Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muleba kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kabisa kwa kusema kwamba naunga mkono hoja. Nampongeza sana mdogo wangu Mheshimiwa Profesa Ndalichako, amekaa vizuri na yameshasemwa mengi kwamba yeye ni mchezaji wa kukodisha. Nami nakubaliana na usemi huo. Maana yake ni kichwa, ametafutwa na sasa hivi nadhani nazi imepata mkunaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaposimama hapa, baada ya kuyasema hayo, pia, nitoe masikitiko yangu makubwa kwa Naibu Waziri wake ambaye amempoteza mama na Waswahili wanasema, “aisifuye mvua, imemunyea.” Kwa hiyo, najua machungu anayopita, Mungu ailaze roho ya mama yetu, mahali pema Peponi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasimama hapa kwanza kabisa kama mdau wa elimu. Watu wengi wameshasema, wengine wanasema ni mgongano wa masilahi. Mimi sina mgongano wa masilahi ila I am interested party. Katika hili la elimu, natangaza kabisa, hii ni sekta ambayo Mwenyezi Mungu akinijalia maisha, ninalia nayo, nakufa nayo, nahangaika nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, maana yake Waheshimiwa Wabunge wote ambao mko ndani hapa, ni kwa sababu wazazi wetu katika nyakati mbalimbali na mazingira mbalimbali walitupeleka shule, ndiyo maana tuko hapa. Ni ufunguo wa maisha. Kwa hiyo, hii sekta ambayo tunaijadili leo, tunazungumza mustakabali wa Taifa hili na watoto wetu. Kwa hiyo, hapa ni lazima wachangie kwa uchungu; na wachangiaji wengi nasikia wanazungumza mambo yanatoka rohoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa muda ni mfupi, siyo rafiki. Naomba nianze kwa kumwomba Mheshimiwa Waziri aangalie Waraka Na. 6 wa Elimu wa Mwaka 2015. Mheshimiwa Waziri unajua kwamba nilishawahi kuzungumza kwamba Waraka huu umeandikwa vizuri, lakini unatakiwa kuboreshwa. Ulivyoandikwa, sasa hivi ulivyokaa, sisi ambao tunawakilisha wananchi wetu katika mazingira ambayo bado elimu ni changamoto, unatuletea sintofahamu. Kwa sababu nimeona katika hotuba yako umefafanua jukumu la Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana, napongeza sana kwamba, Mheshimiwa Rais ameona yafaa kwamba Serikali ijaribu kutoa elimu bure kwa maana ya kwamba Serikali inagharamia elimu. Elimu unaposema iko bure inamaanisha, Serikali ndiyo inalipia elimu, wazazi wanakuwa wamepunguziwa mzigo. Kwa sababu kwamwe elimu haijawahi kuwa bure, lazima mlipaji apatikane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo basi, naomba nikupeleke kwenye Jimbo la Muleba Kusini ambalo limenituma hapa. Mheshimiwa Waziri, Waraka ule ulivyosimama, utakaposimama kujibu, naomba unipunguzie matatizo niliyonayo Muleba Kusini. Pale tuna Shule za Sekondari. Kwa mfano, tuna sekondari 44, wanafunzi 15,378, lakini hali ya shule zile bado madarasa hayatoshi, madawati hayatoshi, nyumba za Walimu hazitoshi, mabweni usizungumze, Maabara tunahangaika nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali hiyo, ni muhimu sana Waraka ukatambua pia kwamba kwa kuwa sera yetu ya elimu ni bure, inamaanisha kwamba wazazi ndio wanatolewa mzigo wa kulazimisha watoto kushindwa kuja shule, lakini jamii inachangia. Nataka niseme kabisa kwamba ule Waraka una walakini sana kwa sababu unafanya kazi yetu iwe ngumu. Sijui wenzangu vipi, lakini Muleba Kusini watu wote wanashikilia elimu ni bure, hawataki kuchanga. Hawataki kuchanga katika hali ambayo Serikali Kuu haina fedha za kutosha kuweza kuenea na wengine wameshasema. (Makofi)
Kwa hiyo, kusudi tusijirudishe nyuma, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri, utakaposimama kujibu, ujaribu kutuelezea, utakavyotusaidia katika hili. Elimu ni bure, lakini pia lazima jamii ya Watanzania ilipe. Ni vizuri kwa sababu mwisho wa siku mtoto ni mali ya jamii, siyo mali ya mzazi. Mtoto ni mali ya jamaii, hilo nadhani nimelimaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nimeshasema kwamba, mimi nimekuwa mdau wa elimu kwa muda mrefu; mimi ni Mwanaharakati wa Haki za akina mama, katika hilo wala sirudi nyuma, wala siombi radhi kwa mtu yeyote, ninasonga mbele. Sasa Wanawake ukiangalia, tumepiga hatua, lakini katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nimeona hapa katika lile jedwali.
