Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimshukuru Mungu sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia Wizara ya Nishati, lakini zaidi sana nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mchango.

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kukupongeza sana, unapokaa kwenye kiti chako Bunge linaendeshwa kisayansi na linaendeshwa kwa utulivu mkubwa sana. Wabunge tunaheshimiana na kuthamini kila mchango wa Mbunge anayesimama na hivi ndivyo inavyotakiwa iwe hata kwa wenzako wengine wote unaowaachia nafasi ya kiti wanatakiwa kwa kweli kulinda heshima ya Bunge na hasa pale Mbunge anaposimama na kutoa mawazo yake ambayo pengine wewe unaona kwako hayakufurahishi lakini ni lazima umpe nafasi ya kumsikiliza na zogo la Bunge la juzi halikuwa jambo zuri sana.

Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi sana kwa Mheshimiwa Waziri Dkt. Mendrard Chanancha Matogolo Kalemani pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Subira Mgalu pamoja na Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara. Watu hawa wanafanya kazi kubwa ya kuzunguka nchi nzima, lakini kubwa zaidi kwao hawa wawili ni mahusiano mazuri na Waheshimiwa Wabunge. Hili ni jambo zuri sana, lazima kujenga PR ya pamoja maana hii kazi ni ngumu, kazi inahitaji ushirikishwaji na ushirikiano wa karibu.

Mheshimiwa Spika, vilevile spidi ya Mheshimiwa Waziri na Naibu wake naiona ni kubwa kuliko spidi ya makandarasi, yaani Waziri anagawa umeme kwa spidi sana kuliko wajenzi, kama ni forward wakati mwingine unasema inaweza ikaingia kwenye nyavu yenyewe ikaacha mpira nje, sasa kidogo hapo inatupa mazingira magumu sana.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie Jimbo la Mtera katika tarafa zangu tatu, Tarafa ya Mvumi Mission, Tarafa ya Makangwa na Tarafa ya Mpwayungu. Tunavyo vijiji ambavyo bado havijafikiwa umeme, lakini kama unavyojua ukijua kulaumu ujue na kushukuru. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kufikisha umeme kwa mara ya kwanza katika Tarafa ya Mpwayungu katika Kijiji cha Nagulo na Kijiji cha Mpwayungu chenyewe.

Nimwombe sana vile vitongoji anavyovitaja, vijiji anavyovitaja kwamba umeme hautamruka mtu, wale watu wanaorukwa wote kimbilio lao ni kwa Mbunge. Kwa hiyo unajikuta Mbunge anafanya kazi kubwa sana baada ya Waziri kuondoka, wakisema mbona Waziri alisema tusirukwe, sasa kwa nini tunarukwa. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake na timu nzima washughulike kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba yale maeneo waliyoagiza maagizo yao yanatekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ukisoma ilani za hivi vyama ambavyo vina Wabunge humu unaweza ukacheka sana. Nimepitia ilani ya CHADEMA hapa sioni mahali wameahidi megawati 18,000 alizokuwa anazisema mzungumzaji wa CHADEMA, kwa hiyo unaweza ukaona wakati mwingine maneno haya yanayozungumzwa ni maneno ya kufurahisha tu Bunge. Unajua faida kwenye uongozi wa nchi wakati mwingine haionekani moja kwa moja…

T A A R I F A

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Esther.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa Mheshimiwa Lusinde taarifa kwamba wakati Mheshimiwa Silinde anachangia alisema trilioni sita ambazo zinatarajiwa kujenga Stiegler’s Gorge zikilinganishwa na extension one ya Kinyerezi ambayo inajengwa kwa bilioni ambazo ni megawati 185 equivalent yake ni ya kujenga megawati 18,500, hakusema inatokana na Ilani ya CHADEMA.

SPIKA: Mzungumzaji pia hajasema hivyo kama inatokana ameuliza tu kwenye ilani yenu hakuona. Endelea Mheshimiwa Lusinde.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, shemeji yangu Matiko nataka nimsaidie tu kwamba unajua wakati mwingine faida kwenye shughuli za Serikali haifananishwi na faida ya genge la nyanya au pengine mgahawa. Huwezi ukaiona moja kwa moja wakati mwingine unaona MSD wananunua dawa nyingi mpaka zile za ugonjwa wa Ebola, sio mpaka wasubiri ugonjwa uwepo ndio wanunue.

Kwa hiyo, wakati mwingine tunasema kwa nini dawa zina-expire zina-expire kwa sababu zilikuwepo na ugonjwa haukutokea, sasa huwezi ukangoja mpaka utokee ndio uanze kununua. Kwa hiyo kuongoza Serikali tunawafundisha tu, ni mambo makubwa sana, huwezi kufananisha na biashara ya genge au mama ntilie, kwa hiyo kuna faida unaweza ukazitafuta kwa macho usizione.

