Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Stanslaus Shing'oma Mabula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nyamagana

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia walau machache kwenye hii Wizara muhimu kabisa, Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Spika, mimi naomba nijikite kwenye mambo machache ambayo kwa kweli nadhani yananipa deni sana kama sitayazungumza. Jambo la kwanza, wiki chache zilizopita nilizungumza juu ya masuala ya minada. Tunafahamu, kuna minada ya upili na minada ya msingi. Sasa miaka michache iliyopita Wizara iliamua kwa kukaa tu na kufikiria bila kuwa na sheria ambayo ingeweza kutuongoza vizuri, kwamba kwa sababu yako baadhi ya maeneo yana minada iliyokuwa inaendelea ilikuwa imejaa sana, sasa wakaamua kuhamisha ile minada kupeleka kwenye maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana watu wa Nyamagana na Ilemela kule minada yao ya msingi ikaondolewa na kupelekwa Misungwi ambapo wakaenda kuanzisha mnada wa upili. Matokeo yake ni nini; kuhamishwa huku kwa minada kulitokana na sababu za msingi tu kwamba maeneo ya awali yaliyokuwa yanatumiwa kwa minada, kama pale Nyamagana tulikuwa na eneo pale Igoma, kwamba eneo hili limekuwa finyu sana kwa hiyo ni lazima tuhamishe mnada. Hii imefanyika pia Pugu kwenda Ruvu na sisi tukatoka Nyamagana kwenda Misungwi.

Mheshimiwa Spika, lakini hoja yangu hapa ni nini; kulikuwa na sababu gani ya kuuhamisha mnada Nyamagana ukaenda Misungwi ilihali ule mnada ungeweza kutoka eneo ulilokuepo awali ukapelekwa kwenye eneo lingine. Nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri; sisi Nayamagana tuna eneo mbadala la zaidi ya ekari 35 mpaka 50, linatosha kwa ajili ya kupata mnada mpya wa msingi ambao utakuwa Nyamagana ili tuondoe hizi kero na changamoto tunazoziweka kwa wafanyabiashara.

Mheshimiwa Spika, nilisema hapa mfugaji au mchinjaji anakwenda kununua ng’ombe Magu, analipa 7,500 anapewa kibali kwenda Misungwi, anatoka Magu anapitiliza mpaka Misungwi, anafika Misungwi analipa 7,500 ndipo anapewa kibali kutoka Misungwi kuja kuchinja ng’ombe Nyamagana, hii siyo sawa. Tunaongeza mzigo kwa wavuvi, tunaongeza mzigo kwa wachinjaji na hatutawasaidia sana. Kwa hiyo niombe sana Wizara kwa sababu mlishaanza kulifanyia kazi, tunaomba mnada wetu uliokuwa unatakiwa urudi Nyamagana urudi ili tuweze kuendelea na shughuli za uchinjaji na mapato ambayo yaliyokuwa yanapotea kwa kiasi kikubwa sana.

Mheshimiwa Spika, la pili; tuna kiwanda cha ngozi pale Mwanza kinaitwa Mwanza Tanneries, imekuwa ni muda mrefu sasa tunakipiga kelele. Viko vyuo vya ngozi lakini watu hao hata wakimaliza mafunzo hawana sehemu za kwenda kujifunza. Mimi niombe Waziri ulichukue hili, Mwanza Tanneries ipo, majengo yapo, mitambo yote ilishaondolewa, hebu mliangalie na hili kama ni kutafuta wawekezaji watafuteni wawekezaji waje haraka tuendelee kunufaika na huyu mnyama anayeitwa ng’ombe na kadhalika kwa ajili ya ngozi hizi ambazo kwa kweli zitaweza kutuletea pato kubwa sana kwenye taifa letu.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie habari ya biashara ya mabondo; biashara hii ni kubwa sana, na Wachina wamejaa Mwanza wananunua mabondo. Bahati mbaya sana ni biashara ambayo haina bei elekezi. Mheshimiwa Waziri, inawezekana Wizara na Serikali inapoteza fedha nyingi sana. Mchina mabondo yakiwa mengi kabisa; maana hawa samaki Sangara wakati mwingine wanakufa tu na kiferezi huko kwenye maji, mabondo yanongezeka, akija Mchina haulizi bei, matokeo yake anashusha bei inakuwa ya kutupa kwa sababu mabondo yamekuwa mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hii haiwezi kuwa sahihi sana. Ni lazima tufike sehemu tuweke bei elekezi ili huyu anayechuuza na yeye kupata biashara hii asinyanyasike kwa sababu tu Serikali haijawawekea mwongozo lakini inataka kodi ya yale mabondo. Kwa hiyo lazima tuangalie maeneo yote mawili ili tuweze kumsaidia mvuvi, tuweze kumsaidia mtu anayefanya biashara ya mabondo, lakini tumuwekee mkakati huyu mfanyabiashara anayekuja kununua ajue msingi wa Serikali unataka nini kwenye biashara ya mabondo.

