Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu Uchambuzi wa Sheria Ndogo Zilizowasilishwa katika Mkutano wa Kumi na Nne na Mkutano wa Kumi na Tano wa Bunge

MHE. ANDREW J. CHENGE - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili niweze kuhitimisha hoja yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru sana Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati hii, Mheshimiwa William Mganga Ngeleja, Mbunge wa Sengerema kwa jinsi alivyowasilisha na umahiri aliouonesha katika kuwasilisha taarifa ya kamati. Amewasilisha vizuri, mtiririko wa hotuba yake na maelezo ya taarifa ya kamati yametiririka vizuri. Pia nimshukuru kwa maneno mazuri aliyosema kuhusiana na mimi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuwa kiongozi, na baadhi yetu kama mimi huwa napenda sana kile kidogo nilichovuna niweze kumega kwa wenzangu, ndiyo maana yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii ujumbe wangu kwa viongozi wengine katika Bunge hili, tuna-talents nyingi sana katika nyumba hii, tusiwe wachoyo kwa kuwashirikisha wenzetu katika kile ulichonacho, na ndiyo tutajenga Institution ya Bunge kwa leo na kesho. Leo sisi tupo kesho hatupo lakini tunataka tuendelee kuliboresha Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge waliosimama na kuongea kuiunga mkono hoja hii. Niwatambue Mheshimiwa Taska Mbogo, Mheshimiwa Saed Kubenea, Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mheshimiwa William Ngeleja mwenyewe, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wote wameongea vizuri sana katika kazi nzuri inayofanywa na Kamati kwa lengo la kujenga. Hata hivyo niseme neno moja, jana wakati tuna ile hoja ya Kamati ya Sheria Ndogo kuhusiana na ule Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali uliohitimishwa jana Bungeni. Napenda sana nimpongeze Mheshimiwa Mariam Kisangi, na jana alisema maneno mazuri tu. Yeye amekuja kwenye Kamati hiyo kujifunza, na katika kipindi kifupi aliweza kutoa mchango mzuri sana kwenye Kamati na jana mlimsikia humu. Hata hivyo linalonifanya niyaseme ya jana yawezekana wengine mmeyapatia tafsiri tofauti. Alisema katika kipindi cha wiki moja chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Chenge amefundishwa mambo mengi, sasa nasema hivi, niliyomfundisha ni mambo ya sheria. (Kicheko/ Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eeh, eeh!Ya sheria tu, lakini ni mwanafunzi mzuri, Waheshimiwa Wabunge!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwanasheria Mkuu amesema maneno mazuri sana, ya mafunzo kwa wanasheria wetu, lakini mimi ningependa niende mbele zaidi, continuing education kwa wanasheria wa Serikali ni kitu kizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa faida ya Taifa hili mimi napenda kuiona Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ule upande wa uandishi wa sheria, ile Idara ya Uandishi wa Sheria ambayo ndiyo roho ya Serikali, mimi nashauri na niiombe Serikali kwa moyo wa dhati kabisa, tuendelee kuwekeza, tuendelee kuwekeza katika uandishi wa sheria. Kada hii ya wanasheria duniani kote ina waandishi wa sheria walio wazuri wachache sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tumeanza kuwa na crop nzuri ndio wanafika kustaafu, wengine wameondoka wakaenda kutafuta greener pastures, lakini zoezi la kuilinda na kuiendeleza Ofisi ya Uandishi wa Sheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu mimi naomba liwe ni ajenda ya kudumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, kwa sura ya pili kwa upande wa Ofisi ya Bunge, tunataka Ofisi ya Mwanasheria wa Bunge iwe na waandishi pia ambao wataweza kuwasaidia Wabunge katika hoja mbalimbali ambazo wanazileta humu Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, amelisema pia Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, unaona kuna element ya improvement katika uandaaji wa sheria ndogo zinazowasilishwa Bungeni ukilinganisha na kule tulivyoanza; tungependa hii trend iwe nzuri; ninaamini kwa assurance ambayo Mheshimiwa Waziri wa Nchi ameyasema nadhani litaenda likaboreshwe hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara na Idara za Serikali watashirikishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Idara ya Uandishi wa Sheria mapema tutaweza kupunguza sana kasoro zilizokuwa zinajitokeza, hasa katika ukiukwaji wa sheria mama ambayo ndiyo msingi unaoruhusu sheria ndogo husika kutungwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo kwa sababu hoja hii imeungwa mkono na wajumbe wote waliochangia, mimi ningependa nihitimishe kwa kuliomba Bunge lako Tukufu kwamba Maazimio ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, yaliyowasilishwa Bungeni kupitia taarifa ya kamati ambayo yapo kwenye Ibara ya 8(1), 8(2), 8(3) na 8(4) ya taarifa ya kamati, sasa yakubaliwe na Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.