Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
ACT
Constituent
Kigoma Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi jioni hii ya leo. Kwanza napenda niunge mkono Hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni kama ilivyosoma na Dkt. Sware leo, naamini kabisa kwamba Serikali itaweza kuchukua maoni ambayo yameelezwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na kuweza kuyafanyia kazi kwa manufaa ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitajikita kwenye eneo moja tu la uvuvi leo; katika maeneo hayo mawili mifugo na uvuvi mimi nitazungumzia uvuvi peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uvuvi kwa mujibu wa takwimu za Serikali unachangia asilimia 2.2 katika Pato la Taifa (Gross Domestic Product). Kwa hiyo ukichukua Pato la Taifa la nchi yetu la shilingi trilioni 125 maana yake ni kwamba shughuli za uvuvi, yaani mnyororo wote wa thamani wa uvuvi unachangia shilingi trilioni 3 katika Pato la Taifa la shilingi trilioni 125. Ukichukua Watanzania watu wazima leo, ambao wana uzwezo wa kufanya kazi ambao ni takriban milioni 27 kwa population ya watu milioni 54, na kwa takwimu za Serikali kwamba asilimia 50 ya Watanzania wanajishughulisha na shughuli za uvuvi maana yake ni kwamba ukigawa Pato la trilioni 3 kwa mwaka linalotengenezwa na Sekta ya Uvuvi ina maana kila mvuvi nchi hii Pato lake kwa mwaka ni shilingi 230,000 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukilinganisha na Pato la mtu per capita income ya Mtanzania ya takriban shilingi 2,000,000 unaweza ukaona ni namna gani ambavyo wavuvi katika nchi hii wana hali mbaya sana, wana umaskini wa hali ya juu sana. Tunahitaji mkakati maalum wa kuhakikisha dekta hii kwanza inakuwa inachangia kwa kiwango kikubwa kwa maana ya asilimia 5 kama ambavyo Mpango wa Maendeleo wa Taifa ulivyotaka, lakini tunaona Serikali kiwango cha bajeti ambacho kinawekwa kwenye sekta hii wala huwezi kuamini kwamba kuna nia ya dhati ya kuweza kuifanya Sekta ya Uvuvi iweze kukua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu la uchaguzi asilimia 30 ya wakazi wake wanategemea uvuvi katika Ziwa Tanganyika, na sasa hivi tumeanza anza pia kufuga samaki. Lakini sasa ukiangalia Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapin duzi ukurasa wa 22 Ibara ya 27 kuna ahadi 16 zinazohusiana na Sekta ya Uvuvi. Ahadi 16, ukurasa wa 22 Ibara ya 27 ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo ndiyo tunapaswa kuwapima Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Katika ahadi 16 Serikali mpaka sasa tunakwenda kwenye bajeti ya nne haijatekeleza ahadi hata moja ambayo waliitoa kwa wananchi wakati wanaomba kura. Nitawapa mifano ya ahadi tatu tu ambazo mpaka sasa hazijatekelezwa. Chama Cha Mapinduzi waliahidi wakiunda Serikali watanunua meli tano za uvuvi zenye uwezo wa kuvua samaki bahari kuu na kuzalisha ajira 15,000, hakuna hata meli moja imenunuliwa mpaka sasa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama Cha Mapinduzi kiliahidi kujenga bandari ya uvuvi ambayo itaweza kuzalisha ajira 30,000 hakuna hata dalili za kuanza kwa hiyo bandari ya uvuvi. Sasa tunashindwa kuelewa tutawapima namna gani mwaka 2020 sisi wavuvi? Tutawapima kwa nyavu za wannachi ambazo mnazichoma kila siku? Tutawapima kwa mitumbwi ambayo mnawavunjia wananchi kila siku? Tutawapima kwa umaskini ambao mmetengeneza kwa wavuvi katika nchi hii? Naomba Chama Cha Mapinduzi na Wizara ya Mifugo Uvuvi…
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa kidogo.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naom ba Waziri ana nafasi ya kujibu dakiak zake, aniache nitiririke, a-relax, relax brother!
MWENYEKITI: Mheshimiwa Zitto subiri kidogo. Mheshimiwa Waziri, Taarifa.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa Taarifa hii. Naomba nimpe taarifa; kwa kuwa amezungumza jambo kubwa sana linalohusu Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi, ingekuwa kama anachangia katika njia ya kawaida pasingekuwa na taabu, lakini anaposema kuwa mpaka kufika sasa mwaka wa nne Serikali ya Chama Cha Mapinduzi katika ahadi tulizozitoa upande wa Sekta ya Uvuvi hakuna tulichokifanya, nataka nimwambie asome vizuri hotuba ya Mheshimiwa Waziri ataona yale ambayo tumeyafanya katika kipindi kifupi baada ya Mheshimiwa Waziri Mpina na mimi Naibu wake kuingia katika Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, katika hayo ya uvuvi nataka nimkumbushe atazame liko jambo linalohusu TAFICO. Na nataka nikuambie kaka yangu Zitto ya kwamba huwezi kwenda katiak uvuvi wa bahari kuu bila ya kuanzisha Taasisi ya kusimamia, shirika la kusimamia. Tumeanzisha TAFICO, tumefufua TAFICO kwa lengo la kuhakikisha kuwa tunakwenda kusimamia uvuvi wa bahari kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nataka nimuelimishe kidogo katika eneo hili…
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, umefahamika…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
MWENYEKITI: Mheshimiwa ulishafahamika, Mheshimiwa Zitto, taarifa hiyo.
MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa siipokei. Mimi nimetaja kurasa ya Ilani ya Chama ambacho yeye ndiyo anapaswa kuitekeleza. Ukurasa wa 22 Ibara ya 27 kuna ahadi 16, hakuna ahadi ya TAFICO. Kwahiyo huwezi kujitungia swali na ukajitengenezea jibu, ukajipa tiki, hakuna! Angalieni Ilani yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa uvuvi katika Ziwa Tanganyika tuna malalamiko mengi. Baadhi ya malalamiko yamejibiwa na Serikali lakini pia tutapenda kuona kama wale ambao waliumizwa na maamuzi ambayo sasa Serikali imeyageuza na namna gani ambavyo watakavyofanyiwa compensations zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza tuna tatizo la tozo, export, ushuru wa export. Nchi yetu inachimba na inavuna dhahabu. Wawekezaji wa dhahabu wanauza dhahabu nje, hakuna tozo ya export ya dhahabu. Kwanini tunaweka tozo ya export ya samaki? Tozo ya export ya dagaa Ilikuwa dola 1.5 kwa kilo sasa imekuwa dola moja, kiwango kikubwa, tena wanatoza kwa dola. Wavuvi wa Kalya, wavuvi wa Kagunga, wavuvi wa kila mahali wanatozwa kwa dola, ni kwanini? Kwa hiyo naomba tozo hii ya export iondolewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili pamoja na nyavu kuchomwa na pamoja na Serikali kutoa maelezo mengine kuhusiana na suala la nyavu, kama nilivyosema tungependa tufahamu, sasa wale ambao wamechomewa nyavu zao na vyombo vyao ambao Serikali sasahivi imebadilisha sera yake, Serikali itawalipa namna gani? Kwa sababu ni watu ambao wameshaingizwa kwenye umaskini na ningependa kwakweli tuweze kuhakikisha ya kwamba jambo hili linashughulikiwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kulisemea ni suala la leseni nyingi kwenye chombo kimoja. Sisi wavuvi boti ya kuvua ndiyo kama trekta kwa mkulima. Trekta kwa mkulima halina leseni sijui ya SUMATRA, n.k lakini mvuvi chombo chake cha kufanyia kazi anakata SUMATRA, lesseni ya boti, anakata leseni ya mwenye chombo, anakata leseni ya wavuvi, sisi ambao tunatumia vipe kule katika Ziwa Tanganyika unahitaji wavuvi sita kwenye kipe kimoja wote wanahitaji leseni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeeleza hapa kwamba inaangalia namna ambavyo italirekebisha jambo hili na pia hata leseni ambazo zinaweza kutumika kwenye zaidi ya halmashauri moja; na nimeona kwamba tayari GN namba 383 imeshatoka; lakini jambo ambalo naliomba Serikali ilifanyie kazi ni suala zima la kwamba hakuna haja ya chombo cha uvuvi kuwa na leseni kwa sababu leo hii hata road license tumetoa; road license tunailipa kwenye mafuta. Mvuvi anapokwenda kuvua ananunua mafuta! Kwa hiyo ina maana na yeye ameshalipia leseni yake moja kwa moja kama ambavyo mwenye trekta alivyo. Kwa hiyo kuna haja kubwa jambo hili liweze kuondolewa kwa sababu ni gharama kubwa kwa wavuvi na haliwezi kuwasaidia wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho, pamoja na marekebisho kadhaa ambayo yamefanywa na mapendekezo ambayo tumeyatoa ya tozo n.k. naomba Serikali inipe maelezo kidogo. Ukiangalia takwimu kutoka kwenye kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa utaona kwamba mwaka 2014 tuliuza nje bidhaa za mazao ya uvuvi ya thamani ya dola za Kimarekani million 832. Lakini tangu Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama Cha Mapinduzi iingie madarakani mauzo nje ya mazao ya uvuvi yameporomoka mpaka dola milioni 182 kutoka dola milioni 832 mwaka 2014, mwaka mmoja kabla Serikali hii haijaingia madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokiona kila siku na sifa kubwa ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inapata ni kuonekana wakiwa na njiti za viberiti wakiwa na mafuta wanachoma nyavu za wavuvi ilhali exports zetu kwenye mazao ya uvuvi zinazidi kuporomoka. Tunaomba Wizara hii itakapokuja kujibu hoja za Wabunge hapa waweze kutoa maelezo ya kina ni nini ambacho kinasababisha mauzo nje ya mazao ya samaki yanaporomoka tangu Serikali hii ya Awamu ya Tano iingie madarakani, ni kwasababu ya uchomaji wavuvi wamepungua, ni kwa sababu ya tozo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Kigoma pale kupata mgebuka imekuwa ni tatizo kwa sababu ya amri ambazo Serikali imekuwa inazitoa, mara msitumie vipi, mara msivulie sijui neti, mara msifanye nini. Kwa hiyo, wavuvi wanakuwa hawaelewi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia, kuna tatizo kati ya msimamizi wa Wizara, dada anaitwa Judith, mimi simfahamu, nimezungumza na wavuvi, hana mahusiano mazuri na wavuvi wa eneo lote la ukanda wa Ziwa Tanganyika. Naomba Wizara ifanye consideration kutazama, kwa sababu kuna measures ambazo wamezichukua, basi angalau na msimamizi aweze kubadilika, kwa sababu malalamiko ya wavuvi ni makubwa na tunahitaji wavuvi nao wajione ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa muda ambao umenipatia na hongera sana kwa kazi uliyoifanya leo asubuhi. (Makofi)