Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza naunga hoja mkono asilimia mia moja au zaidi ya mia mbili. Namuunga mkono Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Makatibu Wakuu, Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara hii inafanya kazi kubwa sana inasaidia wafugaji na wavuvi, kitu cha kushangaza kabisa utakuta Wabunge wengi hapa wanachangia kuisema Wizara ya Mifugo kwamba ndio inakamata mifugo ya wananchi. Kitu cha ajabu kabisa, mfugo unaingia National Park au Game Reserve anausikaje Mheshimiwa Waziri wa Mifugo kukamata ile mifugo, inakamatwa kwa sababu imefanya makosa imeingia kwenye National Park au Game Reserve. Mheshimiwa Waziri wa Mifugo hausiki, unakuta Mbunge anatoa na povu anasema Wizara ya Mifugo ndio inakamata mifugo, ni kitu cha ajabu kabisa sijaona. Unapochangia changia inapohusika kama huwezi kuchangia kaa kimya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi kweli Mheshimiwa Waziri, Maafisa Mifugo wanakamata mifugo au mifugo inakamatwa na Wizara ya Maliasili wakati inaingia kwenye National Park au Game Reserve, unapochangia changia hoja sio kuchangia against Wizara, kama huna uwezo wa kuchangia kaa kimya. Huwezi kuingiza kitu ambacho cha uongo na kuisema mpaka povu zinakutoka kitu cha aibu, kama hujui kaa kimya.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja na naisifu Wizara, nazungumzia habari ya uvuvi. Wizara ya Uvuvi tuzungumze ukweli kila mara nazungumza hapa, tuelimishe wavuvi wetu, sisi Wabunge tuna kazi vilevile ya kuelimisha wavuvi wetu. Mimi mara mbili nimekwenda Kituo cha Kipili wakati wanachoma nyavu nimezuia wasichome wasichome nyavu tukaenda nikapima zile nyavu, unakuta kweli nyavu ziko milimita nane halali, amechanganya na kipande cha milimita sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nyavu zinachanganywa, unakuta milimita sita, milimita nne wanachanganya nyavu, sasa utatetea wavuvi kwamba hawavui kiharamu, ndugu zangu tuseme ukweli, Serikali inafanya kazi ya ziada kulinda maliasili ya uvuvi. Haiwezekani sisi Wabunge tumekaa hapa, tunaisema Wizara ifanye kazi, iache wavuvi wafanye kazi wanavyotaka, wengine tuige mfano tuseme hata Congo kama Congo wanaharibu kule uvuvi wao haramu acha waharibu.

Mheshimiwa Spika, kuna nyavu zinatoka Congo zinakuja kwetu, tuziache? Nyavu zinatoka Burundi zinakuja kwetu, wanaita free mayai zinakuja wanavua kwetu, tunazikamata tunazichoma, hatuwezi kuita Serikali ya Congo au Serikali ya Burundi au Serikali ya Zambia haiwezekani! Kama anaharibu Congo na sisi aharibu huku kwetu, haiwezekani, hata kama samaki anatembea, acha atembee lakini haiwezekani na sisi tuingilie uharibu kama wanavyoharibu wenzetu haiwezekani! Kwanza ni dhambi kuvua visamaki vidogo vidogo hata Mwenyezi Mungu hapendi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishukuru Serikali, juzi tumekutana na Katibu Mkuu, ameruhusu ring net wavue, lakini lazima tuwashauri na wavuvi wetu wale wasitumie ring net chini ya milimita nane na uvuvi lazima wavue mita 300 toka mwambao wa Ziwa Tanganyika na wavue usiku sio mchana, haiwezekani tuache tu kwa sababu ya kuomba kura kwa wavuvi au kwa wafugaji, tuingie hapa Bungeni tuharibu mali yetu, haiwezekani. Tuwe wa kweli, hawa samaki sio mali yetu peke yetu humu ndani, vizazi na vizazi, mimi nina miaka zaidi ya 70, ingekuwa wanavua tangu zamani kama wanavovua samaki tungewakuta sisi, tungekuta masanamu ya samaki tu, tuwe wakweli bwana, mtu lazima afuate sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tufuate sheria inavyotaka ya kulinda mali yetu, ni mali yetu wote tumepewa na Mwenyezi Mungu, haiwezekani kutetea mvuvi ambaye anavua kiharama unatoa povu zako, haiwezekani kumtetea mfugaji anaharibu mazingira mpaka povu zako zinakutoka, fuata sharia. Unasema wewe anaingia mnyama, kwanza atapata magonjwa kwenye wanyama wale wa asili, tembo mle ndani wamo, mna simba na chui, unapeleka ng’ombe zako wakaharibu mazingira unataka wapeleke magonjwa ya sotoka mle ndani.

