Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CHADEMA
Constituent
Bukoba Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILFRED M. LWAKATARE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana. Kwanza nipongeze hotuba ya Kambi ya Upinzani ambayo imejaribu kurejea mambo mbalimbali ambayo yanapaswa kuzingatiwa na Wizara hii ili waweze kuyafanyia kazi mambo ambayo yametolewa kama ushauri na mambo ambayo wameweza kuyaainisha kama sehemu zenye kasoro ndani ya Idara mbalimbali za Wizara hii. Pia nipongeze hotuba ya Kamati ambayo pia imeainisha mambo mbalimbali ambayo yanapaswa kuzingatiwa na Wizara hii ambayo bajeti yake tunaijadili.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia, kwa ufupi kabisa kutoa pole kwa wananchi wa Manispaa ya Bukoba ambao wamepatwa na dhahma ya mafuriko na ambapo mpaka sasa hawajaweza kukaa sawa. Ninaamini kwamba Wizara hii itajaribu kurudisha kwa kasi sana miundombinu ambayo ya umeme ambayo imeharibiwa na mafuriko haya ili watu waweze kurejea katika hali iliyo salama na kuendelea kutumia nishati ya umeme.
Mheshimiwa Spika, Katika tamko la Serikali ambalo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa aliainisha bayana kwamba Serikali inatoa ushauri na msukumo wananchi waanze kuhama katika maeneo mengi ya Mji wa Bukoba kwenda katika maeneo ya Vijiji Mji, ambavyo ni Nyanga, Kahololo, kuna Vijiji vya Ijuga Nyondo, Kibeta na Kagondo. Vijiji hivi, kama ambavyo nimekuwa nikieleza huko siku za nyuma, na Mheshimiwa Waziri anajua, sehemu nyingi hazina umeme. Sasa kama alternatively ya kukimbia mafuriko imekuwa kwenda kwenye vijiji hivi naomba huu mpango wa kuweka umeme kwenye Vijiji Mji uweze kufanyika kwa haraka katika Mji wa Bukoba ili watu waweze kupata huduma hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Pamoja na mambo mbalimbali ambayo yameshauriwa katika hotuba ya Kambi ya Upinzani na Kamati ya Nishati ningeomba kutoa ushauri kwa mambo mbalimbali yafuatayo.
Mheshimiwa Spika, Mradi wa REA ni miongoni mwa Miradi ambayo inapata fedha, au ina vyanzo vya uhakika vya kupata fedha. Lakini pamoja na uhakika wa vyanzo hivi tumeona kupitia katika hotuba hususani ya Kambi Rasmi ya Upinzani figisu zinazojitokeza hasa za matumizi mabaya au usimamizi mbaya wa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nimejikita zaidi kuangalia tatizo linaweza likawa nini. Mimi binafsi sikubaliani na mfumo wa usimamizi wa fedha unaotumika ndani ya REA. Kuifanya TANESCO kuwa mshauri au kuwa consultant wa hii Miradi ya REA ni jambo kidogo ambalo mimi nafikiri linakosesha transparency inayopaswa kufanyika kwa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Ni vyema REA ikawa na ma- consultant, ikatangazwa nafasi ya consultant, kazi za consultant, ili TANESCO ambayo kimsingi nayo unakuta kuna wakati inakuwa ni Kampuni shindani kwenye baadhi ya Miradi, lakini pia ni Kampuni ambayo inakuja kurithi Miradi ya REA; unapomfanya ni consultant mimi naamini unatoa nafasi ya baadhi ya mambo kufukiwa ndani kwa ndani na hata kufanya kazi ya trace, hata kama pesa imekuwa misused inakuwa ni kazi ngumu kwa sababu msimamizi ni yule yule, huyo huyo anachukua contract na anashindana na Kampuni nyingine. Hata wakati mwingine tumnapata taarifa kwamba nguzo ambazo TANESCO kama