Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nyang'hwale
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Katibu na Watendaji wote kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.
Mheshimiwa Spika, mchango wangu nauelekeza upande wa wachimbaji wadogo hususan wa Wilaya ya Nyang’wale. Wachimbaji hawa mapato yanazidi kupotea, huwa nasema kila mara, lakini pia niipongeze Serikali ya Wilaya ya Geita ama Mkoa wa Geita kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji asilimia 109. Hata hivyo asilimia hizo bado mimi nasema kuwa ni ndogo kwa sababu wachimbaji walio wengi mpaka sasahivi hawajatambuliwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika, kuna wachimbaji katika maeneo ya Isekeli, Bululu, Ifugandi, Shibalanga, Rubando, Iyenze, Nyamalapa, Iyulu, Ibalangulu na Kasue. Maeneo yote yale, uchimbaji madogo mdogo unaendelea na ile dhahabu inapotea. Kwanini Serikali isichukue hatua ya haraka ya kwenda kuyapima yale maeneo ya kuwapa leseni wale wachimbaji wadogo ili tuweze kuwatambua na kuweza kupata yale mapato? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu wa pili ni kwamba kuna changamoto kwa wachimbaji wadogo wadogo wadogo na wadau wa madini katika Wilaya ya Nyang’wale kwa sababu tumeuwa hatuna Afisa Madini maeneo hayo na wachenjuaji wamekuwa wakipata gharama kubwa kwa kufuatilia vibali kutoka Wilayani Nyang’wale kwenda Geita. Kibali hicho unakifuata kwa gharama ya kilometa 180 kw akutumia trip mbili za gari. Trip ya kwanza ni kufuata kibali kwa ajili ya kuchukua carbon kuzipeleka Geita, na kibali cha pili ni kutoka pale Madini kwenda Ilusion, gharama zote hizo zinakuwa ni za mwenye carbon. Kwa hiyo ninakuomba Mheshimiwa Waziri, tufungulie ofisi ndogo ya Madini pale Nyang’wale tuweze kuepusha zile gharama kwa sababu gharama zinakuwa ni kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia bado tuna changamoto nyingine, tuna illusion zetu pale katika Wilaya ya Nyang’wale. Maafisa Madini wanakaa Mkoani Geita, ukitaka kuwafuata inabidi utumie gharama zako wewe mwenyewe kwenda kuwafuata. Hizo gharama tunaomba mtuepushie kwa kuwasogeza karibu hao Maafisa Madini pale Wilayani Nyang’wale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kuna urasimu mkubwa sana; Ofisi ya Madini Geita kuna urasimu. Unapofuatilia vibali ukifika pale unachukua zaidi ya masaa matatu kupewa kile kibali. Hicho kibali ni cha kwenda kuchukua carbon kutoka kwenye maeneo yako, kibali hicho ni cha kupeleka carbon pale madini. Lakini pia kibali kile cha kutoka madini kwenda illusion nacho unachukua zaidi ya masaa matatu kukipata kile kibali. Mimi nadhani utaratibu huu sio mzuri, jaribuni kuangalia utaratibu huo, haupendezi.
Mheshimiwa Spika, pia bado kuna urasimu mwingine. Unapomaliza kuchoma dhahabu yako pale kwenye illusion, TMA yuko pale, madini yuko pale na maafisa wengine wako pale wanakuandikia kibali hicho cha kubeba dhahabu yako kuipeleka kwenye soko; lakini bado utakapoibeba ile dhahabu ambayo labda umeipata gramu 100, utakapokwenda kwenye lile soko unakuta ofisi ya Tume ya Madini wanaipima tena ile dhahabu pale, ile dhahabu bahati mbaya ikitokea imepungua ilikuwa gramu 100 lakini wakaipima ikawa gramu 99 wanakusumbua kwamba gramu moja imekwenda wapi, ilhali kule kwenye illusion wamekuandikia gharama ya mrahaba na service levy iko kwenye karatasi. Kama imepungua si ni gharama yangu mimi acha ipotee hiyo? Lakini wana usumbufu na wanatisha watu, kwamba wameipeleka wapi.
Mheshimiwa Spika, suala hili sio zuri, urasimu huo sio mzuri. Dhahabu si cocaine, hii ni biashara. Jiulize huyu amepitaje hiyo dhahabu mpaka gramu 100 leo hii imepungua gramu moja, ni kipimo, vipimo vinatofautiana; lakini pamekuwa na usumbufu na vitisho. Kwa hiyo nakuambia Mheshimiwa Waziri, jaribu kuliangalia kwa Mkoa wa Geita, usumbufu huo upo. Kwa haya machache nakushukuru sana Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasiya kuweza kuchangia. (Makofi)