Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu. Kazi yake ni nzuri, tufike mahali Watanzania tuanze sasa kukubaliana. Hii Wizara ya Elimu ina mambo mengi sana, lakini kimuundo wake jinsi ilivyo, mambo mengi tunayozungumza Waheshimiwa Wabunge ni ya TAMISEMI. Ukizungumzia Shule za Msingi, Shule za Sekondari, vyote viko chini ya TAMISEMI na hata ukiangalia suala zima la bajeti yake, sehemu kubwa inagharamia wa Loan Board na taasisi nyingine za juu. Yeye amebaki na function role ya kutunga sera na kusimamia sera. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna haja ya kuangalia vizuri mfumo mzima na muundo wa Wizara hii ili kweli ifanye kazi na tunaposema elimu hapa, basi moja kwa moja iweze ku-tricle-down kutoka kwa Wizara ya Elimu kuja mpaka elimu ya chini. Sasa hapa kuna gap na hata ukiangalia mazungumzo mengi ya Waheshimiwa Wabunge humu ndani, tunajaribu kuzungumza lakini kimsingi functionally, Waziri wa Elimu ana jukumu dogo sana hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kuna haja ya kuangalia muundo mzima wa Wizara hii ili sasa unapozungumzia Wizara ya Elimu, iwe na mantiki yenye kwenda mpaka kwa mwananfunzi wa chekechea. Leo hii unakuta Walimu wanadai stahiki zao, wana matatizo yao, wana mambo chungu nzima, hawana motisha, lakini bado kama Wizara ya Elimu, haina majibu ya haya. Haya peke yake yatajibiwa na Wizara ya TAMISEMI zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna debate inaendelea humu ndani, suala la shule binafsi na shule za Serikali. Waheshimiwa Wabunge, naomba nijielekeze kwamba bado suala la ada elekezi ni muhimu zaidi kwa Watanzania wote kwa sababu ukiangalia elimu siku hizi ni biashara. Mheshimiwa Mama Tibaijuka hapa ana shule zake as a business na wengine kadha wa kadha is a business. Sasa kwenye biashara zamani ilikuwa elimu ni huduma, lakini leo wanakopa kwenye mabenki wanawekeza kwenye elimu. Ni kama miradi mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa usipokuwa na regulation policy hawa watoto wa mkulima watoto wa Mtanzania ambaye hana uwezo wa kuweza kulipa ada, inakuaje? Kwa hiyo, lazima ifike mahali Serikali i-play role yake ya kuwasaidia Watanzania wote. Naheshimu kwamba shule za binafsi wacha mwenye kipato cha juu ampeleke mtoto wake kwenye shule ya binafsi alipie hiyo ada, ana uwezo wake; lakini yule ambaye hana uwezo, tunamsaidiaje? Sasa ni wajibu wa Serikali kuweza kuboresha. Lazima Serikali iboreshe. Inaboreshaje? Waheshimiwa Wabunge hapa tuje na mkakati tuseme iboreshe namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoanza kusema Wizara ya Elimu iboreshe, hataboresha huyu! Serikali kupitia TAMISEMI kwa Mheshimiwa Simbachawene, ndiyo tuipe jukumu kubwa la kuboresha Shule za Sekondari na Shule za Msingi ambao ndiyo msingi wa chimbuko la mwanafunzi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunasema kwamba lazima kuwe na ada elekezi, Serikali lazima iweke policy hiyo. Hawa watoto ambao wazazi wao hawana uwezo, watasomaje hizi shule? Hawa watoto ambao Serikali hii imejitolea kuchangia kupitia kodi za Watanzania, kwa sababu leo hii Watanzania katika kuboresha zile kodi za Watanzania, zimesaidia sasa kwenye kuboresha shule hizi. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, katika hili naomba tukubaliane tu. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, katika hali ya kawaida, mitaala yetu ya elimu bado ina mapungufu makubwa sana. Leo watoto wanapohitimu, hatuwatengenezi katika akili ya kujiajiri au kujitegemea. Tunawatengeneza katika akili ya kuajiriwa kitu ambacho ni tatizo. Kwa hiyo, kuna haja ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, naomba mje na mtaala ambao utasaidia wahitimu wanapohitimu iwasaidie kuweza kujitegemeza katika kujenga maisha yao. Bila kufanya hivyo, suala la ajira ni tatizo na bado Watanzania tunazidi kulia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii katika Labour Market Watanzania tunapoenda ku-compete watu wengi hatuwezi kufaulu. Niwape tu mfano. Leo hii Makao Makuu ya Kiswahili yako Zanzibar lakini anaye-head ile timu ni Mkenya kwa sababu Mtanzania hakuna aliyefaulu kujua kusema Kiswahili vizuri kuliko Mkenya.
