Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla, Naibu wake na watendaji wote wa ofisi yake. Kwa kweli wanafanya kazi nzuri sana, unaweza kusema sasa Wizara imepata viongozi na sio viongozi wamepata Wizara. Hongereni sana kwa kazi nzuri. Tumeona kuna mabadiliko mengi ongezeko la watalii na mambo mbalimbali. Kwa kweli hongereni sana tunawaombea kwa mwenyenzi Mungu aweze kuwazidishia afaya muweze kuitendae haki nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo ambayo yanaweza wakati mwingine yakafanywa na watu chini yake na si yeye ni vyema kabisa tukamweleza japo kuwa nimeeleza kwa njia moja au nyingine, nimeona leo hii nirudie. Upo mgogoro mkubwa sana kati ya wavuvi wa Ziwa Rukwa na watu wa Maliasili wa Uwanda wa Game Reserve. Hii uwanda wa Game Reserve miaka ya 60 ilikuwa na squire kilometre 5,000, lakini baada ziwa kupanuka limemeza uwanda mkubwa wa game reserve limemeza karibu kilomita 4,100. Kwa hiyo nchi kavu ya Uwanda Game Reserve ishabakia na kilomita 490, kwa hiyo, sehemu yote ni ziwa
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wapo wavuvi kutoka maeneo mbalimbali au kutoka mikoa mbalimbali ambao wanaenda kutafuta riziki katika maeneo yale na wanapoingia wanakata leseni za biashara, wanakata leseni za mitumbwi, wanakata leseni za uvuvi, wanakata leseni za mazao ya samaki. Wanaingia kwa njia halali, lakini hawa watu wanasurubishwa, wanakamatwa, wanaharibiwa vyombo vyao utadhani sio Watanzania, utadhani hawalipi kodi. Mgogoro huu ninaozungumza ni mkubwa sana umefika mahali ambapo kama Wizara haitachukua hatua utaleta mgongano mkubwa sana kwa sababu, watu wanaohusika na uvuvi ni watu wa uvuvi. lakini maliasili wameingilia kati kuwa-harass wavuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule wanaenda akinamama wajane, vijana wanaotoka vyuoni wanakwenda kujipatia riziki, lakini wanakamatwa. Mpaka saa hivi kuna engine kama tisa zimenyang’anywa, boti 30, engine 17 zimepasuliwa, na engine mbili zimechomwa katika Forodha ya Nankanga na Ilanga. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri alifuatie jambo hili. Niliongea na Mheshimiwa Kanyasu, sikuongea na Mheshimiwa Waziri, akanimbia atakwenda kuongea na wavuvi aone kulikoni na vilevile katibu Mkuu nimeongea naye, nashangaa mpaka sasa hivi sijaona hatua zozote. Kwa hiyo naomba sana najua amekuja kwangu mara ya kwanza, alifanya kazi nzuri sana na alisharejesha nidhamu, lakini katika hili namwomba tena atafute namna ya kwenda kuumaliza mgogoro huu, wavuvi wanapata tabu sana. wananyanyaswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikwambie wakati fulani wale watendaji wadogo wanachukua rushwa, kama huna hela unaonekana sio mtu, ukitoa hela wanakuachia tu, wanakuachia uendelee kufanya shughuli zako. Ndugu zangu wapo akinamama wajane wanaenda kujitafutia riziki, lazima ifikie mahali tuwe na ubinadamu. Kama Mheshimiwa Rais anaweza kuwa na huruma ya kusema tuangalie mapori yale ya akiba, tuwasaidie wafugaji na wakulima, sasa itakuwa eneo ambalo lipo ndani ya maji ambalo ni kwa ajili ya wavuvi. Tufike mahali wakati mwingine tuangalie mwelekeo na huruma ya Rais wetu na tumuunge mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka hili nilisisitize sana sana hasa kule Ilanga, Ilanga ipo karibu na reserve ya Lukwati. Sasa watu wanaingia kuvua wanakamatwa, wananyang’anywa vifaa, wanapelekwa Mpanda, wanaambiwa kung’oka hapa ni mpaka milioni mbili. Kwa kweli wanawa-harras vibaya sana. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri anisikilize vizuri na jambo hili alifuatilie, naona kama hanisikilizi vizuri anashika makaratasi. Jambo hili litaleta matatizo makubwa sana, naomba anisikilize na alifuatilie, wakati anatoa majumuisho alitolee uamuzi. Hizi engine ambazo zimekatwa wazirejeshe, wameziweka tu boti, engine za watu, wamerundika kwenye stoo zao zinafanya kazi gani? Tunaomba Waziri atoe tamko la kurejesha vifaa hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nataka nimkumbushe Mheshimiwa Waziri, alipokuja kule kwenye jimbo langu aliahidi kusaidia ile Zahanati ya Maleza ili iweze kumalizika na aliwaahidi kuwachimbia kisima cha maji. Pia wakati Mheshimiwa Profesa Maghembe akiwa Waziri, naye aliwaahidi Kijiji cha Kilangawana kuwapatia mabati 100. Hii ni ahadi ya Wizara, hata kama hayupo tunaamini kwamba Wizara ipo na Waziri yupo, tunaomba atusaidie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni wingi wa mamba katika Ziwa Rukwa. Ziwa hili lina mamba wengi sana hakuna mwaka ambao mambo hawajala watu zaidi wawili watatu. Wanakula watu na wengine wanajeruhiwa, wengine wanakatika miguu, wengine mikono, ni kigugumizi gani kinafanya wasipunguzwe mamba katika hili Ziwa Rukwa? Mamba wapunguzwe, si ni biashara, wanaweza wakafanyiwa biashara ya ngozi, kuliko waendelee kula binadamu, kuwapunguza binadamu na kupunguza nguvu kazi. Ningeomba sana katika suala hili Mheshimiwa Waziri aweze kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nirudie kumpongeza Mheshimiwa Waziri, anafanya kazi vizuri na Manaibu wake isipokuwa hawa watu wa chini ndio wanaweka doa katika Wizara hii. Tunaomba sana sana ufuatilie wavuvi hawa warudishiwe haki zao na ikiwezekana Wizara ya Maliasili na Wizara ya Uvuvi wakutane wajadili namna ya watu, wanaoenda kuvua ziwani kwa nini wanakamatwa? Ile ni ajira, wasione vijana tu, hata wa chuo kikuu wanakimbilia ziwani na lile ziwa linachukua mikoa mingi. Ukienda watu wa Mbeya, Songwe wapo kule hata watu wake wa Tabora akija atawakuta, hata watu wa Katavi wapo kule wanajitafuta riziki, tuwasaidie vijana hawa na wananchi hawa waweze kupata riziki na bahati nzuri wanalipa kodi, hawana matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)