Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi ninashukuru kwa kupata fursa ya kutoa mchango wangu kidogo katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara muhimu kabisa katika nchi na nchi yoyote ile duniani. Ukitazama kipimo cha maendeleo (Human Development Index) theluthi mbili zinachukuliwa na elimu na afya (afya theluthi moja, elimu theluthi moja).
Kwa hiyo, tukiweza kutatua matatizo haya mawili, afya na elimu, maana yake ni kwamba tunakuwa tumetatua theluthi mbili ya changamoto zetu za maendeleo katika nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wenzangu wazungumzia falsafa tuliyokuwa nayo, falsafa ya elimu ya kujitegemea na mimi swali ambalo ninapenda tujiulize sisi kama nchi, falsafa yetu ya elimu sasa ni nini? Tunataka tuzalishe watoto wa namna gani? Tunataka tujenge Taifa la namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunazungumzia viwanda, lakini tunajua hali yetu ya elimu ilivyo. Watoto ambao tunawazalisha sasa wataendana na Tanzania ya viwanda ambayo tunataka kuijenga? Haya ni maswali ambayo tusipopata majibu yake humu Bungeni kwa miaka mitano tutakuwa tunakuja, tunazungumza, tunapitisha bajeti, tunaondoka hali inabaki ni ile ile. Kwa sababu kelele hizi ambazo zinasikia leo na jana ni kelele ambazo zimepigwa sana huko nyuma. Iliwahi kufikia nchi hii asilimia 20 ya bajeti ilikwenda kwenye elimu, mwaka 2008. Lakini ukiangalia uwekezaji tulioufanya kwenye elimu na ubora ambao tunaupata kwenye elimu haviendani kabisa. Na hapo ndipo ambapo tunapaswa kuangalia ni namna gani ambavyo tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya kujitegemea ilitaka kujenga taifa kujenga Taifa moja. Elimu ya sasa tunataka kujenga nini? Haya ni mambo ambayo ni lazima tujiulize kama nchi na tuyapatie majawabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyozungumza katika watoto ambao wanamaliza darasa la saba asilimia 50 walipofanyiwa utafiti, 50 percent walikuwa hawawezi kupiga hesabu ya sita jumlisha tatu. 50 percent walishindwa kupiga hesabu ya saba mara nane. Na haya si maneno yangu, ni utafiti ambao umefanywa na vyombo mbalimbali. (Makofi)
Kwa hiyo tuna tatizo kubwa kwamba siku zote tunaangalia inputs. Bajeti, majengo, enrolments, hatuangalii outcomes ni nini. Na kwa hiyo ningemshauri Mheshimiwa Waziri kwamba sasa hivi tuanze kuji-focus, na si Waziri peke yake, sisi viongozi, wazazi na kadhalika tu-focus tuangalie kwenye matokeo ya elimu. Watoto wetu hawasomi, lakini si hivyo tu, walimu pia hawafundishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Benki ya Dunia na REPOA wametoa taarifa inaitwa Social Delivery Indicators. Inaonesha kwamba ukienda ghafla kwenye shule zetu bila kutoa taarifa, the so called ziara za kushtukiza asilimia 49 ya walimu hawapo shuleni kabisa. Kwa hiyo, tunapozungumza tunataka tuwekeze kufanya walimu wawe motivated, wawe na hamasa wafanye kazi, tuwalipe vizuri lazima pia tuwaambie walimu wawajibike kufundisha watoto wetu. Kwa sababu takwimu zetu ni mbaya sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo nusu ya walimu hawaingii darasani maana yake ni kwamba hiyo inayoitwa mishahara hewa hii ndiyo mishahara hewa kweli kweli, kwa sababu nusu ya walimu hawafundishi, maana yake mishahara ambayo tunailipa, tunailipa bila watu kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri, kwanza salary scale ya walimu tuibadilishe. Salary scale ya walimu tuiweke sawa sawa na angalau nusu ya salary scale ya Wabunge. Na tusim-judge mwalimu kwamba huyu anafundisha primary, huyu anafundisha sekondari, huyu anafundisha chuo kikuu, walmu wote salary scales zao zifanane, mishahara yao itofautiane kulingana na muda ambao wamefundisha na kulingana na kiwango cha elimu ambacho wanacho. Kwa maana hiyo ni kwamba tutakuwa tuna walimu wazuri, dedicated, ambao wanaanzia chini kabisa kwenda mpaka ngazi ya juu kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vikuu vyetu ndiko hali mbaya kabisa. Juzi kuna taarifa imetoka inaonesha kwamba kuna vyuo vikuu bora 30 Afrika, Tanzania hatumo. Hata Makerere na Nairobi ambao tulikuwa tunawazidi sasa hivi wanatuzidi. Lakini hii inatokana na nini? Ni kwa sababu ukiangalia bajeti ya elimu, hivi vitabu vya bajeti ya elimu tukivishika utaona development budget kubwa sana, zaidi ya shilingi bilioni 500, lakini 80 percent of that ni mikopo. It is distorting na ndiyo maana Kamati imependekeza kwamba fedha za mikopo ya wanafunzi zitoke hazina ziende Bodi ya Mikopo moja kwa moja, zisipite kwenye vitabu vya Wizara kwa sababu inaonekana vibaya, bajeti inaonekana ni kubwa wakati haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu nchi kama hii 0.001 percent ya bajeti yetu ndiyo inakwenda kwenye research and development, vyuo vikuu vinafanya kazi gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna commitment ambayo tumeweka, kuna commitment kwenye Five Years Development Plan, kuna commitment za matamko ya viongozi kwamba tutaweka asilimia moja ya Pato la Taifa kwenye research and development, kwa nini hatufanyi? Vyuo vikuu vyetu haviwezi kufanya research and development. Nilikuwa naomba nisisitize hili, na niwaombe Waheshimiwa Wabunge. Takwimu za GDP tunazijua. Waziri wa Fedha anaweza akatuambia GDP ya sasa hivi ni ngapi. Tuangalie bajeti. Leo hii tunatenga 500 billion kwenda kununua ndege, 500 billion, 500 billion kwenda kununua ndege, atakayerusha hizo ndege ni nani? Atakayezitengeneza hizo ndege ni nani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, one percent ya GDP ni bilioni 59 tu. Tunyofoe kule, tuwaombe watu wa Kamati ya Bajeti wakae tunyofoe kule, tuweke kwa ajili ya reseach and development, watu wetu wafanye kazi ya utafiti tuweze kuzalisha na tuweze kuitengeneza nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumalizia kwenye ufundi. Na Wabunge wengi wamezungumza hili. Kwa hiyo ni consensus, lakini nimeangalia bajeti hapa, tunazungumza kuhusu VETA kila Wilaya, tunazungumza kuhusu vyuo vya ufundi katika Mikoa, bajeti ha-reflect. Bajeti yetu hai-reflect hizi VETA tunazozitaka. Lakini tuna zaidi ya 50 percent ya watoto ambao wanamaliza kidato cha nne hawaendelei na elimu ya juu zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba tuwekeze kwenye VETA, tuwekeze kwenye vyuo vya ufundi mchundo na mimi hapa ninakuja kuomba ombi langu rasmi Mheshimiwa Waziri, naomba Chuo cha Ufundi Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma ni lango la Magharibi la nchi hii, Kigoma ndiyo center ya nchi zote za Maziwa Makuu. Ukitaka kufundisha watu utengenezaji wa boti Kigoma fits, ukitaka kufundisha watu maritine Kigoma fits, ukitaka kufundisha watu namna ya kuvua kisasa Kigoma fits.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri katika mipango ambayo tunakwenda kuifanya kwa ajili ya kufungua vyuo vya ufundi yva kutosha tupate chuo cha ufundi pale ili tuweze kusaidia, kama jinsi ambavyo wengine wameweza kuomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa naomba kusisitiza kwamba tuwekeze kwenye matokeo, tuangalie namna gani ya kuboresha watoto wetu waweze kusoma. Watoto wetu hawasomi.
Naomba tuji-focus huko, tuondokane na inputs, tumeshawekeza sana kwenye inputs, tumeshawekeza sana huko, naomba sasa hivi tujikite sasa hivi kwenye outcomes na ili tuwe na outcomes nzuri ni lazima tuwe na mwalimu ambaye yuko motivated, na ni lazima tuwe na mwalimu ambaye yuko accountable, nashukuru sana.