consultant anazikataa wakandarasi wasizitumie yeye anapokuja kufanya kazi yeye anatumia nguzo hizo hizo wakati ambapo anakuwa amezikataa kwa wakandarasi binafsi; hii ni double standard. Mimi ushauri wangu ni huo; kwamba kwa kweli ifike mahala hizi kazi wapewe ma-consultant ili TANESCO naye asimamiwe badala ya kuwasimamia watu wengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la tatu ni suala ambalo limezungumzwa katika hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambapo mara nyingi Wizara au taarifa mbalimbali zinazotolewa na Kampuni za TANESCO, REA wamekuwa wanatumia kigezo cha kijiji usambazaji wa umeme kwa kigezo cha vijiji. Kama Kambi ilivyo shauri, ni vyema tukaanza kutumia kaya, Maana katika maeneo mengi tunaambiwa vijiji kadhaa vimepewa umeme au vimesambaziwa umeme lakini ukienda kwa uhakika unakuta kuna vitongoji vingi mno, vinakuwa havijapewa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, unakuta kwenye kijiji ziko kaya kama 30, 40 lakini maeneo mengine ya vijiji, tukija hapa Bungeni tunaambiwa takwimu chungu nzima ya vijiji kwamba vimepata umeme; hii tunakuwa tunajitekenya na kucheka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kamati yetu imekuwa inaomba sana kukutana na wakandarasi ili waeleze maeneo wanayokwama, lakini imekuwa kizungumkuti, sasa nitaomba kujua kupitia kwa Waziri wakati ana-windup; tatizo liko wapi kwa Kamati kukutana na Wakandarasi? Kunafichwa nini la kutukutanisha na Wakandarasi hawa? Maana kukutana nao kutatupa picha wanakwama wapi au wanakwamishwa wapi na Serikali. Hata hivyo na wakandarasi wenyewe nasikia nao wanatishwa juu ya suala la kukutana na Kamati, wengine wanaogopa hata kukutana na Kamati kwasababu wanahisi wanaweza wakakosa hata tenda pindi wakija kuomba. Sasa ili tuwe wawazi mimi nafikiri mchakato wa kukutana na Wakandarasi ufanyike.
Mheshimiwa Spika, Suala la tano, gharama za kuunganisha umeme. Tulipokuwa kwenye Kamati, Waziri alizungumza bayana kabisa, kwamba kuunganisha umeme wa REA pamoja na ile miradi inayorithiwa na TANESCO unapaswa kutozwa 27,000, ndicho kiwango kinachopaswa kutolewa. Ili kuweka mambo bayana mezani tulimuomba Waziri na akaahidi kwamba utatolewa waraka ambao utagawiwa kwa Waheshimiwa Wabunge wote kipindi hiki cha bajeti waondoke nao kwenda kuwaelewesha na kuwafahamisha wananchi kwamba wasitozwe pesa zaidi ya 27,000. Mheshimiwa Waziri tutaomba waraka huo utoke kwa sababu ni ahadi yako, ili watu tuondoke nao twende nao huko na kuufahamisha Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mwisho ni Kuhusu Miradi Mikubwa. Ifike mahala Bunge linapokuwa linajadili mambo tuweke binding ya kutopindua maneno yetu. Nilikwenda library kusoma Hansard ya mwaka 2013/2014 baadhi ya Wabunge walioko humu ndio walishadadia gesi, kwamba gesi sasa tumepata biashara imekwisha mkombozi wetu ni gesi, na baadhi ya Wabunge wako humu, akiwemo na kaka yangu Mwijage. Leo hii wamehama wanakuja kwenye Stiegler’s Gorge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mimi naomba Bunge lijiwekee utaratibu wa kuweka binding ya maneno ambayo tunakuwa tumepitisha na kushadadia badala ya kuwa tunaokota huku tunakuja huku, kesho kutwa tunaokota hili tunakuja hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia ahsante sana. (Makofi)