Mheshimiwa Spika, Rukwa kule wamegawiwa vitalu Kalambo Ranch, vitalu zaidi ya 20 wameuza vile vitalu, lakini ukienda mpaka leo ni miaka 10 wamegawiwa vile vitalu mpaka leo hawana ng’ombe mle ndani, walionunua vile vitalu mpaka sasa hawana ng’ombe, wanakodishia watu na ng’ombe chache.

Mheshimiwa Spika, juzi wamegawa vitalu vingine kula Kalambo Ranch kule wapeleke ng’ombe mle ndani kule kwenye Kalambo Ranch, lakini kuchunga hovyo halafu wanaingia Game Reserve, National Park wasiwakamate kwa vipi, halafu hilo swali wanapeleka Wizara ya Mifugo inahusika wapi? Haiusiki Wizara ya Mifugo ya Uvuvi, sijaona siku moja Afisa Mifugo akaenda kukamata ng’ombe National Park hata siku moja, sijaona mimi, wanaokamata ni watu wa TANAPA au watu wa Game Reserve, leo unachachamaa na povu linakutoka, unamshambulia na kwa jina, mnamtaja kabisa Mheshimiwa Mpina. Tulitegemea Mheshimiwa Mpina utatusaidia kwa sababu wewe unafuga ng’ombe, aaha imekuwaje! Biashara gani, haiji hata kidogo! Unategemea Mpina kwa kwa sababu ametoka kwenye kufuga asaidie ufugaji haramu. Mimi natoka kwenye uvuvi na ndugu yangu Mheshimiwa Ulega asaidie uvuvi haramu kwa sababu ni mvuvi, haiji! Ni lazima tufuate sheria ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusije hapa unatoa povu zako bure, kuwakashifu Waheshimiwa Mawaziri, kuwakashifu Makatibu Wakuu kwa sababu wewe unataka kura kwa wafugaji haramu na wavuvi haramu, haiji. Waambieni ukweli, waelimisheni wavuvi, haiwezekani mvuvi, nimeona kwa macho yangu kule anavulia chandarua, unategemea sasa utakuta mazalia ya samaki, chandarua!

Mheshimiwa Spika, mimi nimekamata mwenyewe vyandarua, mimi mwenyewe nampigia Bwana Samaki Kipili, naye amekuta vyandarua vinavua samaki. Kwa sababu najua hata kura wasiponipa potelea pote, kwani nimezaliwa kuwa Mbunge mimi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani, sikuzaliwa kuwa Mbunge, lazima tufuate haki. Haiwezekani kokoro likavua Ziwa Tanganyika, makokoro bado yapo na uvuvi haramu bado upo, naomba operesheni ziendelee. Operesheni lazima ziendelee uvuvi haramu bado upo lazima operesheni ziendelee, lakini operesheni za hekima na busara, lakini tusiache operesheni. Tusitegemee tuache operesheni kabisa samaki watakwisha. Haiwezekani, lazima operesheni ziendelee kwenye maziwa yote na bahari hizi zote, tusikubali.

Mheshimiwa Spika, kuna mabomu yanapigwa, wote mnasikia kuna mabomu yanapigwa. Kule kwangu zamani ilikuwa mabomu mpaka kuna watu wameathirika vidole miaka ya nyuma ya zamani, siku hizi ndiyo hakuna mambo ya mabomu, lakini wako mpaka waliokuwa wanakatika vidole, bomu linachelewa mkononi kwake, samaki unakuta wamelegea wote. Sasa hii ndugu zangu tukianza kutetea, tufuate haki.

Mheshimiwa Spika, hatukuja hapa sisi kwa ajili ya kura za kuombaomba, hapana. Kura zetu tumekuja hapa kutetea Serikali yetu na kutetea wavuvi wetu na wafugaji wetu kuwatetea; lakini wewe una-base upande mmoja tu kwa sababu wameletana hapa wanataka kusema aa, yule Mbunge ndiye mzuri tukampe kura katutetea sisi wafugaji na wafugaji na wavuvi, hapana. Lazima tuwawajibishe wavuvi wetu, kama milimita nane itumike milimita nane, lakini kama unachanganya milimita nane na milimita sita, yote umechanganya ni haramu. Huwezi kuweka kwenye sanduku lako umechanganya bangi na sigara, tumbaku, unasema ni halali, utakamatwa tu, yote ni bangi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mchango wagu ndio huu. Lazima tuelimishe wavuvi wetu, tuelimishe wafugaji wetu, tufuge kihekima na busara ili nchi yetu ipate kuendelea. (Makofi)