikali hii ilikuwepo, wananchi wale wakapewa huduma mbalimbali, huduma za umeme, maji wameendelea kuishi kwa miaka na kufanya mifugo yao mahali pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka Serikali itoe taarifa kwa wananchi, wakaweza kutoa na elimu na kuwaelimisha wananchi ili waweze kujua maendeleo yao, maana yake mwisho wa siku walinzi wa hifadhi wa hizi ni hao hao wananchi wanaoishi maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania hawa wamezaliwa katika maeneo hayo, leo hii tukiwafanya wakimbizi katika nchi yao tunakuwa hatuwatendei haki. Mpaka sasa Serikali inaleta hoja hii mezani kwako hata Kamati yenyewe haijafika kwenda kukagua maeneo husika na kuona ni jinsi gani wananchi wameathirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza wenzangu juu ya TANAPA, TANAPA tumeipatia mzigo mkubwa na ndiyo kazi yetu offcourse lakini je, bajeti tunazopanga kwa Mheshimiwa kiongozi huyu wa TANAPA, je, pesa hizi zinamfikia ili aweze kufanya kazi yake kwa ufanisi na kazi akafanya kwa uweledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vibaya zaidi kuongeza kazi zaidi wakati pesa Serikali haitoi kwa TANAPA wala haitoi msaada wa kuisaidia TANAPA kuweza kufanya kazi yake vizuri, hata tunapoingia kwenye ushindani wa utalii ni lazima mapori haya yawekwe kimpango mzuri hata kuweza kuvutia hawa watalii, lakini kama hawana pesa wanajipangaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya wananchi katika hizi hifadhi zimekuwa za muda mrefu, tunaomba Wizara hata kama leo mnapitisha kwa kura nyingi...

MBUNGE FULANI: Taarifa.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA:...mbazo ziko upande wa pili, tunaomba Mheshimiwa Waziri Kigwangalla uende ukahakikishe hiyo migogoro kwa ukaribu sasa, japokuwa tumetangulia mbele wewe utakuwa unarudi nyuma, wananchi wakaweze kutatuliwa matatizo ya kwao, tunakuomba ufanyie hivyo bwana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mheshimiwa Waziri tunataka tujue katika vijiji kwa mfano kwa upande wa hili Pori la Ugalla kuna watu wa Sikonge na Kaliua mmekataje? Ni kiasi gani ambacho kitaenda kwenye hifadhi mtuambie na kiasi gani ambacho kitabaki kwa wananchi, kilio changu mimi bado ni wananchi, kwa sababu tunajua mwisho wa siku wananchi hawa mmeshawawekea mawe, kuna wakati Mbunge wa Kaliua aliwahi kuzungumza hapa kwamba mnaweka mawe mpaka kwenye vitanda vya wananchi.

Sasa tunaomba Mheshimiwa Waziri kama Mtanzania, naomba urudi tena ukaangalie uhalisia wa Mheshimiwa Mbunge aliyezungmza katika Bunge hili, kama ni kweli vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya ninaunga maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, ahsante sana. (Makofi)