Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Catherine Valentine Magige

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kufanikiwa kudhibiti ujangili katika nchi yetu. Tumeshuhudia Waziri wa Maliasili na Utalii Mheshimiwa Dkt. Hamis Kigwangala akizunguka nchi nzima, siku 48 pori kwa pori. Nilifuatilia katika Gazeti la Mwananchi, walifanya tathmini, walisema Mheshimiwa Kigwangala amezunguka kilometa 28,000. Mimi mwenyewe nilikuwa nikiangalia najiuliza huyu mtu ni wa namna gani? Kwa kweli Mheshimiwa Kigwangala anastahili pongezi, amefanya kazi kubwa sana; anamsaidia Mhehsimiwa Rais na vilevile hata Watanzania na sisi wenyewe tunamuona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tembo wanaongezeka kwa wingi, wanaendelea kuzaliana, ujangili umepungua. Zamani ilikuwa hata tembo akifa bahati mbaya, unakuta majangili wameshachukua meno ya tembo lakini sasa hivi tembo akifa tunakuta meno kama yalivyo, ina maana ni Wizara imejitahidi sana kupunguza ujangili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuanzisha Jeshi Usu kwa ajili ya misitu na wanyamapori. Sasa hivi wanyama na misitu yetu ipo salama. Vilevile nawapongeza kwa kuanzisha kikosi kazi kwa ajili ya kudhibiti ujangili na ndiyo maana siku hizi hatusikii tena habari za ujangili kama ilivyokuwa hapo nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, idadi ya watalii inaendelea kuongezeka kila siku, yaani watalii wanaendelea kumwagika katika nchi yetu; zote hizi ni jitihada za Wizara ya Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Waziri, watendaji wake na taasisi zake mbalimbali. Hivi karibuni hapa tumeshuhudia meli ya watalii 2,500, ndege ya Waisraeli1,000 na Wachina 343, wote hawa wanapokuja katika nchi yetu wanaondoka wanarudi huko, wakisharudi fikiria kila mmoja aliyekuja huku akifika katika nchi yake anawaambia watu wangapi na wanatangaza Tanzania kwa namna ama nyingine; wanatangaza vivutio vyetu kwa namna moja ama nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijielekeze katika Mkoa wangu wa Arusha kwa wafanyabiashara wa hoteli za kitalii. Wafanyabiashara hawa wamekuwa wanatozwa bed night levy kwa siku ambapo wanalipa dola moja na nusu. Nayo haijalishi kwa hoteli ambayo labda inachaji dola 150 au 200 kwa siku, au hata ile hoteli ndogo ambayo inachaji kwa siku 40,000, wote wanalipa sawa. Kitu hiki kimekuwa kikiwaumiza sana wafanyabiashara wa mahoteli, kwa sababu inawezekanaje mtu ambaye anachaji mtu kulala kwa siku dola 250 na mwingine 40,000 wakalipa sawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri alikuja Arusha, alikutana na wadau wa utalii walimwambia, lakini kipindi kile nadhani alishindwa kuamua labda kwa sababu tulikuwa hatujaenda kwenye bajeti. Sasa Mheshimiwa Waziri ndiyo wakati muafaka, wafanyabiashara wa utalii wanamwamini sana na wamesema nimfikishie hili na wana imani kubwa na yeye na atalitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iendelee kuangalia mazingira ya Ziwa Manyara; kina kinapungua na tunajua kuwa Ziwa Manyara lina ndege wazuri sana ambao ni kivutio cha watalii wengi, ndege aina ya flamingo. Kwa hiyo kina hiki kinapopungua ndege watapotea na tutakosa watalii. Naomba sana Serikali iangalie kwa karibu ili tusije tukapata hasara ya kupoteza ndege aina ya flamingo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali iangalie mazingira ya Ngorongoro kwa sababu Ngorongoro magugu yanaharibu mazingira, wanyama wadogowadogo wanakosa chakula, wanakufa. Serikali ifanye utafiti namna ya kukabiliana