Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Mtwara Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kupata fursa ya kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Nishati.
Mheshimiwa Spika, nianze kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayoifanya. Nadhani sifa ambazo wanapewa kwa kweli wanastahili sana; si wachapakazi tu lakini pia ni wasikivu, wanyenyekevu na wanashaurika, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda wangu ni mchache, naomba niende moja kwa moja katika maeneo ya Jimbo langu. Nishukuru sana kwamba vijiji vingi katika Jimbo langu vimepata umeme lakini nina kata mbili; Kata ya Muungano na Kata ya Moma hazina hata kijiji kimoja ambacho kina umeme. Nikushukuru Mheshimiwa Waziri juzi ulivyokuja umeniahidi vijiji viwili katika Kata ya Muungano na Vijiji viwili katika Kata ya Moma, nakushukuru sana na pia umeniahidi umeme katika Sekondari ya Nanguruwe. Pia niombe umeme katika sekondari yangu ya Lilido na yenyewe Mheshimiwa Waziri nayo niweze kupata umeme ili wanafunzi wangu waendelee kufanya vizuri.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana kwa kuanzisha mpango wa kupeleka gesi ya majumbani. Mwaka jana tulifanya uzinduzi pale katika Sekondari ya Mtwara kwa sababu sasa hivi inachukua na wasichana, Sekondari ya Ufundi Mtwara lakini mradi ule naona kama unaenda taratibu na nilivyosoma katika kitabu chako cha hotuba naona kwamba bado mko katika usanifu. Nikuombe Mheshimiwa Waziri huo usanifu uharakishwe ili mradi ule uanze kutekelezwa kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri, eneo ambalo ningependa kulisisitiza ni suala la utoaji wa leseni za utafutaji na uendelezaji wa gesi. Mheshimiwa Waziri nimeshakuja kwako zaidi ya mara mbili na Kampuni ya Ndovu Resource wakiomba leseni kwa ajili ya kuendelea kutafuta gesi na pia wakiomba leseni kwa ajili ya kuendeleza maeneo yale ambayo tayari gesi imepatikana, huu unaingia mwaka wa pili. Mheshimiwa Waziri nikuombe chondechonde tunasema kwa Kimakonde hivi vibali au hizi leseni kwa nini zinachukua muda mrefu hivi? Mji wa Mtwara sasa hivi unasinzia, kipindi kile wakati utafutaji unaendelea, mji ulichangamka na uchumi ulikuwa unakua.
Mheshimiwa Spika, tukuombe hayo majadiliano yakamilike, mnachojadiliana ili leseni zitolewe kwa watafutaji wa gesi na wale ambao tayari wameshapata gesi wanataka kuendeleza vitalu vyao haswa hao watu wa Ndovu Resource wamechimba katika Jimbo langu wamegundua zaidi ya maeneo matatu, sasa wanaomba leseni ya kutaka kuendeleza shughuli tangu mwaka 2017 mwezi wa kumi wameleta maombi mpaka leo bado majadiliano naambiwa sijui mkataba upo kwa AG.
Mheshimiwa Spika, nakusudia kutoa shilingi ili niambiwe ni lini leseni zitatolewa kwa watafutaji na waendelezaji wa gesi kwenye vile vitalu vyao. Mheshimiwa Kalemani tangu umeingia hujatoa leseni hata moja na watu wapo wanaotaka kutafuta hiyo gesi, wapo wanaotaka kuendeleza hizo gesi lakini leseni imekuwa ni mtihani.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa AG bahati nzuri upo, utasaidia katika kurudisha hiyo shilingi ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu Waziri hastahili hata kidogo kunyang’anywa shilingi lakini naambiwa mambo yote yapo kwako lakini ili nifike kwako ni lazima nipitie kwa Waziri. Kwa hiyo, nitachukua shilingi ya Waziri ili Mheshimiwa AG ufanye kazi kwa haraka ya kumuwezesha Waziri kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili ambalo nilitaka nalo nipate ufafanuzi ni kuhusu Kiwanda cha Mbolea cha Msanga Mkuu kupitia Kampuni ya HELM…
SPIKA: Bahati mbaya dakika tano zimeisha.
MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuunga mkono hoja lakini Msanga Mkuu na suala la leseni nipate majibu. (Makofi)