Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Jang'ombe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu, ambaye ametujaalia uhai na kutupa afya tukahudhuria hapa kutekeleza wajibu wetu huu ambao tumeuomba kwa
wananchi.
Pili nawashukuru wananchi wa Jimbo langu la Jang‟ombe kwa kunichagua kwa kura nyingi na kwa kumchagua Rais Dkt. Magufuli kwa kura nyingi na hatimaye leo tumepata fursa hii ya kusimama hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni kwako, kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia hotuba ya Rais aliyoitoa wakati akilihutubia Bunge siku ya ufunguzi wake.
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya baadhi ya maeneo ambayo tayari ameshayafanyia kazi baada ya kuahidi kwa kipindi kifupi sana. Hii tayari tumeona jinsi alivyokuwa na nia ya dhati ya kuifikisha Tanzania hapa ilipo. Hii imeonyesha kwamba nia yake ataipeleka Tanzania pale tunapotaka.
Maana tukichukulia hotuba tutapata ushahidi wa kutosha kwamba hivi sasa maeneo mengi yameshafanyiwa kazi na tumeyaona. Ni kweli hapa kazi tu, maneno na fitina baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nimsifu Rais wangu, huyu ni muungwana. Kuna usemi wa Kiswahili unasema kwamba ada ya mja hunena, muungwana ni vitendo, tenda watu wataona, majisifu weka kando. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais baada ya kuapishwa aliahidi katika ukurasa wa 10 wa kitabu cha hotuba, kwamba atashughulikia ule mgogoro watu wanaouita wa Zanzibar. Kwa hiyo, alifanya hivyo, tumeshuhudia sote, alimwita Makamu wa Pili wa Rais, Rais wa Zanzibar,
Makamu wa Kwanza wa Rais ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha CUF, akaenda akazungumza nao na hatimaye matokeo tumeyaona kwamba Tume ya Uchaguzi imeshatangaza tarehe ya uchaguzi, nayo ni tarehe 20 Machi, 2016. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kulizungumza hili kwa sababu inawezekana kuna watu wakawa wanakosa njia za kuzungumza, wakafikiria kwamba Zanzibar kuna mzozo kiasi ambacho kwamba hakuna amani na usalama, kitu hicho siyo kweli. Ndugu zangu tufahamishane kabisa hapa, Zanzibar kuna amani na Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar ndiyo yenye mamlaka ya kufanya uchaguzi na kutoa matangazo ya uchaguzi. Hao waliosema kwamba aliyeshinda atangazwe, atangazwe nani? (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, matangazo yako mengi, kuna matangazo ya vifo yatatangazwa yote, lakini suala la kutangaza matokeo ya uchaguzi liko chini ya Tume, kifungu cha 42(1) mpaka (5), hakuna mwingine. Sasa katika suala hili la amani na mgogoro wa Zanzibar, Mheshimiwa Rais amelishughulikia vizuri sana na kwa sababu anafahamu yale mamlaka yaliyokuwepo ndani ya Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu walikuwa wakijinadi kwamba wanataka mamlaka kamili, leo wanakimbilia Marekani, wanakwenda Uingereza, wanakwenda kwa Papa, sasa hapo mamlaka hayo kamili ya ndani unayakataa mwenyewe. Wewe umetaka upate mamlaka
kamili, basi tumia Tume yako ambayo imepewa mamlaka kamili. Kwa hiyo, Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar ina mamlaka kamili kwa mujibu wa Ibara ya 104 ya Katiba ya Tanzania na pia kwa mujibu wa Ibara ya 119 ya Katiba ya Zanzibar, hilo limeelezwa wazi na halina utata wowote.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuhusiana na habari hiyo ya matangazo nani anagombea Urais, Mwenyezi Mungu ndiyo anaamua nani awe Rais, hatuwezi kuamua hapa.
