Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Hamoud Abuu Jumaa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibaha Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuwepo mahali hapa nami niweze kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya Mwaka 2019/2020. Vilevile nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Waziri na watendaji wake wa Wizara kwa kuandaa hotuba nzuri, hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi kwa kuhakikisha sekta nzima ya kilimo inaendelea kuimarika kama ilivyoainishwa hasa ukizingatia nchi yetu ina uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuanza kwa kutoa pongezi zangu kubwa kwa Serikali, hakika Serikali imeendelea kuweka jitihada za kutosha katika sekta nzima ya kilimo. Hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2017/2018 na upatikanaji wa chakula kwa mwaka 2018/ 2019 imeendelea kuimarika kutokana na hali nzuri ya mvua katika maeneo mengi ya nchi, kuongezeka kwa tija na uzalishaji. Uzalishaji wa mazao ya chakula umefikia tani milioni 16.89 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula ya tani milioni 13.57. Hivyo nchi ina ziada ya chakula ya tani milioni 3.32 za mazao yote. Hii ni hatua nzuri na ya kujivunia kwa usalama wa chakula ni usalama wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingine kwa Serikali ni Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Tarehe 4 Juni, 2018 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizindua Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Programu hiyo inalenga kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo; kwa maana ya mazao, mifugo na uvuvi; ili kuongeza uzalishaji na tija, kufanya kilimo kiwe cha kibiashara na kuongeza pato la wakulima, hususan wakulima wadogo kwa ajili ya kuboresha maisha na usalama wa chakula na lishe, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ASDP II.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeimarisha Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ili kuwa benki mama itakayoongoza mipango inayolenga kutatua changamoto ya ukosefu wa mitaji kwa wakulima, wafugaji na wavuvi nchini. Lengo la Serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni kuifanya TADB kuwa benki ya mfano na ya kisasa katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini kutoka katika kilimo cha mazoea cha kujikimu kwenda katika kilimo cha kibiashara na uzalishaji wenye tija katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kujivunia sana, hadi kufikia Februari, 2019 TADB imetoa mikopo ya shilingi bilioni 100.7 ikilinganishwa na shilingi bilioni 10 mwaka 2017. Mikopo hiyo imewanufaisha zaidi ya wakulima na wafugaji milioni moja nchi nzima. Aidha, TADB tayari imeshafungua ofisi mbili za kanda Jijini Dodoma na Mwanza.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa menejimenti na Bodi ya TADB ni kukamilisha ufunguzi wa ofisi zilizopangwa kwa wakati ili kutatua changamoto za upatikanaji wa pembejeo na miundombinu duni ya uzalishaji, usafirishaji, uchakataji wa mazao na masoko zinazokabili wakulima wadogo nchini; kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyotangulia kuzungumza katika hotuba yake.

Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao makuu ya biashara ya kimkakati yakiwemo chai, kahawa, korosho, pamba na tumbaku umeimarika kutokana na juhudi zinazofanywa na Serikali ikiwemo kuimarisha ushirika. Kwa mfano, uzalishaji wa zao la pamba uliongezeka kutoka tani 132,934 mwaka 2017/2018 hadi kufikia tani 222,039 mwaka 2018/2019, wakati uzalishaji wa zao la kahawa uliongezeka kutoka tani 45,245 hadi kufikia tani 65,000.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa mazao hayo na mengine kwa kuwa ndiyo mhimili wa kutoa malighafi za kuendesha viwanda na yana mnyororo mpana wenye fursa ya kutoa ajira nyingi na kuliingizia taifa fedha za kigeni. Mfano, katika mkakati wa uzalishaji wa zao la chikichi Serikali kwa kweli imekuwa ikitumia fedha nyingi za kigeni kwa ajili ya kununua mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. Aidha, uzalishaji mdogo wa zao la chikichi ni miongoni mwa sababu za kushindwa kujitosheleza kwa mahitaji ya mafuta ya kula nchini. Kutokana na changamoto hiyo Serikali imeamua kuweka nguvu kubwa kwenye uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta ili kuondokana na utegemezi na kuokoa matumizi ya fedha za kigeni.

Mheshimiwa Spika, sina budi kuendelea kuishukuru Serikali kwa kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto za wakulima jimboni kwangu. Hata hivyo bado kuna baadhi ya maeneo kumeendelea kuwepo changamoto za migogoro ya wakulima na wafugaji. Migogoro hiyo baadhi yake imekuwa ikilalamikiwa na wakulima kwa baadhi ya maamuzi yanayochukuliwa na kuonekana kesi nyingi zikiwapendelea wafugaji.

Naiomba Wizara kuchukua hatua madhubuti hasa katika kipindi hiki kwa kuangalia namna gani itaweza kutatua migogoro hiyo kwa kuhakiki mipaka ili maeneo ya wakulima na wafugaji yajulikane. Kufanya hivyo kutasaidia kumaliza tatizo kubwa lililopo jimboni kwangu la migogoro hii. Aidha, kuna madai ya muda ya wakulima wa zao la korosho wa Soga, Kikongo na kadhalika. Wakulima hawawana madai yao kwa Serikali, ni fedha za malipo kwa ajili ya zao la korosho. Sasa namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa akihitimisha hotuba yake anipe majibu ya changamoto hizi ili wananchi wangu wapate kujua hatma ya maswali wanayojiuliza.

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika kuna tatizo katika mradi wa Shamba la Umwagiliaji la Mongomole, Kwala. Mradi huu umetumia fedha nyingi na inasemekana kuna ubadhirifu mkubwa umefanyika. Nakuomba Mheshimiwa Waziri atupe majibu juu ya mradi huu na tuhuma hizi. Je, Serikali inatambua hilo na hatua gani za haraka itakwenda kuzichukua, kwani mradi huu umetumia fedha nyingi na umekuwa hauna tija kwa wananchi?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.