Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Kavuu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi nami niweze kuchangia katika hotuba hii muhimu ya Nishati. Kwanza kabisa napenda niwapongeze viongozi wa Wizara hii wakiongozwa na Dkt. Kalemeni pamoja na watendaji wengine Wizara.
Mheshimiwa Spika, naomba niende moja kwa moja katika ukurasa wa 44 katika hotuba ya Waziri ambao unaongelea mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV 400, mradi ambao unaanzia Iringa unakuja kufika mpaka Nyakananzi na unatekelezwa kwa awamu tatu. Niwashukuru kwamba mradi huu umeweza kuwekwa hata kwenye mpango na katika kazi zilizofanyika 2018/2019 ni pamoja na upembuzi yakinifu kati ya Mbeya na Sumbawanga na uthamini wa mali kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri kwa kuwa mradi huu umeshafanyiwa uthamini na upembuzi yakinifu, basi ni vema sasa wakatafuta huyo mkandarasi wa kuweza kuratibu mradi huu ili uweze kufanya kazi. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu umeme wanaotumia hasa kutoka tunduma mpaka Sumbawanga umeme ule mwingi unatoka Zambia na umekuwa ukikatika mara kwa mara. Sasa tuondoshe hii adha ya wananchi wa maeneo haya ambao ni pamoja na Jimboni kwangu Kavuu katika Kata ya Kibaoni ambapo pia wanatumia umeme huu ambao umekuwa ukikatika mara kwa mara na hivyo kuwafanya wananchi ambao wamejiajiri kupitia sekta hii kutoweza kufanya maendeleo yao vizuri.
Mheshimiwa Spika, naomba nirudi katika Kata yangu ya Kibaoni katika Jimbo la Kavuu. Naomba niongelee transformer ya Kijiji cha Mirumba, transformer hii imekuwa ni tatizo, kila leo nimekuwa nikisema. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja anieleze tatizo lipo wapi katika transformer katika Kijiji cha Mirumba ambayo inapokea umeme kutoka Sumbawanga kupeleka pale Kibaoni ambapo umekuwa ukikatika karibu kila siku, kila siku kwa kisingio cha transformer. Kwa hiyo niombe kama transformer hiyo ni mbovu naomba mbadilishe transformer pale ili wananchi waendelee na shughuli zao za utekelezaji wa shughuli zao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba nije katika Mradi wa REA awamu hii, naishukuru sana Serikali kwa sababu wameweza sasa na sasa hivi ninavyoongea wakandarasi wapo kule jimboni kwangu katika Kata ya Majimoto na Kasaka wakiendelea na kuweka nguzo. Kwa hiyo niombe sasa katika vijiji vilivyorukwa katika Kata ya Kasansa, ambavyo nasema ni Iziwasungu, Majimoto kuna Kijiji cha Luchima ukija Mbede kuna Kijiji cha Kansisi ukija Mbede hapo hapo kuna kijiji cha Nyambwe ukija Kata ya Majimoto kuna Kijiji cha Lunguya; naomba vijiji hivi viingizwe kwenye mradi kwa sababu vimerukwa na vipo kwenye mradi. Waziri alipokuja tulipoenda Majimoto aliongea kwamba ni lazima vijiji vyote viingizwe na vitongoji vyake kwenye njia hii ya umeme wa REA, awamu ya tatu ili wananchi na sisi kule tupate kuona umeme, kwa sababu nitoka uhuru hatujaona mwanga wa taa.
Mheshimiwa Spika, tunaomba sasa na kazi ya huyo mkandarasi iwe kubwa kiasi kwamba wananchi wana hamu ya kuwekeza. Mheshimiwa amefika Majimoto, yeye mwenyewe anapapenda na anataka awekeze pale, kwa hiyo namwomba sasa, kasi pale ya kusambaza huo umeme wa REA iwe kwa kasi kubwa ili tuweze kuendelea na shughuli zetu za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niliwahi kuongelea suala la nguzo zinazowekwa na TANESCO. Unaenda kuomba kuwekewa umeme, TANESCO wanakuletea nguzo unalipia laki tatu mpaka laki tano, lakini kuna mwingine jirani atataka naye kuunganishwa umeme atatumia ile nguzo, zimekuwa zikileta matatizo hasa kwa wananchi huku kwenye maeneo ambapo naye anataka kuunganishiwa kwenye ile nguzo, kwa nini? Kwa sababu yule aliyeweka mwanzo naye anataka arudishiwe gharama.
Mheshimiwa Spika, nashauri kwa sababu tunalipa umeme kila mwezi, kwa nini nguzo hizi ziwekwe bure ili wananchi waweze kupata na kuweka umeme kwa urahisi, kwa sababu hata hapa Dodoma wapo wanaoshindwa kuweka umeme kwa sababu tu ya gharama za nguzo. Kwa hiyo, niombe kama kweli tuna nia ya dhati na wananchi wetu wapate umeme basi wananchi nguzo ziwekwe bure kwa sababu tunalipia umeme. Kwa hiyo kama tunalipia naomba hizo nguzo ziwekwe bure.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda ni mchache, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)