Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Kutekeleza Itifaki ya Cartagena (Nagoya – Kuala Lumpur Supplementary Protocol on Liability and Redress on Cartagena Protocol on Biosafety) pamoja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Haki Miliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. (Protocal for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeder’s Rights) in The Southern African Development Community – SADC) pamoja na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Marrakesh wa mwaka 2013 unaowezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu au ulemavu unaomfanya mtu kushindwa kusoma (The Marrakesh Treaty to Facilitate Access to Published Work For Persons Who Are Blind, Visually Impaired or Otherwise Print Disabled)

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya pamoja ya ziada ya Nagoya – Kuala Lumpur kuhusu Uwajibikaji Kisheria na Fidia kwa Madhara yanayoweza kutokea kutokana na matumizi ya Bioteknolojia ya Kisasa katika Kutekeleza Itifaki ya Cartagena (Nagoya – Kuala Lumpur Supplementary Protocol on Liability and Redress on Cartagena Protocol on Biosafety) pamoja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Haki Miliki za Wagunduzi wa aina mpya za Mbegu za Mimea. (Protocal for Protection of New Varieties of Plants (Plant Breeder’s Rights) in The Southern African Development Community – SADC) pamoja na Azimio la Kuridhia Mkataba wa Marrakesh wa mwaka 2013 unaowezesha upatikanaji wa kazi zilizochapishwa kwa watu wasioona, wenye uoni hafifu au ulemavu unaomfanya mtu kushindwa kusoma (The Marrakesh Treaty to Facilitate Access to Published Work For Persons Who Are Blind, Visually Impaired or Otherwise Print Disabled)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuhitimisha hoja ya Mkataba wa Marrakesh. Pia naishukuru sana Kamati ya Viwanda na Mazingira kwa ushirikiano walioipa Wizara yangu katika mchakato mzima wa kuandaa azimio hili mpaka kufikia Bungeni leo hii. Nawashukuru sana Mheshimiwa Suleiman Saddiq Murad, Col. Masoud pamoja na Wajumbe wote wa Kamati ya Viwanda Biashara na Mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru sana Naibu Waziri Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya, Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa COSOTA na wataalam wote kwa kazi nzuri walioifanya katika maandalizi ya azimio hili la Mkataba wa Marrakesh.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru sana Chama cha Wasioona wakiongozwa na Mwenyekiti Lucy Benito pamoja na Emmanue Simon, Katibu; nawashukuru sana kwa kufika kwenye Bunge letu Tukufu kushuhudia azimio letu hili muhimu sana kwa walengwa wetu, ndugu zetu, watu wenye ulemavu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru sana Naibu Waziri, dada yangu Mheshimiwa Stella Ikupa, Mheshimiwa Balozi Venance Mwamoto, Mheshimiwa Dada Amina Mollel na Mheshimiwa Kaka Ally Saleh, wametoa mchango mkubwa sana katika kusukuma azimio hili liweze kufikia hatua muhimu ya leo. Nawashukuru sana Waheshimiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia, waliotoa ushauri na wale ambao hamjachangia, wote najua mnaunga mkono hoja hii. Tunawashukuru sana kwa niaba ya ndugu zetu watu wenye ulemavu, nawashukuru sana kwa kuunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi nimekuja kushukuru kwa sababu hoja hii haijapingwa na Mbunge hata mmoja zaidi ya kutoa maoni ushauri na tumeelekezwa na Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira pamoja na michango ya Waheshimiwa Wabunge kwamba mara tu baada ya kuridhia Itifaki, basi tujitahidi sana marekebisho ya Sheria ya COSOTA yafanyike haraka iwezekanavyo ili ndugu zetu walengwa waweze kunufaika na itifaki hii, nasi kama Serikali, ushauri huu tumeuchukuwa tutasukuma kwa nguvu ili mapitio ya sheria hizi yaweze kufanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na concern ya copyright kwa mwandishi wa awali, pale ambapo maandishi yake yanahamishwa kwenye muundo wa nukta nundu, kwamba copyright yake, intellectual propaties, atapoteza ile haki, lakini napenda kuwaondoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, kuhama kwa machapisho kunahama pia kwa copyright ya author. Kwa hiyo, jambo hili nilitaka kuwaondoa wasiwasi, copyright inahama pamoja na muundo wa machapisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Ally Saleh kama alivyopendekeza, tuna fursa ya kujifunza kutoka kwenye nchi ambazo tayari zimesharidhia. Kwa hiyo, tutaangalia best practice kwenye hili pamoja na mengine ili kuhakikisha mapitio na ya sera na sheria yanakidhi kiu na nia ya kuhakikisha mkataba huu unawasaidia ndugu zetu wasioona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulitolea maelezo ni suala la ushirikishwaji wa wadau. Mchakato mzima umeshirikisha wadau kikamilifu; na kwa mara nyingine niwashukuru sana ndugu zetu upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wote kupitia COSOZA wametupa maoni mazuri sana ambayo yamepelekea kukamilika kwa mchakato wa kushirikisha wadau na kuleta azimio hili hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tutahakikisha maudhui ya itifaki yanatafsiriwa katika Kiswahili ili yaweze kupatikana kote nchini kwa walengwa wetu pamoja na suala zima la kanzidata kama ilivyoshauriwa. Kuwa na kanzidata ni muhimu sana kwa sababu itatusaidia kuwahudumia walengwa wetu vizuri. Kwa hiyo, jambo hili nalo tumelichukuwa tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa kunipa nafasi hii tena na ninaomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.