Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. UPENDO F. PENEZA: Ahsante Mheshimiwa Spika, na nina mshukuru mungu kwa kunipatia fursa hii kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Nishati. Kama ambavyo umekwisha sikia wachangiaji wengine waliotangulia ni kwamba Bunge lako Tukufu ama Wabunge ambao wako ndani ya Bunge hili wana-concerns zao katika vitu viwili. Kuna concern ya kwanza kwa maana ya gharama, na kuna concern ya pili kwa maana ya mambo ya kimazingira yanayozunguka mradi huu wa Stiegler’s Gorge.
Mheshimiwa Spika, lakini katika suala zima la gharama leo tumeambiwa na Serikali na tumekuwa tumeambiwa tangu bajeti iliyopita kwamba mradi huu utagharimu trilioni 6.5. Lakini ukiangalia katika namna ambavyo Serikali imekuwa ikitoa hela mpaka sasa, ni dhahiri kwamba mradi huu hauwezi kuisha kwa miaka mitatu kama ambavyo Serikali inatuambia na kama haitaweza kuisha kwa muda wa miaka mitatu, maana yake ni kwamba tutalipa hela zaidi, tutalipa hela zaidi na hatimaye inawezekana tukafika hata kwenye gharama tunazoambiwa za trilioni 22.9.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti iliyopita Serikali ilitenga bilioni 700 lakini mpaka tuna.. kwa maana mpaka mwezi Desemba ulikuwa umetoa mia mbili sabini na kitu baadaye wamemalizia hizo bilioni 688 ambazo na bado hawajamalizia kwa maana ya kumlipa mkandarasi wa anayejenga huo mradi wa Stiegler’s Gorge. Na sasa hivi tumetoa trilioni 1.4 maana yake ni kwamba kama Serikali inakusudia kwamba tumalize huu mradi kwa miaka mitatu, ni kwamba ingekuwa inatoa zaidi ya trilioni 2 kila mwaka, ili kuhakikisha kwamba mradi huu unaweza kuisha kwa hiyo miaka mitatu ambayo imetengwa.
Mheshimiwa Spika, lakini zaidi ya yote ni kwamba leo tunazungumza gharama ya trilioni 6.5 kwa kujenga mradi mmoja. Mradi ambao ukiangalia kimazingira, watu wanaonesha concern kubwa na hata kama ukiuangalia mradi huu wenyewe je tukimaliza kujenga maji yatajaa kwa kutumia miaka mingapi ndani ya dam ili kuhakikisha kwamba huo umeme unaweza kupatikana.
Mheshimiwa Spika, tumeambiwa kwamba itatumia takriban miaka 10 ili dam hiyo iweze kujaa maji na hatimaye kuzalisha umeme, kwahiyo mpaka kupata umeme huo wa megawatt 2100, itatumia takriban miaka 27. Sasa kwa namna hiyo maana yake ni kwamba tunatumia hela nyingi kujenga kitu ambacho hatutapata matokeo ya haraka kama ambavyo tunategemea.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, leo tunawaaminisha watanzania kwa kiasi kikubwa sana kwamba huu mradi ukiisha tutapata megawatt 2100 kitu ambacho si kweli. Lakini hata ukiangalia miradi ambayo imekwishaendelea ambayo inatumia maji kuna miradi ya Kihansi na hapo Mtera mpaka leo hii hakuna hata asilimia 40 ya uzalishaji unaoendelea katika maeneo hayo. Kwa hiyo, kama mifano tuliyonayo leo haitoi picha halisi mnatuambia vipi, kwa huo mradi ambao mnasema kwamba baada ya miaka mitatu utafika huko. Maana yake ni kwamba inawezekana tunataka tutengeneze historia kwamba awamu hii ilijenga huo mradi tukatelekeza vingine na ni uharibifu wa hela kama hatuwezi tukapata matokeo ya haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia vile vile tumeongelea suala zima la gesi na kuna pia vyanzo vingine ambavyo watu wamesema mix energy lakini katika hilo suala ukiangalia katika bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri ameiwakilisha hapa tuna miradi ya jua, tuna miradi ya upepo, tuna miradi ya maji hata katika maeneo mengine yote hii hiyo hela ya trilioni 6.5 kama ingegawiwa kwenye hiyo miradi midogo midogo tungepata zaidi ya hizo megawatt 2100 tena kwa haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na zaidi ya hapo ni kwamba kama mradi wa umeme ungetengenezwa katika eneo moja usambazaji ungefanyika na hizo megawatt kuingizwa katika megawatt kuingizwa katika grid ya Taifa hata usafirishaji wa umeme kwenda kwa umbali mrefu kusingekuwa na upotevu wa umeme kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, tungeweza kuzalisha umeme