Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Maftaha Abdallah Nachuma

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu wataala na leo niweze kuongea machache haya kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza naomba nipate ufafanuzi kwa Waziri, Mheshimiwa Zitto kamalizia hapo kusema kwamba, kumekuwa na utaratibu wa Serikali kuchoma nyavu za wavuvi wadogowadogo na hasa maeneo ya ukanda huu wa pwani kutoka Mtwara, pale Mikindani, maeneo ya Kiyanga, lakini pia mpaka kule Kilwa, nyavu zimechomwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kufahamu hapa ni kwamba, wale waliochomewa nyavu zao, wao wanakuwa wamenunua zile nyavu madukani, naomba kujua kutoka kwenye Wizara hii, kwamba Serikali imechukua hatua gani mpaka hivi sasa, ama wanunuzi wangapi walioleta zile nyavu Tanzania wamekamatwa na wameshtakiwa na Wizara hii, badala ya kuwachomea wale wavuvi wadogowadogo ambao wanatafuta fedha kwa shida sana kupata zile fedha za kununua nyavu na mwisho wa siku wameenda kuwachomea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kujua, Mheshimiwa Waziri alipofika Kilwa, amefika Kilwa akawaita wavuvi wa Kilwa wote kwa maneno mazuri sana, akawaambia kwamba tunahitaji hivi sasa tuzungumze na nyinyi kama ndugu, kama rafiki, tunaomba nyavu zenu mzikusanye wenyewe kwa amani. Wale wavuvi wakazikusanya nyavu zao, Mheshimiwa Waziri akasema, nakwenda Dodoma, nakwenda Wizarani halafu nitarudi tena hizi nyavu tumezitunza, lakini anaondoka pale Kilwa, anafika baada ya kilomita tatu, nne, tano, anawaagiza watendaji, chomeni moto hizo nyavu, wakati aliwaahidi kwamba wazitunze! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kujua, kwa nini Mheshimiwa Waziri aliwahadaa wale wananchi akasema zile nyavu za milimita nane zitatunzwa halafu mwisho wa siku akatoka hatua mbili, tatu, akaagiza kwamba zile nyavu zichomwe moto pale Kilwa na wanachi wakawa na majonzi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kujua, kwamba kulikuwa na hii inaitwa Operation Jodari na Operation Sangala ambayo Wizara imekuwa inafanya kwenye maziwa makuu kule lakini pia kwenye Bahari ya Hindi kutoa Mtwara mpaka kule Kilwa na maeneo mengine yote mpaka kule Tanga na Zanzibar. Naomba kujua kwa sababu mwaka jana kuna kijana aliuawa pale Mtwara Mjini Kiyanga, mtu ambaye anakwenda kutafuta samaki kwa mikono, kwa kutumia mideki, akapigwa risasi ya kisogoni! Nikazungumza ndani ya Bunge hili, anaitwa Abdillah Abdulrahman, mkazi wa Kiyanga Mtwara Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikaeleza kwamba Serikali ichukue hatua juu ya huyu mtu aliyeuawa kwa kisingizio cha Operation Jodari ambacho kinafanyika kwenye Bahari ya Hindi. Mpaka leo sijapata majibu, naomba Mheshimiwa Mpina atupe majibu, kwamba yule kijana, ile roho iliyopotea mpaka leo Serikali imechukua hatua gani, kwa sababu hatujaona tume iliyoundwa, hatujaona chochote, hata kutoa pole Mheshimiwa Waziri, hajaja Mtwara kutoa pole, hata kama mimi nimezungumza humu, zaidi ya mara tatu, mara nne, mara tano ndani ya Bunge hili. Hata nikimsemesha, hata Waziri ukimsalimia, haitikii! Yaani leo ukikutana naye hapo nje, unamsalimia kwa ajili ya kujenga mahusiano, hata kuitikia imekuwa ni shida. Sasa kwa sababu Serikali hii ni sikivu sana, Mheshimiwa Rais anasalimia watu, tunasalimiana naye, Waziri Mkuu anasalimia watu, Mawaziri wengine wanasalimia, lakini Mheshimiwa Waziri Mpina, hata tukimsalimia, mimi mwenyewe zaidi ya mara tatu nimemsalimia anakaa kimya. Sasa, Waziri kama Waziri jambo la kwanza ni kujenga mahusiano na wale ambao unawaongoza, sasa Mheshimiwa Mpina, tunaomba atupe maelezo ya kina kwamba yule kijana aliyeuawa, zimechukuliwa hatua gani mpaka leo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba kujua, kwamba pale Mtwara kuna Chuo cha Uvuvi, chuo ambacho kimekuwa kinazungumzwa kila siku na nilimweleza Mheshimiwa Naibu Waziri hapo juzi, kwamba kile chuo lini kinaanza kazi, Chuo cha Mikindani cha Uvuvi. Pale tunaona kuna madawati yamewekwa, kuna meza zimewekwa lakini hakuna walimu, mpaka leo hawajaletwa walimu, hakuna kifaa chochote, hakuna hata Boti ambayo wale wanafunzi wakidahiliwa wataweza kuzitumia kwa ajili ya kwenda kufanyia mazoezi ya kuvua pale Mikindani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naishi Mikindani hapohapo kwenye chuo, niliambiwa kwamba kimeanza, kile chuo mpaka leo nazungumza na watu wa Mtwara hakijaanza. Sasa tunasema, tunataka tuvue uvuvi wenye tija, uvuvi ambao utapelekea Watanzania kujikomboa na umaskini na sisi wananchi wetu wa Pwani wengi ni wavuvi. Wananchi wangu wa Mtwara Mjini maeneo ya Kiyanga, maeneo ya Mikindani, wote ni wavuvi, wanategemea uvuvi katika Bahari ya Hindi ili waweze kujikwamua. Tunaomba kile chuo kifanye kazi isiwe kila mwaka, tunazungumza, tunaahidi lakini utekelezaji unakuwa haupo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naiomba sana Wizara hii, kwamba, ili tuweze kuvua uvuvi wenye tija, kama ilivyozungumza kwenye Ilani, kwenye nini, lakini pia Serikali inaahidi kila mwaka, lazima tuwe na vifaa vya kisasa vya kuvulia samaki, lazima tuwe na Boti za kisasa za kuvulia samaki. Wakati tuko Chuo Kikuu, mwaka 2008 pale, tuliweza kula samaki wengi sana, ambao Mheshimiwa Rais kipindi kile akiwa Waziri wa Wizara hii alikamata meli, wakaletwa wale samaki Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pale, tukala bure wiki nzima, kwa sababu tu wamevuliwa kitaalam, wale samaki walikuwa ni wengi. Tunaamini kwamba Serikali ikileta maboti, wananchi wetu wataweza kuvua kitaalam kuanzia Mtwara mpaka kule Kilwa, mpaka Dar es Salaam, Tanga na Zanzibar ili tuweze kuondokana na umasikini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.