Kwa hiyo, Watanzania tunakwenda kwenye job Market, hatuna uwezo wa kutaka kuchukua kazi hizi? Anayefuatia pale ni Mganda. Leo Watanzania pamoja na kwamba Kiswahili kilizaliwa Tanzania, kikakua Tanzania, kikaanza kukulia nchi jirani kikafia kwingine na kikazikwa kwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Watanzania tunaenda kwenye soko la ajira tuna tatizo kubwa sana, lakini ni kwa sababu ya muundo na mfumo wa elimu yetu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri, wewe una nafasi ya pekee, umekuwa ni mtu ambaye ni mahiri toka ukiwa NECTA. Umefanya kazi nzuri. Tumia sasa utalaamu wako huo kuweza kui-shape Wizara ya Elimu ili Watanzania wapate wanachokitaka. Leo hii ukiangalia, Tanzania ina wasomi wengi sana lakini wakipelekwa kwenye soko la ajira ni wachache wanaweza ku-compete na kupata kazi za Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hili tuweze kuliangalia. Vile vile kuna suala la mazingira ya elimu na hasa watoto wa kike. Kuna baadhi ya maeneo watoto wa kike wanashindwa kwenda shule kwa sababu hakuna vyoo. Wanashindwa kujisaidia vizuri kwa sababu ni watoto wa kike; wanashindwa kusoma kwa sababu ni watoto wa kike. Naomba tuweke mkazo, Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Mheshimiwa Simbachawene Waziri wa TAMISEMI, naomba muwe na link nzuri na Wizara ya Elimu. Mfanye kazi kwa maelewano mazuri ili kusudi tuwasaidie watoto wa Mtanzania waweze kuhitimu vizuri na wapate elimu inayotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilisoma katika shule za mission Form One mpaka Form Six, ni mdau. Natambua ubora wa shule binafsi, lakini naiomba Serikali hii itusaidie, bado Shule za Serikali zinatakiwa ziboreshwe zaidi ili ziweze ku-compete na shule za binafsi. Tusipofanya hivyo tutakuwa tunacheza mchezo ambao ni wa kuigiza. Mzazi anahitaji asomeshe mtoto wake, lakini tunahitaji quality of education.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima ubora wa elimu tuuzingatie. Tusiwe na wingi tu wa kusema tunaingiza watoto, wanasoma. Tumeanzisha Shule za Kata, zimesaidia sana kuwaelimisha Watanzania, zimesaidia sana mpaka Waheshimiwa Wabunge humu wamesoma Shule za Kata, wako humu ndani. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Aweso huyu ni zao la Shule ya Kata, leo ni Mheshimiwa Mbunge hapa ndani na wengine, lakini watu walidharau wakasema ni yebo yebo, hakuna cha yebo yebo! Hizi shule zimesaidia, naomba tuziboreshe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni madai ya Walimu. Hivi huyu Mwalimu atakuwaje na moyo wa kufundisha? Atakuwaje na moyo wa kumwelimisha mtoto wa Mtanzania…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)