Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. John John Mnyika

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi inapaswa kushirikiana na Wizara ya Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhakikisha kwamba mipango kabambe (master plan) za kila Jiji, Manispaa na Wilaya zinalenga maeneo ambayo ufugaji na uvuvi unaweza kufanyika ili kuepusha migogoro na kuhakikisha uendelevu. Katika muktadha huo niombe katika majumuisho Wizara ieleze iwapo ilipewa nakala ya master plan ya Jiji la Dar es Salam na iwapo imeshatoa maoni ya kuboresha master plan ya Jiji mintarafu masuala na mipango ya mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Spika, Jiji la Dar es Salam ni mtaji mkuu wa uvuvi kwa upande wa nchi yetu ya Tanzania, hata hivyo yamekuwepo malalamiko ya kuletwa kwa samaki wa sato na aina nyingine kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa chini ya kiwango. Aidha, hata kwa samaki ambao wamekuwa wakifugwa kwenye mabwawa wamekuwa wakipewa muda wa wengi na kuwa baadhi ya kuku aina ya broilers. Hivyo, Wizara iwe na mikakati thabiti ya kudhibiti ubora wa samaki kutoka nje ya nchi na ubora wa samaki wanaofugwa katika mabwawa.

Mheshimiwa Spika, katika hotuba ya Waziri yametolewa maelezo kuhusu utatuzi wa migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ambayo yanaonyesha bado Serikali haijawezesha utatuzi kamili na endelevu wa migogoro hiyo. Hivyo, katika majumuisho ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi iwasilishe Bungeni taarifa juu ya utatuzi wa migogoro yenye kuorodhesha migogoro iliyopo na kwa maeneo ambayo migogoro haijatatuliwa bado iwekewe road map ya utatuzi wa migogoro hiyo ambayo pamoja na mambo mengine itaeleza ni lini migogoro hiyo ikatatuliwa. Pia Wizara ya Fedha kwa kuwa suala hili ni mtambuka ieleze ni lini itaongeza fedha kwa Wizara zote zenye mipango ya upimaji wa ardhi ili kuwezesha ardhi ya nchi yetu kupimwa na kupangwa kwa ajili ya maendeleo endelevu ikiwemo ya mifugo na uvuvi nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine naomba kupitia mchango huu Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) itenge eneo katika ardhi yake ya Mkoa wa Pwani kwa ajili ya vijana wa Jimbo la Kibamba kulitumia kwa ajili ya ufugaji ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuongeza ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Spika, suala lingine muhimu kupewa kipaumbele ni nafasi ya Bodi ya Maziwa katika kuhamasisha unywaji wa maziwa ikiwemo kwa wanafunzi wa shule mbalimbali. Hivyo, naomba Bodi itekeleze kampeni maalum katika Shule za umma za msingi na sekondari katika Jimbo la Kibamba ya kuhamasisha wanafunzi kunywa maziwa kwa kushirikiana na wasindikaji mbalimbali wa maziwa.