Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Fatma Hassan Toufiq

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa fursa ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu ambayo ni Hotuba ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla, Naibu Waziri, Mheshimiwa Kanyasu Constantine na Watendaji wote kwa kuandaa hotuba hii tunayoijadili.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza mafanikio ya Wizara kama ilivyobainishwa katika ukurasa namba 10 hadi 18 wa hotuba, ikiwemo kupungua kwa ujangili, uanzishwaji Jeshi Usu, kubadilisha hadhi baadhi ya maeneo ya hifadhi, ongezeko la watalii, mapato na kadhalika. Pamoja na mafanikio yaliyopo bado kuna changamoto ambazo zikipatiwa ufumbuzi zitaleta tija na ufanisi katika utendaji wa Sekta ya Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, iwapo Serikali itatoa fedha iliyoidhinishwa yote na kwa wakati ni dhahiri miradi iliyokusudiwa itatekelezwa, kuna wakati na kuiletea pato kubwa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Suala la Biashara ya uwindaji wa Kitalii ni tofauti na biashara nyingine, ni ukweli usiopingika uwindaji wa kitalii unahitaji amani, uwepo wa vivutio vyenye sifa ili wawindaji wa kitalii waendelee kuja na kuliongezea Taifa kipato, Wizara iwe na mikakati endelevu ya kuwezesha biashara ya uwindaji wa kitalii ishamiri, pia mazingira ya wanyama stahiki yalindwe vema, kwani kuna baadhi ya wananchi wanavamia maeneo ya mapitio ya wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Idara ya Misitu na Nyuki, Wakala wa Misitu (TFS) nina ushauri ufuatao: Uwepo uhifadhi wa misitu wenye tija, kwani uhifadhi misitu, si utaalam tu bali ni pamoja na matumizi endelevu ya misitu, bila kupoteza sehemu yoyote ya malighafi hususan na kuzingatia utaalam wa teknolojia ya kisasa katika uhifadhi misitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado usimamizi wa Misitu haukidhi viwango na misingi inayolenga kuendeleza uchumi wa nchi na uboreshaji mazingira, mfano mashamba ya miti, Tanzania ina maeneo makubwa lakini kasi ya upandaji miti si wa kasi sana. Kasi ya upandaji miti na uvunaji haziwiani hivyo kutishia uvunaji endelevu, hasa miti ya asili. Miti ya asili inazidi kupotea, ni budi Serikali kupitia Wizara ikawe na utaratibu wa kuelimisha watoto, vijana na jamii kwa kuwapa elimu kuhusu umuhimu wa misitu katika maendeleo ya binadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Misitu katika mabonde na mito nayo wananchi waelimishwe umuhimu wake. Katika mazao ya Nyuki, nampongeza Mheshimiwa Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu na wadau wengine wote wanaoendeleza zao la nyuki, ni zao ambalo linaweza kuleta mapinduzi makubwa kiuchumi, hivyo wananchi wengi wahamasishwe ili wajiingize katika biashara ya mazao ya nyuki pamoja na uhifadhi wa mazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iendelee kuwaelimisha hasa wananchi wa pembezoni na vijijini faida ya mazao ya nyuki badala ya kuharibu mazingira kwa kuchoma mkaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kusisitiza Wizara ijikite kwa undani katika masuala ya utalii na fukwe, mapango, mila na desturi za makabila, historia ya Viongozi wa kimila na makabila mbalimbali Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.