Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. James Kinyasi Millya

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Simanjiro

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JAMES K. MILLYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kuwapongeza watumishi wa Wizara wakiongozwa na Mheshimiwa Waziri wetu Dkt. Kigwangala kwa kazi kubwa wanayofanya kufufua na kuendeleza sekta hii ya utalii nchini mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikia kidogo hoja za wenzetu, mtu anasema kwa kawaida miaka yote tumekuwa tukipokea watalii kutoka nchi ya Israel kila msimu, unapata shida kidogo kwa sababu mtu hataki kusifia yale mazuri yanayofanywa kwa wakati huu. Kama hivyo ndivyo, kwa nini mtu asigusie watalii takriban 340 waliofika juzi wa kutoka China? Hili ni eneo jipya ambalo hatukuwa nalo, Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wamefanya vizuri na uongozi wa nchi hii. Tungeona watu waungwana wataje na hayo. Kwamba siyo lazima utaje ya Russia au utaje mahali pengine kama Ukraine, taja na China kwamba hili ni soko kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mheshimiwa Waziri kwa kuboresha kidogo hilo, ningeomba ushirikishe balozi zetu nchini. Balozi zote zilizopo mataifa mengine ya nje watuandalie ili watu wetu wanaofanya utalii hapa ndani kama Arusha au maeneo mengine tuwapeleke na wafanyabiashara wakakutane na wale ambao wanauza biashara ya utalii duniani kote wakutane na watu kama ambavyo nchi ya Kenya inafanya mara nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, niongelee hoja kubwa aliyofanya Mheshimiwa Rais. Vijiji vyetu vya wafugaji kwa miaka mingi sana baada ya uhuru na hata wakati wa uhuru na Mheshimiwa Waziri umegusia kwenye hotuba yako. Tumeumia muda mrefu kwa miaka mingi, Mheshimiwa Rais baada ya kusikia kilio cha vijiji takriban 350 nchi hii, akaamua kuelekeza Wizara karibu nane zikae pamoja na akawatuma Mawaziri kila mahali, walifika Kimotoro Mawaziri nane. Nia ya Mheshimiwa Rais ni kutatua hii hali iliyokuwepo ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona wenzetu wakiendelea kuuliza hivi itawezekana kufanyika kweli? Nia ya Mheshimiwa Rais ni njema, niombe sasa Wizara yako Mheshimiwa Waziri msukume jambo hili ili lisijelikawa ni jambo ambalo halitatekelezeka, wananchi wanasubiri kwa hamu Kimotoro, Simanjiro na nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma vizuri hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani ukurasa wa 18 na 19; wenzetu bado hawaweki imani kwamba Serikali hii ni Serikali ambayo haiongei tu bali inatenda na hizi zote ni sifa za Mheshimiwa Rais. Ukiona kwenye hotuba yao wanagusia suala la Stiegler’s Gorge; Serikali inataka umeme wa kutosha. Wanaongelea pia suala la hizi hifadhi, kwamba kwa nini tumege eneo fulani la hifadhi halafu tuwape wananchi; wenzetu mmeuliza tayari SGR tunafanya nini? Mnauliza bado masuala ya ndege. Mimi niseme kitu kimoja, nimepata bahati ya kupanda ndege hizi mpya za Serikali, ni ndege za kisasa zitatuongezea utalii na nimeambiwa kuanzia mwezi ujao mtaanza kwenda India na Afrika ya Kusini, huu ni mwanzo mzuri sana. Na crew yetu mimi nilivyoisikiliza kwa uzoefu wangu wa masuala ya ndege, ni crew nzuri, tutaongeza utalii kwenye nchi hii na Mungu aendelee kuwabariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kitu kimoja, nchini Ghana baada ya kupata uhuru, Kwame Nkurumah alianzisha miradi mikubwa sana. Tulipata wasaliti waliompinga Kwame Nkurumah wakati ule. Lakini mnakumbuka pia katika ukombozi wa Congo, wakati Congo inakombolewa kulikuwa na mtu anaitwa Patrice Lumumba akatokea msaliti mmoja anaitwa Moise Tshombe wakati wa kugawa Jimbo la Katanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasaliti duniani hawakosekani wala Mheshimiwa Rais asiache kufanya miradi mikubwa ya kusaidia nchi kwa sababu ya kusikiliza kelele za wale ambao hawatakii mema nchi hii, aendelee kupambana na sisi wengine ambao tupo upande huu, tunajua anafanya mema kwa ajili ya nchi hii, tupo tayari kusaidia Taifa