Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiteto
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL P. JOHN: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kazi nzuri, ambayo inaifanya baada ya kuteuliwa na Mheshimiwa Rais. Napenda kushauri mambo machache yafuatayo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naona kwenye elimu Serikali imefanya mambo mengi, lakini na mengi yamezungumzwa humu ndani ambayo yanaelekeza ni jinsi gani ambavyo elimu inaweza kwenda na jinsi gani iwe na watu wote wametoa ushauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kumshauri Mheshimiwa Waziri kwamba aanze na Primary Schools. Ile mitaala ya Primary Schools ya zamani tuliyoizoea airudishie ule mfumo kwamba ukikuta Kitabu cha Darasa la Kwanza anachokisoma Mwanafunzi aliyeko Nkasi Tanzania, kule Rukwa, Sumbawanga, kitabu hicho hicho tukikute Lindi cha Darasa la Kwanza, kinachofanana na kinachosomeka vile vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Mheshimiwa Waziri a-plan Primary Schools kwanza, asiende haraka! Sekondari pumzika, Vyuo pumzika, taratibu tu, kule kunakwenda kuna Makamishina, kuna watu wanafanya, wewe nenda na Primary Schools, jenga misingi; hakikisha Walimu wanafundisha, hakikisha shule zinakaguliwa, hakikisha kuna utaratibu wa elimu kwa zile ambazo ni Sekondari, za Kiingereza Primary Schools wawe na mitaala inayofanana. Zile za Kiswahili zirudi vile vile kama zamani. Sayansikimu; mtoto afundishwe kutengeneza mwiko, chungu, afundishwe kupika, kulima; tunataka hiyo ianze Primary School bila haraka kwa mwaka huu. (Makofi)
Mwaka kesho wewe nenda Secondary School, Form One mpaka Form Six, panga mambo vizuri, usiwe na haraka, pesa hazitoshi na sisi ndiyo wakusanyaji, hazipo! Hicho kidogo kinachopatikana, mwaka kesho plan for Secondary School, Form One mpaka Form Six. Mwaka unaofuata, plan kwa ajili ya vyuo, nenda tena mpaka Vyuo Vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri awatafute wale Walimu wa zamani waliokuwa wanafundisha zile shule za primary; kaa nao, zungumza nao wakupe tactics na the way kuingia katika huu mfumo wa kutengeneza elimu bora kama ile ya zamani ambayo tunahitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri akae na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje. Tunao Mabalozi nje, wafanye kazi ya kutafuta scholarships kwa ajili ya wanafunzi wetu waende wakasome nje. Kila mwaka Balozi yeyote kwenye nchi aliyomo ambayo ina uwezo, aweze kuita na kutafuta wafadhili wasaidie watoto wetu wakasome nje. Lengo kuu la kusomesha watoto wetu nje, Watanzania wamejifunga; Watanzania wako magereza, wamefungwa; hawatoki nje! Wanafikiri hapa panaweza. Waende nje wakapigwe, wapigwe baridi, wapate shida, walale njaa, wakirudi Tanzania watashughulika na uwekezaji. Mheshimiwa Waziri, hebu jitahidi zungumza na hao watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, hawa wawekezaji mnaowaona ni kwa sababu wameona fursa huku, tupeleke watoto wetu kule. Wale watoto ukikaa nao ukiwaambia nenda kasome au nenda Netherlands, ukimaliza degree shawishi mfadhili ndugu yako mwingine apate nafasi umlete huko huko. Mkibaki huko, sawa; mkirudi Tanzania, sawa. Tutakuwa tumetengeneza Watanzania kwenye exposure ya dunia hii nao watoke nje wakaone vilivyoko huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkaguzi mmoja Kiteto alikuja ametoka kwenye kanda, ana gari, hana mafuta, hana nini. Nikamuuliza, sasa vipi? Anasema sasa nitakagua nini? Anataka kukagua na anayeombwa mafuta ni Mkurugenzi na akienda kuomba Mkurugenzi mafuta Mkurugenzi haiwezekani akamnyima mafuta kwa sababu anakwenda kumkagua; akimkagua anamletea madudu; akimletea madudu, hawataelewana. Matokeo yake anakosa mafuta, anakaa mezani analipwa mshahara bure. Hii ndiyo mishahara hewa ambayo tunazungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba hawa Wakaguzi waanze na Primary School wakutengenezee kitabu, wakuletee ujue matatizo ya Primary School kwa nchi nzima kwa mwaka huu ili ujue sasa shida za ku-tackle matatizo ya Primary School yanaanzia wapi na yanakwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiteto tuna shule za mabweni chache, lakini watoto wetu kwa sababu ya maeneo ya kifugaji, ni mbali. Shule nyingine ni kilometa 14, shule nyingine 15, sasa watoto kwenda shuleni ni ngumu.
Nakuomba, kuna shule za Dongo za sekondari, tunaomba hizi shule za bweni, za kifugaji basi mtusaidie waweze kusoma kwa maana ya kupata hela ya chakula ili wale watoto tuweze kuwa-accommodate kule kwa sababu wakirudi majumbani mwisho wa siku wanaolewa. Kule kuna ndoa ambayo Mkuu wa Shule akipewa ng‟ombe mmoja anaachia mtoto anakwenda anaolewa na anaolewa underage. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba zile shule zangu za Dongo, kuna Engusero, kuna Resoit Secondary School, kuna Rarakin Primary School. Hizi shule tunaomba zipate msaada wa kupata hela ya chakula ili watoto waweze kulala bwenini na wote tuwabebe wakae huko wasiweze kutoka kwenda kuolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunamshukuru Mheshimiwa Rais, ali-plan na sasa tumefikia, changamoto zipo, ni nyingi, lakini tuna hakika kwa kushirikiana tutaweza. Naomba niseme, Bunge hili lilikwenda likazuia kidogo fimbo za makalio kidogo na kwenye mikono, hebu turudishe fimbo watoto wajue kwamba jamani kuna malezi. Turudishe bakora kidogo kwenye mikono; Walimu wanadharaulika! Wakisema, hawasikiki! Hebu turudishe huo utaratibu jamani, turudi tulikotoka. Sisi ni Waafrika. Ni lazima kuwa na nyenzo kidogo twende, hatutafika!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hebu ajitahidi aangalie namna ya kuliweka hili, fimbo zirudi kidogo. Aombe huko juu fimbo zirudi halafu watoto waanze kuogopa, hata wawahi shuleni wakasome wakiambiwa wasome; wakikemewa wakimbie, wakiitwa waje wanakimbia. Discipline iwepo. Walimu wanatukanwa shuleni na mtoto wa Darasa la Tano na wazazi twende tukaseme. Waheshimiwa Wabunge nanyi semeni huko tushinikize hili tuondoe tabia utovu wa nidhamu, halafu watoto warudishiwe fimbo kidogo halafu mambo yasonge mbele.
Mheshimiwa Waziri, naomba kusema kwamba nakushukuru lakini anza na primary mwaka huu, umalize matatizo ya primary; mwaka kesho sekondari, mwaka kesho kutwa vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha, naunga mkono hoja. Ahsanteni sana.