Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Ninaze kwa kumpongeza sana mtoa hoja leo asubuhi Mheshimiwa Waziri pamoja na timu yako yote ndugu yangu Mheshimiwa Ulega, Katibu Mkuu na timu yote pale Wizarani. Nitaanza na ukurasa wa 77 wa kitabu cha leo. Mheshimiwa Waziri pale anasema zimetengwa shilingi milioni 153 kwa ajili ya mgao wa maduhuli katika vijiji ambavyo vipo katika hifadhi ya bahari katika Kisiwa cha Mafia. Matatizo yangu yanaanzia pale, nina mambo mawili pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, hizi milioni 153 zimeandikwa pale kwamba zinakwenda kwenye vijiji 17 na Mheshimiwa Waziri alikuja Mafia tukasomewa taarifa kule Jibondo, Hifadhi ya Bahari ipo katika vijiji 12 tu na vitongoji vitano, hiki kitabu leo kinasema hifadhi ya bahari iko katika vijiji 17, imenishtua sana, hizi takwimu Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku- wind up naomba sana atupe maelezo, pengine inawezekana ikawa ni typing error, lakini kama sio typing error, basi kuna tatizo kubwa sana, kwa sababu moja ya kilio cha watu wa Mafia ni kwamba hifadhi ya bahari imekuwa ikiongeza mipaka kila uchao. Vilianza vijiji vitatu, vikaja saba sasa vipo 12, leo kitabu kinatuambia vijiji 17. Sasa naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja atuambie, hivi vilivyoongezeka ni typing error au tayari himaya ya hifadhi ya bahari sasa imeongezeka tena kwa vijiji vingine. Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna mgao hapa, kuna taarifa njema ambayo nashukuru sana Mheshimiwa Waziri amesema kuna shilingi milioni 43 zitaendelea kwa ajili ya kutolewa mikopo kwa wanavijiji ambao wamo ndani ya hifadhi ya bahari, ni jambo jema nashukuru sana kwa niaba yao. Hata hivyo, nataka nitoe tahadhari namna ya mikopo hii itakavyotolewa, uwepo utaratibu mzuri sana. Huko nyuma mikopo ilitolewa nje ya utaratibu, matokeo yake fedha nyingi sana hazikwenda kwa walengwa. Kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, watu wa hifadhi ya bahari, bahati nzuri naamini wapo hapa, wajue mambo yatakapokwenda uwepo utaratibu mzuri ili kusiwe na matatizo yaliyotokea kabla ya hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika kitabu chake leo asubuhi hapa ukurasa wa 62, wameeleza vizuri sana na nampongeza sana, kwamba wanafanya mapitio ya Sheria ya Uvuvi, Namba 22, ni jambo jema sana na katika moja ya mambo ambayo alipokuja Mafia Mheshimiwa Waziri tulimlalamikia kwamba kuna mgongano baina ya Sheria ya Uvuvi Namba 22 na Sheria ya Hifadhi ya Bahari. Sasa kwa kilio hiki sasa kuna mambo matatu ningeomba sana Mheshimiwa Waziri ayatilie maanani katika mchakato wake wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, suala la ukubwa wa nyavu wametuambia samaki watavuliwa kwa nyavu za nchi tatu. Mheshimiwa Waziri alipokuja Jibondo pale alipotamka neno kwamba samaki watavuliwa kwa nyavu ya nchi tatu wananchi walianza kugunaguna kwa sababu kule kwetu kwenye bahari kuna samaki wengine kwa asili ya maumbile yao hawakui zaidi ya ukubwa wa nchi moja na nusu, samaki aina ya ngalala, tili, mbono, samaki wadogo ambao kimaumbile hata ukiwaacha miaka 50 hawawezi kukua.

Sasa wametuletea sheria na sisi tumetoa maoni katika hii sheria mpya wanapoweka nchi tatu kuna baadhi ya samaki kama hawa niliowataja ngalala, misusa, tili, mbono hawatovuliwa maisha kwa sababu tundu la nchi tatu atapita tu huyo samaki, kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri waliangalie na hao wataalam, namshukuru sana alipokuja Jibondo akatuachia wataalam waje kutoa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa taarifa yako watalaam wale wavuvi waliwaambia tunashukuru sana mmekuja kutupa elimu, lakini mara ijayo mtakapokuja mje na wataalam wenyewe hasa wa kwenda kuvua baharini, tutachukua nyavu ya nchi tatu, tutakwenda baharini pamoja halafu na sheria kwamba nyavu hairuhusiwi kufungwa mawe chini isiburuze chini ili hao wataalam waende wakaoneshe namna gani ya kumvua samaki, nyavu chini isiguse na nyavu hiyo ni ya nchi tatu, kama utampata samaki hata mmoja. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri kama utaalam upo wa kuvua samaki wa nchi tatu kwa kutumia nyavu bila nyavu kugusa chini, basi tunaomba sana atuletee wataalam hao kwa ajili ya shughuli hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nyavu za milimita…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Dau malizia.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nyavu za milimita nane za kuvulia dagaa, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri, ametaja kwenye kitabu chake watabadilisha kutoka kwenye milimita 10 kuja kwenye milimita nane, ni jambo jema na tunashukuru sana. Tunaomba sana taarifa hizi ziende kule chini kwa sababu bado kule wataalam watekelezaji wa sheria wanaendelea kuwasumbua wavuvi. Mheshimiwa Waziri dakika moja tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Uvuvi; hili ni jambo ambalo limezungumzwa sana humu. Namna pekee ya kuleta ukombozi katika uvuvi na kuongeza mapato ya Serikali tuwe na bandari yetu ya uvuvi na nashukuru kwenye kitabu hiki nimeiona bandari ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni lile alilolisema Mheshimiwa Tizeba, Mheshimiwa Waziri akaiangalie ile kanuni ya 0.4 kwa ajili ya uvuvi wa bahari kuu imewakimbiza wakubwa wote wale hawaji sasa hivi, kwa hiyo naomba sana kama watai- relax ile ili meli zile zije zivue kwa sababu ile DSFIA inakufa na inakufa kwa sababu hakuna mapato yoyote anayekuja kukata leseni kwenda kuvua katika bahari kuu kwa sababu gharama ile ya loyalty ya 0.4 wanaiona ni kubwa, iliwekwa kwa nia njema lakini bahati mbaya sana wenzetu hawa hawajakubali kutuletea meli. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Dau, muda umepita kwa kweli.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)