Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, kwanza nikushukuru sana kunipa fursa nami niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati. Awali ya yote kwanza nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutupa kibali kuwepo katika Bunge lako hili Tukufu. Lakini kipekee sana nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya katika Wizara hii ya Nishati na kwa Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wako mmekuja Jimboni kwangu Busokelo na mlifanya mikutano hata saa mbili usiku ilibidi kufanya ili tu wananchi wa Jimbo la Busokelo wapate umeme. Katika hili nawapongeza sana kwa niaba ya wananchi wangu Jimbo la Busokelo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina machache katika Wizara hii ya Nishati kwa sababu kwenye awamu ya kwanza REA III mzunguko wa kwanza Jimbo langu lilipata vijiji 50 kati ya vijiji 56 na katika hivi vijiji 50 ni vijiji 42 ambavyo vimepewa kipaumbele katika awamu hii ya REA III, kwa hiyo nipongeze sana Serikali katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba tumepata vijiji 42 kuna changamoto ambazo zimeambatana na mkandarasi kwanza kwa kuviacha vile vijiji 8 ambapo Mheshimiwa Waziri ulipokuja ulitoa amri na kauli kwamba lazima atekeleze vyote pasipo kujali aina ya nyumba ya nyasi ama si ya nyasi ama ya bati kwamba vyote vinastahili vipewe umeme.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, ningependa kushauri katika jambo hili la kupeleka umeme katika huduma za jamii, kuna baadhi ya maeneo hasa hasa mashule, zahanati, hospitali, makanisa vimerukwa. Kwa hiyo, ningeomba katika awamu hii ambayo tunaingia mzunguko wa Awamu ya III wa REA viweze kupatiwa maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine mwenzangu ameshauri hapa kwamba kuna baadhi ya vitongoji hasa hasa umeme unapofika kwenye kijiji kimoja ambacho kina vitongoji vitano na kinafika kwenye kitongoji kimoja vitongoji vingine vyote vinne vinakuwa havijapata umeme hii inakuwa ni shida sana kwa wakazi jirani. Nafikiri katika mpango huu wa Awamu ya III mzunguko wa pili, ingefaa sana kwanza umeme unapofika kwenye kijiji basi na vitongoji vyake vyote viweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ningependa kushauri ni suala hili la miundombinu hasa hasa baadhi ya wakandarasi wanapopeleka hizi nguzo katika baadhi ya vitongoji ama vijiji, wanaweka karibu sana na miundombinu ya barabara na wakati mwingine watu wa TARURA wanapotaka kuanza kutengeneza zile barabara wanashindwa kwa sababu tayari nguzo zimeshasimama karibu kabisa na barabara nafikiri kungekuwa kuna umuhimu wa kushirikisha taasisi na Wizara zingine hasa hasa Wakala wa Barabara Vijijini ili wawe na umbali kiasi fulani ambapo itawezesha hizo nguzo ziweze kuwekwa badala ya kuweka karibu sana na barabara na baadaye inakuwa gharama tena ya kuanza kuzitoa maeneo yale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ningependa kushauri suala la kukatika katika umeme Mkoa wa Mbeya na Wilaya zake zote ni miongoni mwa Mikoa ambayo umeme unakatika mara kwa mara na hasa katika Wilaya za Kyela, Rungwe, Busokelo, Mbeya Vijijini, Chunya, hadi Mbarali na hii yote ni kwa sababu ya miundombinu imechakaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningeomba kwamba Mheshimiwa Waziri kwa sasa tuna teknolojia nyingi ya kusimika nguzo na kwa kuwa kule mvua nyingi zinanyesha karibia mwaka mzima na upepo unakuwa ni mwingi sana nafikiri tungetumia teknolojia ya kuweka nguzo ama nyaya kwa maana ya underground badala ya kuweka angani ambapo kila mara baada kupigwa na upepo ama ikipigwa na mvua ama na radi mvua umeme unakatika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine napenda kuzungumza suala la TPDC, TPDC ni shirika ambalo hakika mimi ni mjumbe wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma linafanya kazi nzuri na tumejionea sisi wajumbe namna ambavyo wameanza mchakato na kuona hata nyumba ambazo zinapata umeme kwa kupitia njia ya gesi. Pia tumeshuhudia hata magari ambayo yanatumia gesi ya Kitanzania, ambayo inachakatwa kule Mtwara. Kwa hiyo niwapongeza sana TPDC pamoja hata na wataalam ambao akinamama wapo pale ma-engineer na ni wazalendo Watanzania. Kwa hiyo niwapongeze sana uongozi wa TPDC pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa shirika hili.

Mheshimiwa Spika, changamoto ambayo wanayo TPDC hasa hasa katika suala zima la gesi asilia ambapo baadhi ya taasisi zingine zinapewa fedha kwa ajili ya kutengeneza miradi yao, lakini wao wanapewa fedha kwa maana ya kutengeneza mradi ambao fedha baadaye itakuwa claimed na TPDC.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mwakibete.

MHE. FREDY A. MWAKIBETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)