hili na tutamuunga mkono Mheshimiwa Rais. Kwa hiyo, na Mheshimiwa Dkt. Kigwangala usitishwe na maneno yoyote ya watu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nigusie suala la Makumbusho ya Taifa letu. Ninaomba Mheshimiwa Waziri, bajeti tunayotenga ni ndogo sana, Makumbusho ya Taifa yanaisaidia Serikali na sisi Watanzania kuhifadhi kumbukumbu ya leo, kesho na miaka ijayo. Inawezekana mambo mengine yanafanyika kwa sababu ya kutaka kutufurahisha tulioko duniani sasa, tuna watoto na wajukuu wanaokuja keshokutwa wanataka kujua Tanzania imetoka wapi, inaenda wapi na miaka mingine inaenda wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri, bajeti ya makumbusho iongezwe, ni ndogo kweli. Hii ni taasisi muhimu ambayo haipigiwi kelele mara nyingi. Mimi nimepata bahati ya kuzunguka kwenye makumbusho mbalimbali, kuna makumbusho mazuri sana duniani, naomba usaidie ya kwetu, ya kwetu ipo hoi bin taaban. Ninaomba Mheshimiwa Waziri unapokuja kuhitimisha hoja yako ugusie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lingine ni Kuhusu Ujangili. Nimeona umesifiwa kuhusu ujangili. Mimi Simanjiro nimepata ujumbe jana, wafugaji wanalalamika kuhusu ujangili, ujangili umeongezeka Simanjiro eneo la Terat, Sukro mpaka Kimotoro, ninaomba usaidie. Lakini nimesikia kwenye hotuba yako umeongea mambo mazuri, umesema unaanzisha hunting blocks tena na unagawa vibali vipya, hilo litasaidia kwa sababu kwa kugawa hunting blocks, wale ambao umewapa hunting block watasaidia kushirikiana na Serikali kulinda wanyamapori wasiuwawe. Wachungaji wetu wa Simanjiro wanashindwa kuchunga kwa sababu wanahisi wanaweza kupigwa risasi na majangili, ninaomba muongeze taskforce ile National Taskforce ya Anti-poaching ipelekwe Simanjiro sasa hivi wanyama wanauwawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la fidia. Hatuwezi kumfidia binadamu, juzi Simanjiro kijana mmoja mtoto wa shule ya sekondari alienda machungani akauwawa na tembo. Ninaomba msaidie mfikirie kuleta sheria hapa Bungeni tubadilishe at least tupate kidogo kifuta machozi kizuri. Mngechukua mila zetu za kifugaji za Kimasai, mtu akiuwawa kwa namna yoyote bahati mbaya, sisi tulikuwa tunatoa fidia mpaka ng’ombe 49.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba mfikirie ni namna gani basi, kwa sababu katika mila za Kiafrika, mimi ninavyofahamu kama wafugaji wa Kimasai, mtoto ni kama kiiunua mgongo cha mzazi, akishaondoka binadamu mtu unamtegemea ni mtoto wako. Ninaomba msaidie hili suala la fidia mlirekebishe kidogo, halijakaa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kuna lingine, kuna mfugaji wa Morogoro, Game Reserve ya Matambwe aliuwawa ng’ombe wake 200 kwa kupigwa risasi na watumishi wa Wizara yako mwaka 2015, ametozwa faini lakini bado maaskari wale wakapiga risasi; ninao ushahidi hapa maaskari wa wanyamapori wakipiga ng’ombe 200 risasi; mpaka leo mfugaji yule hajapewa fidia yoyote, hajaangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Mheshimiwa Waziri nitakuletea ushahidi huu wote uwasadie, nina majina ya hawa walioamuru ng’ombe hawa wapigwe risasi. Jina la huyu aliyepiga risasi na mtu aliyechukua video lakini naomba kwa muktadha wa hoja hii nisitaje majina yake lakini nitakuletea ili wewe kama kiongozi wetu wa kisiasa katika Wizara usaidie hilo lipatikane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala ya ujirani mwema. Asilimia 70 ya wanyamapori wako nje ya hifadhi, tunawatunza sisi lakini hatuoni faida gani mnatupa kama kuchimba maji, hospitali, kuhudumia shule mnatoa kidogo sana. Mheshimiwa Waziri naombeni mfikirie kwenye Wizara yako ili hili tupate na lenyewe kwa sababu mkitushirikisha tukapata faida ya wanyama hawa, tutawatunza kwa sababu tunaona faida yao, ninaomba Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niunge mkono hoja, kwamba unafanya kazi nzuri kwa kweli Wizara haipo kama ilivyokuwa mara ya kwanza, hizi sifa tukupe na Serikali imejitahidi sana. Baada ya kusema hayo nawatakia heri katika utekelezaji wa majukumu yenu, ahsante sana. (Makofi)