Mheshimiwa Spika, nimezungumzia sana kuhusu kuwabana wakandarasi ili waendelee kusambaza umeme katika vijiji vyote. Tumeona namna ambavyo…

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde unapewa taarifa na Mheshimiwa Getere.

MHE.BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji anayeongea kwamba CHADEMA katika miaka ijayo itakapokuwa kwenye madaraka tutahakikisha tunafanya utafiti wa kina kuhusu vyanzo mbalimbali vya nishati hatimaye kutunga sera ya kupata nishati hizo. Kwa taarifa kamili ni kwamba mpaka leo CHADEMA haina chanzo cha nishati, kwa hiyo anachosema Silinde ni sawa tu.

SPIKA: Mheshimiwa Lusinde, tafadhali.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nimesema kuongoza nchi faida zake ni wananchi kunufaika. Sisi Rais wetu na Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kujitoa muhanga kujenga kinu cha kufua umeme katika maporomoko ya Rufiji. Haya ni maamuzi makubwa ambayo impact yake itaonekana wakati Watanzania watakapoanza kunufaika na ndio maana hakuna Mbunge humu ndani anayesimama na kusema umeme huo nisipewe humwoni. Kwa hiyo ni kweli kwamba Serikali imepatia na iendelee kujenga huo umeme ambao utatunufaisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa kwenye vijiji ambavyo vilikuwa vimesahaulika kabisa, tumeona mawaziri wetu wakiwasha umeme mpaka kwenye nyumba za nyasi, nyumba za tembe, kule waliko Watanzania, hili ni jambo jema. Tumeona umeme unawashwa mpaka Loliondo, kwa babu wa kikombe, hili ni jambo jema. Kwa hiyo nataka nimsihi sana Mheshimiwa Waziri aendelee.

Mheshimiwa Spika, nimeachiwa hapa taarifa na jirani yangu na mimi ni mtu muungwana Mheshimiwa Mwamoto amesema nizungumzie habari ya Kata ya Image. Kwa bahati nzuri naomba ku-declare interest, Kata ya Image ndiko nilikoolea mimi, Waziri apeleke umeme kwa wakwe zangu pale Image katika Jimbo la Kilolo na wakwe zangu nao kule wafurahie waseme na mzee alitaja ili mtoto wao aendelee kubaki mikono ni mwangu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwenye suala la kuongoza nchi ni suala ambalo hata wenzetu wameonyesha kwamba kuna kipindi unahesabu faida, ukiona faida ni kubwa unachukua huo huo uamuzi. Tumeona CHADEMA ni chama cha kidemokrasia na maendeleo lakini tumeona demokrasia hawaitendi, wana Mwenyekiti ana miaka 20 kwa sababu gani, pengine wanaona kuna faida kubwa kuendelea na huyo Mwenyekiti. Kwa hiyo wakati mwingine huwezi kuona faida ya moja kwa moja mpaka watu wakuelimishe kwamba hapa sasa unatoka kwenye reli. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika,Jambo lingine ambalo naliona hapa naona hapa tunazungumzia madeni ya TANESCO. Mheshimiwa Waziri hapa nataka anisikilize kwa makini sana. TANESCO imekuwa na madeni makubwa sana…

SPIKA: Mbona hakuna anayesimama upande huu huo msumari. (Kicheko)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, TANESCO ina madeni makubwa sana na madeni haya yanatokana na capacity charge za makampuni, makampuni haya matatu yanaipa mzigo mkubwa sana TANESCO. Kuna IPTL, kuna Aggreko, kuna Symbion, haya makapuni kila kampuni moja kwa mwaka linaitia deni TANESCO karibu bilioni 635, sasa hii si sawa. Serikali iondoe haya makampuni, iondoe mitambo yao, wanaipa TANESCO madeni makubwa sana, wanaagiza mafuta, wanaagiza vitu gani, matokeo yake ni kwamba tunapoteza fedha nyingi na tunaipa TANESCO mzigo mkubwa sana wa madeni.

Mheshimiwa Spika, vilevile ukiangalia kwa hesabu tu za shule ya msingi ukiondoa mitambo ya haya makampuni matatu utaokoa karibu trilioni mbili, maana ni trilioni moja na bilioni 930 na kitu, kwa hiyo utakuwa umeokoa karibu trilioni mbili. Hii itasaidia sana kuboresha uendeshaji wa TANESCO na wao watafika mahali watafanya kazi zao vizuri.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nimeona linatupa tabu, umeme ukikatika kutokana na mvua inawachukua muda mrefu TANESCO kwenda kushughulikia kwa sababu tuna umeme sehemu nyingi vitendea kazi vichache, magari machache ya TANESCO, mafundi wachache sasa wanachukua muda mrefu na kupoteza muda mrefu na kupoteza fedha nyingi, maana hivyo vijiji vina wateja tayari.