“Qul-allahumma maalika‟lmulki tuuti-lmulka mantashaa‟u watanzi‟u-lmulka mimman tashaa‟u.” Mungu yeye ndiye anayetoa ufalme, hakukupa Mungu huwezi kuupata kokote; sema, toka mapovu, zunguka, hutoweza kupata chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mshairi mmoja anasema, kutapatapa haachi mfa maji baharini, ashika kila mahali aokoke maskini, kafa angali mbichi, mfa maji buriani. (Kicheko)
Sasa ndiyo maana watu wanashika kule na huku wapate hayo mambo. Watu labda hawaelewi, kwa nini Tume ya Uchaguzi ilifuta matokeo ya uchaguzi au ilifuta uchaguzi na matokeo yake hawajui. Kwanza yale ni mamlaka ya Tume, hakuna yeyote wa kuingilia Tume, ile ni Tume Huru, mambo yametangazwa wazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa mfano mmoja, mnaweza mkalia nyinyi. Kura ambazo zimepigwa Zanzibar, nyingine zimepigwa za watu waliokufa. Watu wote wanaelewa kwamba ilitokea ajali ya MV. Spice, watu zaidi ya 6,000 lakini baadhi ya waliokufa mle wamepigiwa kura
zao, sasa huu ni ukiukwaji kwa mujibu wa Tume na Tume ndiyo imetoa takwimu hizo. Sasa wako watu hata vitambulisho hawana…
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Hata vitambulisho hawajachukua, lakini kura zao zimepigwa, katazameni katika taarifa ya Tume.
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Hapo hapo ndipo aliposema Rais mzozo na ndipo hapo hapo walipojadili watu na sisi tunajadili hapo hapo. Kwa hiyo, Tume ndiyo yenye mamlaka kamili, watu ambao…
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza muda wangu uulinde. Sasa wamepigishwa kura maiti, sasa hawa wanakaa wapi? Leo mnasema kama uchaguzi ule halali, hawa watu mnaweza kuturejeshea, tukawaona? Kule kwetu kuna kitu kinaitwa giningi au wamewekwa giningi? (Makofi/Vigelegele)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Naibu Spika, hiki ndicho kilichotokea, kama hamjui, mnashabikia mnacheza ngoma si yenu, huo ndio ukweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine, napenda kuipongeza Hotuba hii ya Rais na napenda Rais aendelee kutufanyia mambo mazuri. Miongoni mwa mambo mazuri katika Mfuko wa Jimbo, Rais ameahidi kwamba atautoa mapema na haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, tunasubiri
ili tuweze kwenda kufanya maendeleo yetu. Ombi letu katika Mfuko huu wa Jimbo uwe unawiana kwa thamani ya sasa hivi kwa sababu ulifanyiwa thamani muda wa nyuma kidogo, kwa hiyo, uende na wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo tunamsisitiza Mheshimiwa Rais, kwa sababu tunafahamu yeye ni mzee wa hapa kazi tu, ni kwamba katika mchakato huu wa Katiba Mpya, amesema amepokea kiporo, kwa kuwa ni kiporo kipashwe moto tu, halafu tuendelee,
kwa sababu mchakato wa Katiba ulikuwa umeshafikia mahali pake, tuanzie pale mahali ambapo tuliachia ili tumalize.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine katika ukusanyaji wa mapato. Tumeona jitihada zake Mheshimiwa Rais, lakini pia, tunapenda ashirikiane na taasisi au zile Professional Bodies ambazo wamo wadau wa ukusanyaji wa mapato. Mle mna Wahasibu, mna na ma-auditors wa Kampuni, ili kusifanyike udanganyifu katika ukusanyaji wa mapato na mapato yasivuje. Kwa hiyo, hii tunasisitiza sana aweze kutumia Sheria, hebu wapewe hizi Professional Bodies zipewe meno.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote haya, tunapenda Rais awe na mashirikiano mazuri na wafanyabiashara au Serikali iwe na mashirikiano mazuri, lakini siyo kwa ajili ya kufanya kodi isikusanywe. Kwa hiyo, wakiwa na mashirikiano hayo, Serikali itaweza kukusanya kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la ulinzi na usalama; katika suala la ulinzi na usalama, nafikiri najilipalipa dakika zangu hapa! Katika suala la ulinzi na usalama hili ni jambo…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kingi, muda wako uliingiliwa hapo katikati, dakika moja ukae!
MHE. ALI HASSAN KING: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Bado dakika moja!
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama hili suala liangaliwe, kwa sababu katika baadhi ya maeneo, watu wanavikebehi vyombo vya ulinzi na usalama. Yako maeneo ambayo vyombo vya ulinzi na usalama havifanyi kazi vizuri kwa sababu ya nature ya
maeneo yale.
Kwa hiyo, hili Mheshimiwa Rais alichukulie hatua, alisema ataboresha makazi kwa wana ulinzi wetu, watu wa ulinzi na usalama. Kwa hiyo, afanye makazi yapatikane ili waepukane na kukaa kwenye nyumba za kupanga katika maeneo ya watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna sehemu moja siitaji, alikatwa kichwa Askari akitoka kweke kwenda kazini. Kama watakuwa wanapewa makazi, basi Askari hawataweza kufanyiwa mambo haya ambayo yako kinyume na Sheria. Ahsante. (Makofi)