Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buchosa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuchangia naomba nifanye declaration ya mambo matatu. La kwanza nimezaliwa nimekuwa na sasa nazeeka katika uvuvi, ufugaji na ukulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, nimebahatika sana kwa fadhira za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, lakini declaration ya tatu Jimbo ninalotoka mimi, asilimia 90 ya wakazi wa jimbo hilo ni wavuvi na asilimia 10 ni wafugaji. Kwa hiyo, haya ninayoyasema na ninayopanga kuyasema yanatokana na hiyo background ambayo nimeitaja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na sekta ya mifugo, hotuba ya Waziri nzuri, imejaribu kugusa changamoto ambazo wafugaji wa nchi hii wanapitia, lakini nishauri tu jambo moja, kama mtu ambaye pia nimewahi kukaa kwenye dawati alilopo. Suala la masoko ya masoko ya mazao ya mifugo, haliishii katika kujenga viwanda, kwa sababu hata vile vichache tulivyonavyo, uuzaji wa mazao hayo unakuwa wa tabu kwa sababu ya jambo moja, kwamba, eneo kubwa la ufugaji wa nchi hii halijawa huru kutokana na maradhi mbalimbali ya mifugo, hasa, homa ya mapafu na ile east cost fever. Haya maradhi mawili yanazuia uuzaji nje wa nyama ya Tanzania na namna pekee ya kuondokana na hili jambo, hiki kikwazo ni kwa kufanya chanjo kuwa ya lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, habari ya wafugaji kuchanja kwa hiari ndiyo inatufanya tuendelee kuwa kwenye hicho kibano, kwamba bado nchi yenu siyo disease free kwa hiyo, hatuwezi kupokea nyama yenu. Leo Jumuiya nzima ya Ulaya haipokei nyama kutoka Tanzania, Marekani haipokei nyama kutoka Tanzania na huko ndiko kwenye soko lenye bei kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, katika mazao ya mifugo ni hili la ngozi, nimesoma takwimu zilizopo katika kitabu cha hotuba ya Waziri, tunachinja ng’ombe wengi, lakini ngozi haitusaidii chochote, hasa wafugaji. Kwa nini haitusaidii, ile export levy iliyowekwa ya asilimia 80, wachakataji hawaitaki, kwa hiyo, hawalipi, lakini on the other side wakulima hawauzi ngozi! Sasa is a zero sum issue, mimi sijui kama Waziri wa Fedha ananisikiliza, hili jambo tunaishia na zero sum issue kwamba, wachakataji hawaji kununua hiyo ngozi na wakulima wafugaji hawana pa kuuza hiyo ngozi, kwa hiyo, ngozi yote inabaki ya kutupa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tunataka ku- protect au ku-discourage export ya ngozi, tufanye hivyo tutakapokuwa tumekwishajipanga, tuna viwanda vyetu vya kuchakata. Kwa hiyo, tuvilinde kwa kuweka masharti magumu ya kuondoa ngozi ghafi nje ya nchi. Vinginevyo, tunapoteza tu pande zote, viwanda havijengwi, ngozi haziuzwi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ninaloomba kuzungumzia leo, ni uvuvi wa Bahari Kuu. Huu uvuvi nao umekuwa kizunguzungu, nikiri kwamba nilifanya marekebisho makubwa ya kanuni, yameanza kutekelezwa baadhi na mengine hayajaanza kutekelezwa. Leo nilikuwa nazumgumza na Naibu Waziri wa Fedha, mpaka asubuhi ya leo, nchi hii, mwaka mzima, hatujaingiza hata senti tano inayotokana na uvuvi wa Bahari Kuu, sasa maana yake nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetunga sheria ili zitufanye tupoteze mapato au tumetunga sheria na kanuni ili zituingizie mapato? Naomba sana jambo hili lifanyiwe tafakari, ushuru ule wa mrabaha wa 0.4 dola kwa kilo moja, wadau wetu waliukataa. Tukakaa miezi minane bila ku-issue leseni hata moja, mpaka tulipo-rethink, tukasema hapana, hebu tuigawe hii issue, miezi sita wasilipe na miezi sita walipe, wakaja wavuvi 51 wakakata leseni. Sasa hili jambo lisipoangaliwa tunaendelea hivihivi kupoteza mapato wakati samaki wanapita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ikumbukwe