Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

Hon. Dua William Nkurua

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nanyumbu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati

MHE. WILLIAM D. NKURUA: Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kupongeza Wizara na hasa utendaji uliotukuka wa Waziri na Naibu wake.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono kwa dhati kabisa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme kule Rufiji. Ni wazi kuwa umeme wa maji utashusha gharama za umeme hivyo wananchi wengi kumudu gharama, lakini pia uwekezaji utakuwa rahisi kumudu ushindani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Nanyumbu ilipata umeme kwa mara ya kwanza mwaka 2013 kwa mpango maalum wa Serikali. Vijiji vilivyopatiwa kipindi hicho ni 23 kati ya 93 kwa bahati mbaya sana REA awamu ya kwanza nay a pili Nanyumbu ilikosa. REA awamu ya tatu Nanyumbu ilipatiwa Vijiji 13 tu. Niliomba nyongeza ya vijiji 17 ili kufanya vijiji 30, ombi ambalo Waziri alikubali kwenye mkutano wa hadhara katika uzinduzi wa REA awamu ya tatu pale Michiga.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tunatarajia kufikia asilimia 84 ya vijiji vitakavyopata umeme ifikapo 2020, naomba kufanyika upendeleo wa maeneo yaliyobaki nyuma kama Wilaya ya Nanyumbu. Vijiji vilivyopo kati ya Mangaka na Lumesule ambapo HT imepita na vijiji hivyo kukosa umeme, vipewe kipaumbele katika utekelezaji wa REA III.

Mheshimiwa Spika, Mjini Mangaka, Makao Makuu ya Wilaya ya Nanyumbu maeneo mengi hayana umeme, hasa Mtaa wa Mchangani, nashauri eneo hili lifanyiwe kazi haraka. Mji wa Mangaka unapata maji toka kwenye bwawa la Kijiji cha Mara ambapo maji yanasukumwa kwa kutumia jenereta ambapo linaharibika mara kwa mara pia gharama za uendeshaji huwa juu.

Mheshimiwa Spika, naomba umeme uende katika eneo hili. Endapo tutapeleka umeme eneo hili tutakuwa tumevipatia vijiji vya njiani umeme ambavyo ni Matimbeni KCU na Sengenya KCU.

Mheshimiwa Spika, kasi ya mkandarasi anayefanya kazi Mkoani Mtwara ni ndogo, hadi sasa ni kijiji kimoja tu ndio kimewashwa na vijiji vingine ni hatua ya kusimika nguzo.

Mheshimiwa Spika, nashauri katika kutengeneza mpango wa kupeleka umeme eneo fulani REA izingatie ushauri wa wataalam wa eneo husika, kwani nimeona makosa ambayo kama aliyepanga angekuwa ni mwenyeji baadhi yake yasingetokea.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.