wananchi wakapata umeme katika maeneo mbalimbali kwa kutumia hizo hizo trilioni 6.5 lakini kwa kuangalia au kuvipa vipaumbele miradi ambayo Serikali yenyewe imeweka kuna miradi ya maji, kuna miradi ya umeme, kuna miradi ya upepo ambayo Serikali sasa inaitupa pembeni na ukiangalia katika bajeti nzima ya maendeleo Serikali imetenga trilioni 2.1, trilioni 1.4 yote inatumika kwenye mradi wa Stiegler’s tunabakiza bilioni 68 tu itumike katika miradi mingine na kusambaza umeme katika maeneo mbalimbali kitu ambacho hakitupi picha halisi ya Serikali kutaka kuifanya Tanzania hii, Tanzania ya viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia ninaomba nizungumzie kuhusu suala la gesi. Naomba nizungumzie suala la gesi Tanzania ni katika nchi ambayo imekubali kufanya uvunaji wake wa gesi katika njia ya production sharing. Kwamba Kampuni ya TPDC inaingia pamoja na hawa wawekezaji na kuna mgawanyo kwa maana ya pesa ya ku-invest lakini pia kuna kugawana baadaye baada ya kuivuna hiyo gesi yenyewe. Lakini pamoja na matatizo yote ambayo TPDC wanayo ukosefu wa hela ya kuwawezesha wao kufanya utafiti na vitu mbalimbali lakini bado wanaweza kupata mgao wa gesi kupitia hii production sharing agreement.
Mheshimiwa Spika, sasa tulipitisha hapa sheria ndani ya Bunge mwaka 2017 sheria ambazo zimefanya wawekezaji ambao wako katika upande wa gesi kukimbia na leo hii hatuna uzalishaji mkubwa katika upande wa gesi, gesi ni kama vile imelala sasa. Lakini katika Bunge lililopita, Bunge hili lilikaa na tukapitia upya vipengele ambavyo vilikuwa vinawakandamiza wale wachimbaji wadogo wadogo na tukasahihisha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, natumia muda huu kukuomba kwamba kamati inayohusika na mambo ya madini na nishati, iweze kukaa pamoja na Serikali pamoja na hawa wawekezaji kujadili ni changamoto gani ambazo zipo katika hizo sheria na hatimaye tutoke na njia moja ya kuweza kusahihisha mapungufu yaliyopo ili tupate njia ya kwamba tupate gesi, huku na miradi mingine inaendelea ili kuhakikisha tunapata hiyo mix energy production katika nchi hii kama ambavyo imekuwa ikisemwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haitaleta maana kama nchi imetumia takriban trilioni 3 kujenga bomba leo hii halina faida kwa nchi ni asilimia 6 tu haileti faida wala haileti value for money, kwa hiyo ni bora tukaboresha hizi sheria tukawekeza tukapata gesi na uzalishaji wa umeme pamoja na matumizi mbalimbali ya gesi yakaweza kuendelea ndani ya nchi hii.
Mheshimiwa Spika, la mwisho ni kwenye upande wa REA, kamati imetuonesha changamoto ambazo zipo katika mradi wa REA kwamba kuna ucheleweshwaji wa Serikali kutoa hela, kwa hiyo mnachelewesha katika huduma hizi za umeme wa REA kufanya kazi na huduma mbalimbali katika maeneo hayo, na hatimaye inazalisha ongezeko la pesa kwa maana ya hii mikataba wale contractors wanadai hela nyingi zaidi.
Mheshimiwa Spika, lakini zaidi ya hapo pia hata wale contractors wenyewe wale waliofanya hizo kazi, na wenyewe pia wapo wanaochelewesha kazi hizo ni vizuri sasa Serikali ikaunda kitengo maalum cha monitoring and evaluation kwa ajili ya kazi hii tu ya umeme wa REA kuhakikisha ya kwamba wanaweza kuwasukuma wale contractors waliowapa kazi lakini na wenyewe pia waweze kutoa hela kwa wakati na kuwapa mikataba kwa wakati kuhakikisha kwamba miradi hii inaweze ikafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, na kwenye hilo kwangu kwa upande wa Geita Serikali ilituahidi kutupa umeme kwa kupitia njia ya REA katika maeneo ambayo yanaitwa ni mitaa lakini kihalisia ni kama vile vijiji sasa tunaiomba Serikali iweze kutukumbuka katika Kata za Ihanamilo, Kata za Shiloleli, Kata za Bungw’ang’oko na maeneo mengine yote kuhakikisha kwamba umeme unaweza ukapatikana na ripoti ya kamati imeonesha kwamba Geita iko chini ya asilimia 40 na sisi tunahitaji umeme katika maeneo hayo kwa hiyo, tunaomba walau tuweze kupata umeme kupitia njia hii ya REA. Ahsante sana nashukuru. (Makofi)