Mheshimiwa Spika, liko lingine, hili nafikiri baada ya Wizara kuwasilisha hii bajeti nitamwona Mheshimiwa Waziri nimletee na hawa watu, walinyanyasika sana na mzigo wao mkubwa wamedhulumiwa, lakini kila wakifuatilia baada ya maamuzi ya Mahakama wanachukuliwa hatua, inakuwa kama ni kazi ya uhasama. Sidhani kama ni vyema kulisema hapa, lakini nalisema kama brief, halafu nitamtafuta Waziri na hawa watu ili aweze kuzungumza nao.

Mheshimiwa Spika, lingine, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwenye suala la uvuvi wa samaki, kiukweli wamefanya kazi kubwa. Jambo lililopo sasa la uamuzi wa kutoka kwenye sentimita 50 kwenda 85 kwa kuamua kuiruhusu 85 hata kama itafika sentimita 200, huu ndiyo uamuzi mzuri na nampongeza sana Mheshimiwa Waziri. Tunataka kama hivi jambo limetokea wamechukua hatua wamekaa wamefikiria wakaamua kwa ajili ya maslahi ya watu, hongera sana, samaki huyu mwenye sentimita 85 na kuendelea ndiyo mwenye soko na ndiye anayelipa kuliko Waziri anavyofikiria.

Mheshimiwa Spika, lingine ni suala la nyavu, sote tunafahamu kwenye suala la nyavu, nyavu za dagaa pamoja na nyavu za sangara ambazo ni milimita nane mpaka milimita sita. Kwenye nyavu za sangara Waziri ameshafanya utafiti zaidi ya mara mbili na jambo moja kubwa tunaona kwamba nyavu za single, maana kuna double na single, nyavu za single ni ukweli kwamba pamoja na tafiti mbili alizozifanya Waziri, inaonekana bado haziwasaidii wavuvi kufikia malengo waliyoyakusudia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwombe Mheshimiwa Waziri turudi pale kwenye double wala asikate tama, arudi pale kwenye double ili wavuvi kulingana na mawazo wanayoyatoa kwa sababu ndiyo wako kwenye field, ataona matokeo yake, Serikali itapata fedha, samaki anazozitaka zitapatikana, vipimo vilivyokadiriwa vitapatikana na tutakuwa hatuna tatizo kabisa.

Mheshimiwa Spika, zaidi ya yote nafahamu sasa hivi Mheshimiwa Waziri anafikiria kuwa na pie kati ya sita au saba, hebu nimwombe tusimame kwenye six pie au turudi chini kuliko kwenda kwenye…

SPIKA: Malizia Mheshimiwa Mabula, dakika moja.

MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Spika, hizi zinaweza zikatusumbua sana kwa sababu mzigo utaenda kwa wavuvi na sio kwa watu wengine.

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana, nafikiri kwa leo hayo machache yanatosha, naunga mkono hoja kwa asilimia mia na Mungu awabariki sana. (Makofi)