Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Eng. Joel Makanyaga Mwaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chilonwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JOEL M. MAKANYAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kwanza kabisa nikushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamechangia wachangiaji wengi na mimi niko ndani yao yaliyozungumzwa kwa hakika ni yale ambayo na mimi ningependa niyazungumze kwa undani. Lakini nataka nijiweke kimsingi katika kukubaliana nao kwamba elimu ndiyo kila kitu, ndiyo msingi wa maendeleo bila kuwa na elimu bora Taifa halitapiga hatua yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila kuwa na elimu bora safari yetu ya kuelekea Tanzania ya uchumi wa kati itakuwa ni ndoto kwa sababu huko tunazungumzia kuwa na viwanda pamoja na kwamba tunapuzungumzia Tanzania ya viwanda maana yake tunazungumzia industrialization. Tukienda katika historia wenzetu wamepita huko miaka ya 1800 wakati sisi tuko kwenye primitive, lakini leo sisi tunazungumzia industrialization basi tuifanye iwe kweli kwa maana ya kwamba iwe elimu bora ndiyo maana wachangiaji wote wanapiga kelele elimu iwe bora tuweze kwenda jinsi tunavyotaka sisi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme machache, kwanza nimevutiwa sana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri, hotuba imesheheni kila kitu ambacho kinahitajika kutufanya sisi tuweze kusonga mbele katika nyanja ya elimu na kwa hiyo kuweza kutubeba sisi kutupeleka katika Tanzania ya uchumi wa kati. Lakini tatizo liko wapi, tunapopiga kelele na elimu kuwa siyo bora, elimu duni tatizo liko wapi, mipango mizuri tunayo, mikakati mizuri tunaiweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu ili tuweze kufika tunakotaka, tunahitaji kuwa na elimu bora inayozingatia usawa kwa wanafunzi wote. Tunapozungumzia elimu bora tunazungumzia elimu yenye mitaala iliyosimama na syllabus zilizosimama, zisizobadilika badilika, hii ni sera hatuwezi kuwa na sera ya kutufikisha popote inayobadilika badilika kila wakati. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi naona sehemu moja ambayo inaleta shida kwetu ni hapo kwamba sera zetu mitaala yetu syllabus zetu zinabadilika na zinabadilika na watu. Leo yuko Mama Ndalichako anakuja kivyake, kesho anakuja Mwaka anakuja kivyake, keshokutwa anakuja Mheshimiwa Zungu anakuja kivyake hatuwezi kusonga mbele hata siku moja, tunatakiwa tuwe na sera iliyosimama, haijalishi leo yuko nani, kesho yuko nani ili tuweze kuwa na elimu bora.
Pili, tunahitaji kuwa na walimu bora, walimu bora utawapata wapi? Lazima uwapate vyuoni je wanadahiliwa vipi kuingia vyuoni. Tumesikia hapa tatizo la udahili wa vyuoni. Tumesikia hatua zilizochukuliwa na Mheshimiwa Waziri kwa wale waliotufikisha pabaya pamoja na kwamba tunalia hawa wanafunzi waliofutiwa masomo kwa kweli tunaomba Serikali iwafikirie mara mbili mbili, kuwapoteze muda mwingi na sasa waende wakaanze upya na hawajui waanzie wapi kwa kweli siyo sahihi. Tunaiomba Serikali iwafikirie kwa sababu halikuwa tatizo lao tunajua kuna namna yoyote inaweza ikafanyika ili nao waweze kujikwamua kimaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini udahili vyuo vya walimu viko vipi huko wanakosoma walimu kukoje vyuo viko sawasawa au wanakwenda kupitisha muda tu miaka miwili, mitatu wanatoka wanakuja kufundisha? Hayo ni mambo ya msingi katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na elimu bora. Mazingira ya kufundishia