Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibaha Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAMOUD A. JUMAA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha nami kuwepo mahali hapa na kuweza kuchangia hotuba hii ya Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii ya mwaka 2019/2020. Aidha, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na wataalam wa Wizara kwa kuandaa hotuba nzuri, halikadhalika hotuba hii inakwenda kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kuhakikisha Sekta nzima ya Maliasili na Utalii inaendelea kuimarika na kuliingizia pato Taifa letu kwa maendeleo ya watu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuendelea kufanya kazi kubwa ya kiuboreshaji hasa katika Sekta ya Utalii, imeendelea kuimarika na kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa pato la Taifa na kuongeza ajira. Mathalan, idadi ya watalii kuongezeka mara dufu na kupelekea watalii walioingia nchini mwaka 2018 kuongezeka na kufikia watalii milioni 1.49 ikilinganishwa na watalii milioni 1.33 walioingia nchini mwaka 2017. Aidha, hapo hapo pia mapato yatokanayo na utalii yameongezeka na kufikia Dola za Marekani bilioni 2.43 mwaka 2018 ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 2.19 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 7.13, ni mwanzo mzuri wa kimkakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuendelea na jitihada hizi ili takwimu hizi ziendelee kukua, halikadhalika Serikali imetuambia katika kutangaza vivutio vya utalii, mwaka 2018/2019 Serikali imeanzisha Chaneli ya Utalii (Tanzania Safari Channel) ili kuvutia Watanzania na wageni kutoka Mataifa mbalimbali kutembelea vivutio vyetu. Hatua hii itasaidia sana kuendelea kukuza hali ya kiuchumi kupitia Sekta hii ya Utalii. Kuanzishwa kwa chaneli hii pia, Serikali imetueleza kuwa inaendelea kuimarisha chaneli hiyo kwa kuipatia wataalam, vifaa na vitendea kazi stahiki. Chaneli hii itaendeleza taswira na sifa nzuri ya Tanzania kimataifa sambamba na kuongeza thamani katika mnyororo mzima wa biashara ya utalii nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo pongezi zangu zinakwenda kwa Serikali kuwa na mpango katika mwaka 2019/2020, kuendelea kuimarisha Sekta ya Utalii kwa kuihamasisha na kuiwezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuendeleza sekta hiyo. Aidha, sanjari na kutangaza utalii, Serikali imeendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo usafiri wa anga ili kuvutia watalii wengi zaidi nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati katika kuendelea kupambana na uharibifu wa maliasili kama misitu na kadhalika. Hatua hii imesaidia sana pia hata katika utunzaji wa mazingira yetu na kuepukana na ukame ambao athari zake ni kubwa, kama nchi ikikumbwa na tatizo hilo. Napenda kuishauri Serikali kuendelea na jitihada hizo kimkakati, na kuendelea kupambana na wahalifu wote wanaojaribu kuharibu mazingira yetu kwa kukata miti hovyo, hata hivyo sasa ni wakati wa kutambulisha utalii wa misitu kwani tunayo misitu mingi yenye vivutio kadhaa hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.