Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi nzuri yenye tija kwa taifa letu. Mheshimiwa Waziri ninakuombea Mungu aendelee kukupa afya, nguvu na wepesi ndani ya utekelezaji wa majukumu yako kwani chini ya uongozi wako Wizara imetulia na unawajibika kwa maslahi ya kuachia urithi watoto wetu na kusababisha kuongeza gawio kwa Pato la Taifa. Tumeweza kubainisha maeneo kadhaa ya vivutio hapa nchini kwa nia ya kupanuwa wigo wa utalii. Tatizo ni kuhakikisha tunaweka mazingira madhubuti ya kuweka miundombinu yote kwa kuanzia kabla ya kutangaza ili wakiingia watalii wasiwe na kigugumizi tena cha kurudi au hata kushawishi wengi kutokana na kukuta ubovu wa miundombinu. Mfano Rukwa kuna Kalambo falls, ni kivutio kikubwa ndani ya Afrika Mashariki na Kati lakini hakuna barabara na hoteli, vyoo na maeneo ya kupumzika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi wa kilimo Rukwa ni Oktoba – Novemba mvua zinachanganya na kwa wananchi wetu kilimo ndio mradi mkuu kwa kuzalisha chakula na mazao ya ziada kwa biashara. Wanapojitokeza wanyama waharibifu kunakuwa na hasara kubwa kwa wananchi wetu na maafisa kuwa na uvivu wa kuyatembelea mashamba yaliyoathirika kwa wakati na kwa eneo zima, wamekuwa wanawahadaa wakulima na hatimaye kuwa na chuki na Serikali yao. Mfano kijiji cha Kisumba – Katanga Kisumba, Wilaya ya Kakumbo – Rukwa. Wakulima wa alizeti walioingiliwa na wanyama ni 140 lakini waliolipwa ni wakulima 60, wengine hadi leo hawajalipwa. Tunaomba Wizara na kitengo husika kufuatilia malalamiko ya wakulima na kuwa shughulikia malipo ya fidia zao ili zitoke; ni kero kubwa sana huko vijijini, maafisa waachane na rushwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu wote tunakubaliana kuwa asali kwa sasa ina soko ndani na nje kwa matumizi ya kakwaida kwa afya zetu. Maadamu misitu tunayo nashauri wale mabwana nyuki tulionao wawe na kazi ya kutoa elimu, uelewa na kushauri makundi mbalimbali na kuunda makundi ya ujasiriamali kwa vijana na akina mama ili kuweza kuifanyia shughuli hiyo. Kwani ni mradi ambao unajizalisha wenyewe na maafisa wanafahamu maeneo yenye tija hiyo. Mikoa, wilaya, kata na vijiji ambavyo vina mwelekeo huo kwa uzalishaji wa asali kuwa na viwanda vya kuchuja na kufungasha kuingiza sokoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Ziwa Rukwa kuna mambo mengi sana lakini kutokana na uharibifu wa mazingira na shughuli za kibinadamu na mito kuporomosha maji kwa wingi na udongo moja kwa moja kwenye Ziwa sasa kina cha maji katika Ziwa Rukwa kinapungua na mamba kutawanyika na kuathiri wananchi wetu. Ushauri, mamba waweze kuvunwa, washirikiane na Wizara ya Maji, Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Tuweze kuvuna maji kwa umwagiliaji, mabwawa nakadhalika. Tuliokoe Ziwa na usalama wa wananchi wetu upatikane kwao dhidi ya mamba. Tunaomba Hazina kuitoa pesa iliyopendekezwa ya maendeleo ya Bilioni 48.889 yenye ongezeko la asilimia 66, tunahitaji matokeo chanya yajioneshe kwenye gawio la Pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.