yako vipi? Madarasa yako vipi, madarasa yasiyokuwa na sakafu, madarasa ambayo darasa moja linaingia wanafunzi mia moja naa mpaka mwalimu anakosa pa kusimama, hilo ni darasa ambalo mwalimu anaweza akafundisha kweli? Tunajua mwalimu anapofundisha ana standard awe na wanafunzi wangapi darasani, aweze kuwapitia hata wale walio slow learners kuwavuta waende na wenzao. Sasa mwalimu anapokuwa na darasa limejaa hata pa kupita haoni atawasaidia vipi hao wengine slow learners na hata hao first learners hawawezi ku-learn chochote katika darasa ambalo limesheheni wanafunzi kiasi hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia vifaa vya kufundishia, viko mashuleni kweli? Maana yake sisi ndiyo tunaotoka huko vijijini, ndiyo tunaotoka huko kwenye majimbo yetu, shule zina vifaa vya kufundishia? Serikali ina mpango gani katika hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie pia maslahi bora ya walimu. Ukishakuwa na mwalimu bora lazima awe na maslahi bora maslahi bora ya mwalimu ni pamoja na mshahara wake uwe mzuri, tunazungumzia kwamba ukitaka kuwa Mbunge lazima utapita kwa mwalimu, ukitaka kuwa Rais lazima upite kwa mwalimu, ukitaka kuwa daktari lazima upite kwa mwalimu, lakini huyu mwalimu ukishapita umemuacha hapo nyuma, leo kuna mwalimu aliyenifundisha mimi pengine nikianza kumgeukia nyuma ninachokipata mimi kama mshahara wangu ukilinganisha na cha mwalimu hakuna heshima hata dakika moja. Wanavunjika moyo, wanaona kwamba kazi hiyo ni kazi ya kudharaulika sana, hebu tuifanye kazi ya walimu kuwa kazi ya heshima kwa kuwaangalia kwenye maslahi yao kwa upande wa mishahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na mishahara hiyo waliyonayo stahili zao wanazostahili wanazipata inavyostahili? Mwalimu anahamishwa, hapati hela ya uhamisho. Mwalimu anatakiwa kwenda kwenye semina au walimu wanatusaidia kwenye kusahihisha mitihani pesa za kusahihisha mitihani hawazipati kwa wakati unaostahili. Hivi tunawaangalie kweli walimu kwa karibu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la nyumba za walimu. Walimu huko vijijini mkienda utawaonea huruma, wanakaa kwenye vibanda ambavyo huwezi kuamini, sasa tunaanza kuwaambia walimu wakipangiwa shule wakienda wakiripoti wanaondoka, hata mimi ningeondoka, anakwenda kuingia kwenye kibanda ambacho huwezi kuamini, kweli mwalimu ametoka chuoni anakuja kuwafundisha wanafunzi anaingia kwenye kibanda hamna taa okay mambo ya taa siyo tatizo watanunua siku hizi kuna mambo ya solar kuna nini, lakini kibanda kimejibana kidogo kidogo tu, kitanda hakuna nafasi ya kuweka kitanda cha sita kwa sita hakiingi kweli jamani? Hii siyo sawasawa hebu tuwaangalie kwa karibu.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho na muhimu katika ubora wa elimu ni hili la kuzikagua shule. Shule hazikaguliwi kabisa, ukienda shuleni ulianza mara mwisho wamekaguliwa lini utacheka, hazikaguliwi na hiki ndicho chanzo kikubwa cha elimu kushuka pamoja na walimu kuwa wamekataa tamaa lakini kama wanajua kuna mtu anawafuatilia nyuma basi hata kawoga kidogo kanakuwepo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu naomba haya masuala Mheshimiwa Waziri ayachukue pamoja na mengine mengi waliyozungumza wenzangu ayachukue na Serikali iyafanyie kazi kama kweli inataka kufanya Tanzania tuwe na elimu bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili usawa kwa wanafunzi. Tuna wanafunzi wengine wenye mahitaji maalum, mahitaji maalum…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante,