Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa hii fursa niweze kuchangia Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Ningependa kuanza na issue za Jimboni kwangu Jimbo langu la Serengeti ninapotoka. Ningependa kuzungumzia suala la kifuta jasho kwa wananchi ambao wanaishi pembezoni ya mbuga ya Serengeti ambao wamekuwa wakipata madhira ya kuvamiwa na Tembo kwa kubomolewa nyumba zao, kuharibiwa mazao pamoja na kupoteza maisha. Naomba nitoe mifano michache tu, mfano mwaka jana Kata ya Machochwe Jimbo la Serengeti karibia asilimia 50 ya mazao yaliharibiwa na mpaka sasa hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kijiji cha Makundusi kuna mama alikuwa na mtoto mgongoni aliuwawa na Nyati na yule mtoto alikuwa mdogo wa miezi mitano anatambaa yule mama alifariki na yule mtoto ameachwa yatima mpaka leo hajaweza kulipwa fidia. Kuna wakazi wa kijiji cha Nata wamebomolewa nyumba zao hawajalipwa fidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri naomba unisikilize, kwenye kitabu chako ukurasa wa 31 umeonyesha shilingi bilioni 1.4 zimeipwa kwa wananchi 7320 kwa wilaya 57 kama kifuta jasho na machozi, lakini kuna malalamiko makubwa na mengi kwa wakazi wa Jimbo la Serengeti kuhusu kulipwa fidia au kifuta jasho kwenye mazao yao yaliyoharibiwa, wanakijiji waliopoteza maisha na nyumba zilizobomolewa. Sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri naomba nipate list ya watu waliolipwa kutoka katika Wilaya ya Serengeti kati ya hizi shilingi bilioni 1.4 ulizozionyesha, na usipofanya hivyo leo nitaondoka na mshahara wako.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba niende kwenye mambo ya Kitaifa, kwenye taarifa ya Mheshimiwa Waziri ameonyesha kwamba mapato yanayotokana na Utalii ni dollar za Kimarekani milioni 2.4, idadi ya watalii ni milioni 1.5. ukitafuta per- capital spending ya kila mtalii kwa maana ukichukua mapato yale tuliyoyapata dollar za Kimarekani milioni 2.4 ukigawa kwa idadi ya watalii wapatao milioni 1.5 unapata shilingi dollar 1.6 sawa na shilingi 3,500, maana yake ni nini, ni kwamba kila mtalii alitumia shilingi 3500 na ningependa kupata ufafanuzi hizi data ni za kweli au hata wale vijana wa bodaboda wanafika kwenye geti la Serengeti na wao mnawahesabia ni watalii?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la mradi wa Stiegler’s Gorge ambao Serikali imeamua kwenda kuutekeleza katika Bonde la Mto Kilombero pamoja na Rufiji ambako kuna pori la Akiba la Selous. Wote tunafahamu Selous is the World heritage, ni urithi wa Dunia. Lakini pia tunafahamu Utalii wa Southern Circuit unategemea mbuga ya Pori la Selous lakini nasikitika kwamba Serikali imeamua kwenda kuharibu mazingira bioanuai na kuathiri maisha ya Watanzania zaidi ya 500,000 wanaofanya activities na wanaoishi pembeni mwa bonde la Kilombero pamoja na Mto Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa watu ambao wa umri wangu ambao walisoma Literature wakati nikiwa form three kuna kitabu kimoja kilikuwa kinaitwa Song of Lawino, kwetu sisi Stiegler’s Gorge ni kama Song of Lawino. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwetu sisi tutaimba mradi wa Stiegler’s Gorge kama Song of lawino ili mtanzania, ili Watanzania wote wenye masikio na wasikie kwamba mradi huu una madhara na hautakwenda kuwafaidisha Watanzania. Stieggler’s Gorge is nonstarter project na ninawaomba namuomba Mungu Waheshimiwa Wabunge 2020 tuweze kupata…
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa!
MHE. CATHERINE N. RUGE: Namuomba Mungu atujalie Waheshimiwa Wabunge turudi hapa 2020 ili muweze kuthibitisha maneno yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivyo, Stiegler’s gorge is non-economically viable, Stiegler’s gorge is not economical viable.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo statement huwezi kurudi Bungeni.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kwanza kabisa gharama za utekelezaji wa huu mradi umekuwa under estimated, kuna taarifa ya mtu anaitwa George Hartman amesema amefanya economic feasibility na ripoti yake inasema kwamba mradi huu utatekelezwa kwa trilioni 21 wakati sisi Tanzania tumesema ni trilioni 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Benki ambazo tumezifuata kwenda ku-finance huu mradi hazina uwezo Egyptian Banks haziwezi ku-finance huu mradi na tukisema tutumie mapato ya ndani pia hatuna uwezo wa ku-finance trilioni 21 kwenye Stiegler’s Gorge. Pia mradi huu unakwenda kuwaathiri watu zaidi ya 500,000 wanaoishi pembezoni mwa Bonde Mto Rufiji pamoja na Bonde la Selous kwa sababu shughuli zao zinategemea maji yanayotoka katika Mto Rufiji. Pia hatujafanya environmental impact assessment kuona madhara ya muda mrefu kwa ajili ya huu mradi.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu utaratibu.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Catherine Ruge naomba ukae. Mheshimiwa Subira kanuni iliyovunjwa.
KUHUSU UTARATIBU
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kanuni ilivyovunjwa ni kanuni 64 naomba nisiisome.
NAIBU SPIKA: Endelea Mheshimiwa Subira.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, hatatoa Bungeni taarifa ambazo hazina ukweli wowote Kanuni 64(1)(a). Mheshimiwa Mbunge Catherine anayechangia anatoa taarifa ambazo hazina ukweli wowote, mradi wa Rufiji hydro power ulifanyiwa tathimini na tenda ilivyotangazwa wakandarasi wameomba kwa kadri wanavyoweza kufanya ule mradi na ndio maana tumeingia mkataba nao wa kiasi cha trilioni 6 ambazo wakandarasi na timu ya Serikali ya wataalam iliyondwa kwa pamoja na kwa majadiliano tumekubaliana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa anaposema kwamba mradi utagharimu trilioni 21 na kwamba Serikali imeingia na mabenki ambapo Serikali utagharamia mradi huo kwa vyanzo vyake vya ndani na imeshatoa asilimia 15 kiasi cha bilioni 685. Sasa anaposema kwamba Serikali imetumia mabenki ambayo hayapo asilipotoshe Bunge Serikali itagharimu mradi huu kwa pesa zake za ndani na imeshalipa asilimia 15 na kazi inaendelea. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge Mheshimiwa Catherine Ruge alikuwa akichangia, Mheshimiwa Subira Mgalu amesimama akionesha kwamba katika mchango wa Mheshimiwa Catherine Ruge ametoa taarifa ndani ya bunge ambazo hazina ukweli kwa mujibu wa Kanuni ya 64(a). Sasa Waheshimiwa Wabunge ukisoma masharti ya hii Kanuni ya 64 na Kanuni ya 63 inanitaka nikiombwa utaratibu kuhusu jambo hili nimtake Mheshimiwa Mbunge aliyekuwa akichangia kwa maelezo hayo yaliyotolewa na Mheshimiwa Subira Mgalu kwa sababu yeye ndio aliyesema hilo jambo si la kweli na amejaribu kuonyesha namna ambavyo yeye taarifa zake alizonazo zinaonyesha kwamba taarifa unayotoa ni tofauti na anayoitoa.
