Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JANETH M. MASABURI: Mheshimiwa Spika, pongezi kubwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Niongelee utafiti. Bila utafiti wa magonjwa ya mazao, bila utafiti wa mbegu bora, bila utafiti wa masoko ya chakula na mazao ya biashara, bila utafiti wa wataalam wa kilimo ili kutambua ni wataalam wangapi waliopo na wako wapi na wanaleta tija gani katika maeno ya wakulima hapa nchini haya yote yasipozingatiwa na umakini mkubwa, na kikubwa bila kutenga bajeti ya kutosha katika maeneo yote hayo. Narudia tena kuiomba Serikali kutenga fedha za kutosha kwenye bajeti katika maeneo hayo na mengine ya kitaalam ambayo yanakuwa ni kikwazo na kurudisha nyuma sekta hii nyeti ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, maafisa ugani; maafisa ugani ni wachache na hata wale waliopo hawaonekani. Hii ni kutokana na ukosefu wa vitendeakazi kama magari, pikipiki, vifaa vya kunyunyizia dawa ya kuulia wadudu waharibifu wa mazao n.k kwenye maeneo ya kata mbali mbali hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kilimo cha muhogo; kilimo cha zao la muhogo ni chepesi na ni rahisi zaidi na kinastahimili ukame, lakini pia kina tija kubwa kwa wakulima wengi, hasa wadogo wadogo na wa kati. Hata hivyo pia kuna wawekezaji wakubwa na wa kati wameanzisha viwanda vya kuchakata zao hili la muhogo kama kule Mkoa wa Lindi na Handeni (Tanga) ili viwanda hivi viweze kuzalisha kwa kiasi kikubwa zao hili la muhogo na ikizingatia kuwa wawekezaji hawa wametumia fedha nyingi kwa kuja hapa nchini kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda kama ilivyo malengo ya Serikali ya Awamu ya Tano (Serikali ya Viwanda). Wawekezaji hawa pia wangepewa maeneo makubwa ya kulima kilimo cha muhogo kama walivyopewa maeneo wawekezaji wa kilimo cha miwa ambao wanazalisha miwa na kisha kusindika (sukari), viwanda vya kuchakata mpunga na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, wawekezaji hawa wanalima mashamba yao na pia wananunua mazao mengine kwa wakulima wadogo wadogo (outgrowers).
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naiomba Serikali iwapatie maeneo makubwa wawekezaji wenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo kama muhogo na mazao mengine ambao wamewekeza kwa kujenga viwanda hapa nchini. Kwa mfano kiwanda cha kuchakata zao la muhogo mkoani Lindi wanahitaji eneo kubwa la kulima zao hili. Wamepewa kiasi kidogo ili kuwapa moyo na kuvutia wawekezaji wengi, ni vyema wakapatiwa eneo la ziada ili kukidhi haja na tija kwa kiwanda na wakulima wengi Tanzania kwa mkoa wa Lindi na mikoa mingine ambayo inalima mihogo. Kiwanda cha Lindi ni muhimu sana, kiongezewe eneo.
Mheshimiwa Spika, kilimo cha umwagiliaji. Kilimo cha umwagiliaji ndiyo suluhisho la kumkomboa mkulima wa Kitanzania na kupata ziada kuuza mazao nje ya nchi. Nchi ifanye jitihada kubwa kujenga miundombinu ya kukinga maji ya mvua ambayo yatasaidia kunywesha mifugo, kufuga samaki, kumwagilia mazao ya kilimo na matumizi ya nyumbani. Je, eneo hili la kukinga maji ya mvua kwa kutengeneza mabwawa makubwa ya kuhifadhi maji ya mvua na kuweka miundombinu ya kutiririsha maji hayo kwenye maeneo ya kilimo yanahitaji fedha za kigeni na wataalam kutoka nje ya nchi?
Mheshimiwa Spika, Ombi. Wizara ya Fedha itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Wataalam wetu katika Wizara ya Kilimo watambue unyeti wa Wizara hii na kwa uchumi wa nchi yetu, na watekeleze kwa kuhakikisha wanashirikisha na Wizara nyingine kama Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Viwanda na Biashara,Wizara Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia na Watoto, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano) n.k.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.