Katika udahili wa Vyuo Vikuu, bado wasichana ni asilimia 50. Bado hawajaweza kuwafikia wale wavulana. 7, 700 wasichana, wavulana wanaingia kwenye 15, 000 na zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utaona kwamba, bado changamoto ya mtoto wa kike bado iko unapozidi kupanda ngazi, ngazi za chini tuko sawasawa. Sasa shule zetu za Kata zimeleta mafanikio makubwa sana. Kama maendeleo yote, zimeleta changamoto! Shule za Kata ndizo tunataka kuhangaika nazo kwa sababu ndiyo mkombozi wa Taifa letu. Sasa hivi naipongeza Serikali ya CCM, imefanikisha kupunguza tatizo la Walimu katika shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba nikupe mrejesho Mheshimiwa Waziri. Nikichukuwa Muleba tu, nilishasema ina shule za sekondari 44, ina wanafunzi 15,000 na Walimu wamepatikana. Katika Hesabu, tuna upungufu wa Walimu 86; na kuna shule 13 za sekondari Muleba, hazina Mwalimu wa Hesabu hata mmoja.
Katika hali hiyo, kama tunavyozungumza, shule ambayo haina Mwalimu wa Hesabu ni hatari sana. Naomba Mheshimiwa Waziri jambo hilo aliangalie, kama hajalifanyia kazi, lifanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Biology, Muleba kuna shule nane hazina Mwalimu wa Biology, upungufu Walimu 47. Shule nane hazina Mwalimu wa Chemistry. Huwezi kutoa Mkemia pale! Huwezi kutoa Daktari pale! Shule 57 hazina walimu hao. Physics, hiyo ndiyo zahama kabisa! Walimu 80 wanakosekana. Shule 18 hazina Mwalimu wa Physics na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naendelea; Kiswahili, Muleba tumeletewa Walimu wa Kiswahili 85 wa ziada. Walimu 85 wa ziada wa Kiswahili, Walimu 80 wa ziada wa Historia, Walimu 30 wa ziada wa Jiografia. Napendekeza kwamba, haya ni maendeleo, lakini maendeleo yanataka mrejesho from the field. Nataka nipendekeze kwamba, baadhi ya Walimu hawa wangeweza kufanyiwa retraining wakatusaidia katika masomo mengine ambayo hayapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza pia kwamba Walimu hawa wanaweza wakapelekwa Shule za Msingi. Hii kasumba kwamba wanaotoka Chuo Kikuu wataishia Shule za Sekondari, nayo tuondokane nao. Pia nataka kusema kwamba shule inapokuwa haina Mwalimu wa Hesabu, hiyo ni crisis. Mwalimu Nyerere, sisi tulifundishwa na wamarekani, tulifundishwa na Walimu kutoka India. Mimi nafikiria kwamba…
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kengele ya kwanza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini ni kengele ya kwanza. Niombe tu Mheshimiwa Waziri utakapo simama au utakapojiandaa na timu yako nzuri ya Makatibu Wakuu waliobobea katika elimu, mwangalie namna ya kutafuta misaada kutoka nje. Nadhani hatuwatendei watoto haki. Mtoto anamaliza Form Four hajawahi kukutana na Mwalimu wa Hesabu! Kwa kweli hapo tutakuwa hatuwatendei haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamesema mengi kuhusu shule binafisi. Mimi ninashiriki katika Taasisi zinazoendesha shule binafisi. Yameshasemwa mengi; elimu ni ya ghali, inaweza ikawa bure kwa sababu Serikali nzuri inaisimamia, lakini elimu ni ya ghali. Sasa hizi shule ambazo tunataka, wazazi wanafanya bidii, wanajiongeza. Nafikiria ifike mahali wazazi na wenyewe tutambue mchango wao. Sisi kama viongozi kusimama hapa na kusema tunaweka ada elekezi wakati wazazi wako tayari kulipa, kwani wazazi ni wajinga? Kwani wazazi hawana akili? (Makafi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, amezungumzia mtu, akasema kwamba Sukari ni pendekezo, lakini huwezi kulinganisha elimu na sukari; ni bidhaa tofauti. Ni bidhaa tofauti kabisa, ziko katika masoko tofauti na mtu yeyote anayeelewa elimu, anajua kwamba elimu ni huduma. Katika shule nzuri, elimu ni huduma, haiwezi kuwa biashara. Wengi wanasema; mimi nikitaka biashara nitauza Bia na kaka yangu Rugemalila, sitahangaika! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikitaka biashara sitahangaika na shule; shule siyo biashara. Ukitaka biashara unakwenda kwenye fast moving items; unauza bia, unauza nini na mambo yanakuwa mazuri. Elimu ni huduma! Sasa wale wanaotoa huduma, tuwatambue mchango wao, tuwaenzi. Katika nchi nyingine, wana utaratibu wa kupeleka fedha katika shule binafsi. Sasa sisi tuna utaratibu huu kidogo ambao unaweza kusema ni aibu kwa Taifa watu wa TRA kwenda kushinda kwenye shule wanatafuta kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo hayatusaidii, nayazungumza kwa dhati kabisa kwa sababu program tulionayo ni nzuri. Kwa hiyo, nataka kusema kwamba hilo nilichangie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine la haraka kama muda utaniruhusu, nizungumzie pia umuhimu…
MHE. PROF. ANNA K. TIBAIJUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.