na changamoto ya mmea vamizi kwenye Hifadhi ya Ngorongoro ambao ni urithi wetu wa dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wangu wa Arusha, eneo la Ngorongoro kuna shule moja ya wasichana ilitakiwa kujengwa katika Kata ya Alaitole, eneo la Isere. Shule hii wananchi wamejitahidi wamekusanya mawe, wamekusanya mchanga, halmashauri imetupa milioni 288, lakini mpaka sasa hivi Ngorongoro hawajatoa kibali cha kujenga shule hii. Akinamama wamekuwa wakilalamika, hata wiki iliyopita waliandamana, akinamama wanataka watoto wao waende shule, lakini hatujajua ni kwa nini wanazuiwa kujenga, mpaka sasa hivi hawajapata kibali kutoka hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mashaka na Mheshimiwa Waziri, vilevile na watu wa Ngorongoro. Naomba ikiwezekana tukutane twende tukasikilize hasa kuna changamoto gani ili tuangalie ni jinsi gani akina mama hawa watasaidiwa watoto wao waende shule. Tunajua Mheshimiwa Rais anasisitiza watoto wasome na akinamama hawa wanataka watoto wao waende shule na ndiyo maana juzi waliandamana kwa uchungu mkubwa sana. Naomba sana Mheshimiwa Waziri alichukue hili na alifanyie kazi ili shule hii iweze kujengwa na watoto wetu waweze kwenda shule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri na watendaji wa Wizara yake kwa kazi nzuri sana wanayofanya ya kuhakikisha nchi yetu inanufaika na vivutio vya utalii tulivyonavyo. Nawapongeza sana kwa mkakati wa ku- rebrand nchi yetu kupitia kaulimbiu ya Tanzania Unforgettable. Hili ni jambo zuri na muhimu katika kutangaza nchi yetu na kuingia katika ushindani wa Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, lazima kufanya kazi ya ziada ili kweli kauli hii iwe ya maana na iwe kauli endelevu. Hii ni kuhakikisha kwamba tunapokwenda kila mahali Watanzania wanaitangaza Tanzania Unforgettable; timu zetu za Tanzania zinabeba Tanzania Unforgettable; wasanii wetu wanabeba, hata Mawaziri wetu wanapokwenda kwenye mikutano ya Kimataifa wanaibeba hii Tanzania Unforgettable. Vilevile hii siyo kazi ya Wizara ya Maliasili tu, ila Wizara ya Maliasili ni kama wenyewe wana- coordinate, lakini tunatakiwa Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposema hivi inawezekana hata Wabunge wengi hawaelewi maana yake, hata Mawaziri, inawezekana asilimia 90 hawaelewi, wanahitaji kueleweshwa na kufahamishwa ili tunapoongea Tanzania Unforgettable kila mahali iwe ni kwa ajili ya Watanzania wote, siyo Wizara tu, tuitangaze kila mahali. Tanzania Unforgettable ni experience itakayopata watalii au mgeni kutoka kutangaza. Mfano, mgeni anapofika tunaangalia ni jinsi gani mazingira ya immigration wamempokea mgeni, wamemkaribishaje. Hiyo nayo ni Tanzania Unforgettable, akitoka anakwenda kuitangaza Tanzania. Tunaangalia amepokelewaje kwenye hoteli, amepataje usafiri, usalama wa mgeni, akitoka katika njia salama anakwenda kuiongelea vizuri nchi yetu, tunaangalia mambo mengi kuhusiana na hii. Au njia rahisi za mtu hata kufanya biashara Tanzania, vilevile akitoka anakwenda kuiongelea Tanzania vizuri. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri aliangalie hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kukupongeza, unajitahidi sana pamoja na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara. Naomba atakapokuja kujibu anijibu kuhusiana na hii shule, maana akinamama kule wanapata shida, wanafuatilia kuhusiana na hii shule. Vilevile na wafanyabishara wa middle class hotels wa Arusha; naomba anijibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante. (Makofi)