Mheshimiwa Spika, nimeona kuna kipindi Ndebo walikosa umeme, Mvumi Mission walikosa umeme inachukua mpaka wiki moja na nusu sasa hii si sawa, tuwarahisishie, aidha kwenye maeneo ambayo wanaona udongo wake haustamili sana wakati wa mvua wapitishe umeme chini au wanaweza kutumia umeme wa nguzo za zege, ukitumia umeme wa nguzo za zege ukazipitisha umeme juu maana yake eneo hilo hata kama mvua ikinyesha zege lile linazidi kujiimarisha.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano, haya maamuzi wanayoyafanya ni maamuzi ya utekelezaji wa Ilani ya Chama chetu. Hatuwezi kurudi nyuma kwa sababu tuliwaahidi Watanzania na wenzetu hawa ambao wanatupinga nao ni maamuzi ya chama chao, lakini hakuna mmoja hapa anayesema hataki umeme, sisi tuendelee kuwahudumia na wao kwenye majimbo yao tuwahudumie. Tunapopitisha hii bajeti tunapitisha pamoja na kusaidia majimbo ya Upinzani wa nchi hii kwa sababu kule kuna Watanzania, tunawahudumia Watanzania.

Mheshimiwa Spika, tuwahudumie wananchi wote kwa sababu mwakani nataka nikuhakikishieni kutakuwa na mabadiliko makubwa sana kupitia hii Wizara ya Nishati, Watanzania wamewashiwa umeme mpaka vijijini kitu ambacho kilikuwa ni ndoto, mwakani wanakwenda kuitunza Serikali hii ya Awamu ya Tano kwa kuipigia kura ambazo hazijawahi kupigwa kwenye Bunge hili, ambazo hazijawahi kupigwa kwenye nchi hii kwa sababu kazi iliyofanyika. Umeme uzuri wake ni kitu kinachoonekana kwa macho, kwa hiyo kila wanapokwenda akina Mheshimiwa Subira tunawaona na wananchi wanavyowapokea tunawaona, hawawezi kuwashangilia vile halafu kesho wakatunyima kura, haiwezekani! Kwa hiyo wanatufanyia kazi njema sana, wanatupa hoja za kwenda kuyasemea hata majimbo yao kwa sababu wanawasikia wanavyokataa bajeti wanawasikia, wanavyokataa umeme wanawasikia, lakini sisi wana CCM kwa sababu tumebeba dhima ya kuongoza Taifa hili tunapeleka umeme nchi nzima bila kujali Mbunge wa Jimbo hilo kasema nini humu ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niombe sana kazi ya kusambaza umeme iongezeke nguvu, vinginevyo kama Waziri atatuhakikishia kwamba anayo awamu nyingine ya nne, lakini kama ni awamu zile zile tatu maana yake hii ndio finally. Sasa kwenye finally kusiwe tena na kulegalega maana wametuambia kuna REA awamu ya kwanza, awamu ya pili na ya tatu, hatuna REA awamu ya nne. Kwa hiyo speed yao lazima iwe kubwa kuhakikisha kuwa mambo yanafanyika na yanafanikiwa ili kutupa hoja za kwenda kuwaambia wananchi umeme upo au haupo, wanasema upo, piga kura kwa Magufuli, shughuli imekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema gharama za kuendesha nchi ni kubwa, umeme wa maji utatuletea punguzo kubwa sana la gharama na hivyo kuifanya nchi yetu iweze kusonga mbele. Kwa hiyo naomba sana Mheshimiwa Waziri atakaposimama hapa vijiji vyangu avikumbuke; nimeomba umeme Kijiji cha Huzi, Kijiji cha Manda, Kijiji cha Ciifukulo, Kijiji cha Muheme, Kijiji cha Mpwayungu umalizike pale na Mvumi Mission tuhakikishe maeneo yote Chihembe yanapata umeme na kule nilikozaliwa mimi ili wananchi wenzangu waweze kupata maendeleo.

Mheshimiwa Spika, leo tumeona saluni zinafunguliwa vijijini, tumeona watu wanachomelea madirisha vijijini, tunaona vijana wanajiajiri kwa kupitia sekta hii ya umeme. Kwa hiyo niombe sana Mheshimiwa Waziri atakaposimama atuhakikishie kumalizika kwa REA III itakuwa ni lini ili vijiji vyote viweze kupata umeme na mambo yaweze kwenda.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)