Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba hii. Kwa sababu muda ni mchache, naomba niende moja kwa moja kwenye mchango wangu.
Mheshimiwa Spika, naomba niende kwenye Fungu 05 - Tume ya Umwagiliaji ambapo katika maelezo ya hotuba inaelezea kujenga na kuboresha na kukarabati skimu za umwagiliaji. Nakuja kwenye Mkoa wa Katavi, Serikali katika hotuba yake imesema itakarabati skimu 16 na nyingine kujenga tano, nafikiri hii ni Tanzania nzima kama sikosei, maana hawajaielezea vizuri. Hata hivyo, ukirudi katika Mkoa wa Katavi skimu ambazo hazifanyi kazi ni skimu sita, skimu ambayo inafanya kazi ni skimu moja na hii skimu nafikiri ni ile ya Urwira, iko katika Kata ya Urwira, Jimbo la Nsimbo ambayo nafikiri inafanya kazi kwa sababu tu iko chini ya usimamizi wa Kanisa Katoliki.
Mheshimiwa Spika, narudi ambazo hazijajengewa miundombinu ziko 84, ambazo zimejengwa baadhi ya miundombinu ziko 35, jumla ya skimu Mkoa wa Katavi ni 126 na inafanya kazi moja. Je, kweli, tuna nia ya dhati katika kuleta mapinduzi ya kilimo ambayo mazao yake ndio sasa yanayoenda kutumika katika viwanda ambayo tunasema uchumi wa viwanda, naomba tuwe serious katika hili ndugu zangu.
Mheshimiwa Spika, narudi sasa mimi, katika skimu hizo hizo naona zisizofanya kazi Skimu za Mwamapuli na Skimu ya Kilida hazimo kabisa. Skimu ya Mwamapuli katika bajeti ya mwaka juzi iliwekwa kwenye mpango mkakati wa Serikali, wa Taifa. Sasa nauliza na hela ile ilitengwa karibu bilioni mbili, sasa sielewi zilikwenda wapi?
Mheshimiwa Spika, huu mradi ninaosema Skimu ya Mwamapuli katika Kata ya Mwamapuli, Jimbo la Kavuu, nauongelea huu mradi kwa heshima kubwa ya Mheshimiwa Mstaafu Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda. Alitujengea pale mradi mkubwa wa kinu kikubwa cha kuchambulia mchele kwa kutegemea kwamba, hii skimu sasa ingelisha kwenye hiki kinu, lakini mpaka leo hii, kile kinu kinaoza, hakifanyi kazi yoyote, wakulima wamejiandaa pale, tuna mbuga kubwa sana pale na skimu hiyo ni kubwa. Nashangaa kwa nini, na kwenye Wizara ya Maji nimeiongelea, nashangaa kwa nini haichukuliwi hatua? Naomba Serikali sasa inipatie majibu kwa nini skimu hii imeachwa haimo kwenye bajeti kabisa? Skimu ya Mwamapuli na Skimu ya Kilida. Skimu ya Kilida ni matengenezo tu inahitaji, lakini na yenyewe hawajaiweka kabisa. Kwa hiyo, naomba sasa watakapokuja waje na majibu wanieleze kwa nini skimu hizi mbili hawajaziweka kabisa? Pia kwa nini Mkoa wa Katavi iko skimu moja tu wakati tuna skimu 126, skimu moja tu ndio inayofanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe sana, narudi kwenye Jimbo langu la Kavuu, nataka wanieleze kwa nini Mradi wa Skimu ya Mwamapuli pamoja na Kilida haumo kwenye bajeti? Je, hauna umuhimu kwa wananchi? Je, ilikuwa haifanyi kazi? Miradi yote hii ilikuwa inafanya kazi. Sasa naomba waniambie kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niongelee suala la pembjeo, hasa kwenye upande wa mbegu. Nataka nijiulize, nimekaa nikijiuliza sana kwani ni lazima kila mwaka mwananchi anunue mbegu? Je, katika zile mbegu wanazokuwa wamezileta mwaka huu, je, mkulima amelima, mimi nakumbuka zamani tulikuwa tukilima, mnachagua mahindi ambayo ni mazuri mnayahifadhi kwa mbegu; je, hizo mbegu zikihifadhiwa zikatumika kwa mwaka unaofuata hazifai? Naomba niulize swali hili kwa sababu, tumekuwa na ucheleweshaji wa mbegu ambazo sasa wakulima wanakuwa hawapati. Nilikwishasema maeneo mbalimbali yana mvua tofauti, kwa mfano katika Jimbo langu la Kavuu mimi kuanzia mwezi wa 11 mvua zinaanza kunyesha, pembejeo wanaanza kuleta mwezi wa Tatu, sasa je, mtu akihifadhi mbegu alizolima mwaka huu akahifadhi akapanda mwaka kesho, hizo mbegu hazifanyi kazi? Nawauliza kupitia kitengo chao cha utafiti? Maana tunataka kujua kwa sababu, hata hizo wanazoleta kila mwaka bado hazioti na hazifanyi vizuri. Kwa hiyo, naomba watufafanulie katika hayo.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Wananchi wangu wamenisikia. Nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)