kwamba samaki siyo kama dhahabu, kwamba iko kwenye shimo fulani Bulyang’hulu, haitoki pale milele na milele kama hujaigusa. Hawa samaki wanatembea, leo wako Mozambique, leo wako Tanzania, kesho wako Kenya, kesho kutwa wako Djibouti. Kwa hiyo, ukisema kwamba tunatunza maliasili hii sijui maliasili, hii siyo maliasili iliyo stagnant pale mahali, wanapita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, as we are speaking, hapo Djibouti na Kenya kuna meli zaidi ya 300, wanaendelea kusubiria samaki waki-cross Tanzania, wanavua. Sisi tunasema tunataka asilimia ngapi sijui, dola 0.4 kwa kilo moja ili tupate mrabaha. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, alitazame hili, Zanzibar wanalia, Zanzibar wanalia, huko natoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo hili la operations zinazoendelea katika maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Zitto amelizungumzia kidogo, lakini mimi naomba nilizungumzie kwa mantiki ile kwamba asilimia 90 ya wakazi ya jimbo langu ni wavuvi. Naunga mkono, asilimia mia moja kufanyika kwa hizo operations kwa wavuvi haramu, hilo naunga mkono kabisa, lakini siungi mkono kabisa, operations hizi kufanyika bila kzingatia sheria za nchi zilizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu kinachofanyika sasa hivi, mtu anakutwa amevunja Sheria ya Uvuvi, anapigwa faini za Sheria ya Mazingira na anayepiga faini hizo za Sheria ya Mazingira wala siyo Afisa Mazingira aliyesajiriwa. Nilizungumza na Mheshimiwa Makamba, nikamuuliza, hivi maafisa wako hawa, watumikaje katika kumkamata mtu na nyavu halafu akapigwa adhabu ya Sheria ya Mazingira, akasema hili haliruhusiwi na nikaenda kwenye sheria, ni kweli, hata Afisa Mazingira, siyo kila Afisa Mazingira anaruhusiwa kutoza faini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotokea ukienda leo, amekutwa na nyavu double mbili, double tatu, anapigwa faini ya shilingi milioni mbili. Ukiuliza, Sheria ya Mazingira, inahusika vipi na kiwango cha nyavu, hii Sheria ya Uvuvi ambayo faini yake haizidi shilingi laki mbili au kifungo cha miezi sita, lakini unakuta mtu amepigwa faini ya shilingi milioni mbili, milioni tatu. Sasa baya zaidi, Mheshimiwa Waziri, Maafisa wake hao, huo umekuwa ndiyo mwanya mkubwa wa rushwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si vizuri sana kumtaja mtu asiyekuwa ndani ya hili Bunge, si vizuri sana, kanuni zetu zinatuomba tuwe na tahadhali kuwataja watu wasiokuwa ndani ya Bunge, lakini yuko bwana mmoja, kiongozi wa shuguli hii ya operation kule Sengerema, ondokana naye huyo. Alikuwepo Ukerewe wa aina hiyo wakamhamishia kwa Mheshimiwa Zitto kule, sasa Mheshimiwa Zitto leo tayari anapiga kelele. Sasa huyu aliyeko Sengerema Mheshimiwa Mpina, amtoe tu, maafisa wako wengi sana wanaoweza kufanya kazi kwa uungwana bila kupaka Serikali picha mbaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, anamkuta mtu kakatiwa leseni na Halamshauri, mwandikaji wa leseni hiyo ni mtumishi wa Halmashauri, kakosea herufi moja kwenye jina, anamchukulia mitumbwi yake, anachukua engine anakwenda compound kule, anadai milioni moja faini kwa sababu ya jina la mtu limekosewa herufi moja! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, okay, nikawaambia basi anapowatoza hizo faini awaandikie na stakabadhi. Stakabadhi haandiki, kwa sababu anajua akiandika stakabadhi ya faini ya milioni moja kwa jina kukosewa atakuwa amevunja sheria, anachukua fedha hizi anaweka mfukoni. Sasa mimi sijui huyu ni mwizi au ni mla rushwa, vyovyote vile, lakini ni mtu anayevunja sheria za nchi. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Tizeba.
MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mbona umenikatili. Naunga mkono hoja. (Makofi)