Kwa hiyo, kwa mujibu sasa wa hii Kanuni ya 64 na Kanuni ya 63 inayozungumzia kutokusema uwongo Bungeni Mheshimiwa Catherine Ruge taarifa hiyo ya Mheshimiwa Waziri na taarifa uliyoitoa wewe uyafute hayo maneno labda kama nawe unao ushahidi tutakutaka kwa mujibu wa kanuni hii. Kwa hiyo, unayo hayo mawili, moja ni kufuta kwa mujibu wa kanuni hizi kama unaoushahidi utanijulisha ili niweze kutoa maelekezo mengine Mheshimiwa Catherine Ruge. (Makofi)
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni maoni yangu na nimesoma report ya George Hartman inasema hivyo mradi utatekelezwa kwa trilioni 21 hiyo ni research report amefanya utafiti kama hauna hiyo report nitaweza kukupa, lakini pia sheria mpya ya madini inasema…
NAIBU SPIKA: Sawa ngoja Mheshimiwa Catherine Ruge kabla hujaendelea kuchangia tulimalize hili kwanza, kwa hivyo katika yale mawazo mawili wewe unasema unao ushahidi.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ndio.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge kwa mujibu wa hizi Kanuni zetu mchango wa Mheshimiwa Catherine Ruge nimelazimika kumuuliza mara ya pili kama anao ushahidi kwa sababu ameanza kwa kusema yeye ni mawazo yake, lakini sasa amethibitisha kwamba yeye anao ushahidi. Kwa hivyo, nitamruhusu aendelee kuchangia ataleta ushahidi wake ambao ushahidi huo kama taratibu zetu zilivyo ili kumbukumbu zetu zikae sawasawa ushahidi huo utapelekwa kwenye Kamati ambayo itatusaidia kuangalia uhalisia wa hiyo taarifa anayoitoa. (Makofi)
Kwa sababu hiyo Mheshimiwa Catherine Ruge mchango wako kuhusu Stiegler’s Gorge kwa kuwa sasa utapeleka ushahidi kwenye Kamati utaangaliwa wakati huo, naomba uendelee kuchangia kwenye jambo jingine linalofuata. (Makofi)
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee na mchango wangu. Nafahamu Tanzania tuna vyanzo vingi sana vya umeme ambavyo tungeweza kuwekeza huko na tukapata megawatts hizo hizo 2,100 au zaidi, lakini pia nafahamu Wajerumani ambao wamekuwa wakitoa fedha kwa ajili ya kuhifadhi mazingira kwenye Bonde la Akiba la Selou toka mwaka 1959, lakini pia wakitoa pesa kwa ajili ya kuzuia ujangili, walitoa offer kwa Serikali kuweza kuwekeza kwenye alternative source of energy ya geothermo na wakasema wanaweza waka- finance huo mradi wa umeme wa geothermo kupata megawatts 2,000, lakini Serikali imekataa offer hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa tu kufahamu, ni kweli tuna nia ya kupata nishati ya umeme au nia yetu ni kwenda kuharibu Bonde la Selou ambalo limekuwa kivutio kikubwa cha watalii kwa Southern Circuit, lakini pia utalii wa Southern Circuit unategemea sana Mbuga ya Selou. Naomba niseme na iwekwe kwenye hansard, mpaka mwaka 2025 hamtakuwa mmetengeneza hata megawatt moja kutoka kwenye Mradi wa Stieglers Gorge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye jambo lingine. Kulikuwa na hoteli za kitalii ambazo zilikuwa kwenye hifadhi ambazo zilikuwa chini ya Serikali, lakini wakapewa watu binafsi, lakini hoteli hizi zimekuwa na hali mbaya kuliko hata zilivyokuwa chini ya Serikali. Jumla ya hoteli hizi zilikuwa 16, lakini nina mifano michache; moja ya hoteli hizo ni Mafia Lodge ya Mafia, Lobo Lodge Serengeti, Seronera Wildlife Lodge, Ngorongoro Wildlife Lodge, Manyara Wildlife Lodge, zina hali mbaya kimiundombinu, mapato, huduma. Ningependa kufahamu msimamo wa Serikali kuhusu hoteli hizi ambazo zilibinafsishwa na hazifanyi vizuri na ni nini sasa way forward kuhusu kuzihusisha hoteli hizi.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa Catherine Ruge.