Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kigoma Kusini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na timu yote ya Wizara kwa kazi kubwa wanayoifanya. Natambua kwamba hawalali wanafanya kazi lakini sisi kama wawakilishi wa wananchi tunapoona wanapita huko mikoani lakini umeme hauwashwi kwenye vijiji lazima tuseme tunapopata nafasi hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri umeme kwenye Kijiji cha Nyanganga wameshawasha na wananchi wanashukuru sana kwa jitihada alizozifanya. Hata hivyo, tuna tatizo kubwa katika Mkoa wa Kigoma, nguzo na vitendea kazi vingine bado havijawasili katika mkoa wetu. Sasa tunashindwa kufahamu, ni lini wakandarasi hawa wataanza kupeleka nguzo Nguruka ili vijiji vyangu vya Chagu, Kijiji cha Mganza, Kijii cha Mtegowanoti, Kijiji cha Nyangabo, Kijiji cha Nguruka, Kijiji cha Bweru, Itebula, Mganza, Kasisi, Mlyabibi, Mpeta na kuendelea, lini watapelekewa nguzo ili angalau umeme sasa uweze kuwafikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri anatambua kwamba jiografia ya Jimbo langu ni mbaya, wananchi wa Ukanda wa Ziwa Tanganyika kwa maana ya Kata ya Mwakizeja, kuna vijiji kama viwili havijapelekewa umeme, lakini Kata ya Ilagala. Tatizo langu mimi kama mwakilishi wao, tangu survey ile ya kwanza waliyoifanya mpaka leo hakuna kinachoendelea. Sasa ninawiwa kwenye kushika shilingi na naomba kabisa niwekwe kwenye list ya kushika shilingi ili niweze kuambiwa ni lini vifaa vitapelekwa kwenye vijiji vyangu 24 ili sasa kazi ya kupeleka umeme iweze kuanza mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri afanye ufuatiliaji wa kina kwa mfano, tunacho Kitongoji cha Muyobozi na Kijiji cha Kabeba. Tangu mwaka jana mwezi wa Saba (7) wenzao wamewashiwa umeme, wao waliwashiwa siku moja, siku ya pili wakabeba transformer wakazipeleka Kigoma Mjini. Sasa swali langu, tangu nimelia kwa Waziri kwamba Muyobozi na Kabeba wawashiwe umeme hawajawashiwa umeme, basi waende wakang’oe nguzo. Wakang’oe nguzo, wakang’oe nyaya ili wananchi waache kuonga nyaya na nguzo kwa mwaka mzima, umeme hawawashiwi, tatizo liko wapi? Nimeshalalamika sana kwa Mheshimiwa Waziri, safari hii nitashika shilingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kwenye vijiji vyangu vya Kata ya Kalya, tulikubaliana vizuri REA awamu ya tatu kwamba Kijiji cha Ubanda, Lufubu, Kashaguru, Tambusha, Kalya na Sibwesa watapata umeme kutoka Ikola au kutoka Mwese. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, hadi leo ninavyoongea hakuna survey yoyote iliyofanywa kwenye hivi vijiji sita, sasa wananchi wamenituma niulize, hii ndiyo bajeti ya mwisho. Bajeti hii tunalialia hapa kwa sababu bajeti inayokuja tunakwenda kwenye uchaguzi, sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa kuhitimisha nataka nijue hivi vijiji sita ndani ya Kata ya Kalya vinapata lini umeme kutoka Ikola au Mwese ili tujue way forward.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa Hasna, ahsante sana kwa mchango wako.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)