Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
Ex-Officio
Constituent
None
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia kwenye hoja iliyoko mezani. Mchango wangu nitajielekeza zaidi hasa katika kutoa ufafanuzi kwenye mojawapo ya masuala yaliyoibuka wakati wa mjadala. Nielezee zaidi position ya kisheria iko namna gani na hili ni suala la fidia kwa walioathiriwa na uchafuzi wa mazingira uliotokea katika mgodi wa North Mara Gold Mine unaoendeshwa na Kampuni ya Acacia kule Nyamongo.
Mheshimiwa Spika, pendekezo lililotolewa ilikuwa ni kwamba fine ile ambayo imetozwa kampuni hii basi ingefaa fine hiyo igawanywe kwa wale waathirika wa uchafuzi wa mazingira, lakini basi kama hili haliwezekani, labda itafutwe namna yoyote ya kuwafidia hao walioathirika na uchafuzi wa mazingira uliosababishwa na huo Mgodi wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya ACACIA.
Mheshimiwa Spika, katika hilo nataka kusema kwamba kuigawa ile fine iliyotozwa kwa waathirika wa mazingira kuna ugumu kidogo kwa sababu hakuna Sheria inayoweza kuruhusu kufanyika jambo hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lile suala la kuichukua ile fine iliyotozwa na NEMC halafu kuigawa kwa wale wananchi walioathirika hilo jambo lina ugumu kwa sababu hakuna Sheria inayoruhusu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu fidia kwa walioathrika na uchafuzi wa mazingira sheria ipo. Ni hii Sheria inayohusiana na ulinzi wa mazingira (Environmental Management Act) na napenda hapa nisome tu kwa haraka hiki kifungu kwa sababu ni kifungu cha 110(1)(3). Kifungu cha 110 cha hii Sheria ya Environmental Management Act tukianza na kifungu cha kwanza kinasema:
“No person shall discharge any hazardous substance, chemical oil or mixture containing oil in any waters or any segment of the environment”
Hicho ndiyo kinachoanza kuweka zuio na katazo la uchafuzi na kifungu cha 110(3) kinasema:
“Apart from the general punishment provided for under this Act, the person convicted of an offence under this section may be ordered by the court”
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunakwenda kifungu kidogo cha 110(3)(b) kinasema:
“To pay the cost of third parties in the form of reparation, restoration, restitution or the compensation as may be determined by the court”.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika msimamo wa kisheria kuna uwezekano wa hawa watu walioathiriwa na uchafuzi wa mazingira kulipwa ama reparation au compensation au kwa namna yoyote itakayowezekana, lakini ni lazima tuangalie kitu kimoja hapo kwamba hii amri inatolewa na Mahakama na kwa sababu hiyo ni lazima pawe pamefunguliwa kesi ya jinai na Mahakama baada ya kupata ile kesi na uthibitisho ukatolewa inaweza kutoa maelekezo ya kulipa fidia.
Mheshimiwa Spika, katika mazingira tuliyonayo tuna changamoto kidogo, kwa sababu ukienda kifungu cha 194(2) cha Sheria hii hii kinasema, mahali ambapo kosa limekuwa compounded kwa ajili ya yule aliyetenda kosa kutoa fine, basi kesi ya jinai au kesi nyingine yoyote ya kimahakama haiwezi kuendelea kwa sababu itakuwa ni kama umetoa adhabu mara mbili.
Mheshimiwa Spika, sasa lakini hiyo haiondoi ukweli kwamba suala la fidia kwa watu walioathiriwa na uchafuzi wa mazingira ni la muhimu kuangaliwa. Kwa hiyo pengine labda baada ya hatua hii ya kulipa fine labda inaweza ikaangaliwa pia hiyo hatua nyingine hapo baadaye ya kulipeleka shauri hilo Mahakamani ili Mahakama itumie mamlaka yake kutoa maelekezo ya kuwalipa fidia walioathrika.
Mheshimiwa Spika, naomba kuhitimisha na naunga mkono hoja. (Makofi)