Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CUF
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAINAB M. AMIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa wanayoifanya ndani ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ushauri; Serikali itenge fedha za kutosha, pia ambazo zinapitishwa na Bunge zitolewe kwa wakati ili kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali iainishe vivutio katika kila Wilaya ili kuweza kujua vivutio mbalimbali vilivyopo kisha kuweza kuzitangaza kama vivutio na sehemu ya utalii. Kwa mfano kuna chemchemi iliyopo maeneo ya Kisaki Mkoani Morogoro, maeneo ya Morogoro Vijijini ambapo Chemchemi hiyo ni ya maajabu maana maji yake ni ya moto kwa centigrade 100, lakini eneo hilo bado Serikali haijalibainisha na kufanya moja ya kivutio. Naishauri Serikali ilitangaze eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuwekeza katika miundombinu kwenye vivutio vya utalii kwa kujenga barabara, viwanja vya ndege, mahoteli n.k ili kuvutia watalii kufika kwenye vivutio hivyo kwa urahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali ipitie upya tozo mbalimbali zinazotozwa katika huduma za utalii na kuziondoa zile ambazo zinaifanya nchi yetu Tanzania kuwa ghali zaidi ukilinganisha na washindani wetu wa nchi jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali kuajiri askari wa kutosha kwa ajili ya kulinda hifadhi zetu maana kumekuwa na uhaba wa watumishi hususani askari wa kulinda hifadhi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali, ili kuondoa migogoro baina ya wananchi waliovamia hifadhi zetu na Serikali, elimu ya kutosha itolewe kwa wananchi hao. Pia Serikali iweke mipaka inayoonekana kiurahisi ili wananchi wasivamie hifadhi za taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Serikali malipo yanayolipwa (kifuta jasho) kwa wananchi walioharibiwa mazao yao, waliojeruhiwa na hata kuuawa na wanyamapori. Kifuta jasho hicho hakiridhishi hivyo Serikali angalau ione haja ya kuongeza ili angalau mwananchi aweze kuona haki imetendeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuomba Mwenyezi Mungu awape afya njema na umri mrefu Mheshimiwa Waziri na Naibu wako ili kuweza kutekeleza majukumu yenu ya kila siku.