Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Riziki Saidi Lulida

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nikushukuru na niwatakie heri Waislam na wasiokuwa Waislam katika mwezi huu Mtukufu na kuwaombea amani na utulivu katika nchi yetu ya Tanzania ambayo itajengwa na Watanzania wenyewe. Hawezi kutoka mtu huko nje kuja kutuletea amani na utulivu, tushikamane Watanzania wote, tuijenge amani yetu na wenzetu wajifunze na iwe mfano katika nchi za wenzetu ambao wameonja vita ikiwemo Libya. Libya wameonja vita wakasema hakuna democracy, leo wenzetu wa Libya wapo katika uchumi mgumu, tujifunze kwa mapana yetu, tusiende kuhangaika na maneno ya uchochezi wakaifanya nchi ikamwaga damu. Nawapenda Watanzania, naipenda amani ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nitazungumzia suala la mjusi ambaye yupo Ujerumani. Nilimwacha katika Wizara ya Maliasili kuileta kwa vile hapa ni sehemu pekee ambayo Ubalozi wa Ujerumani ni kama nchi ya Ujerumani iweze kutuambia sisi watu wa Mkoa wa Lindi ambao lile jusi kubwa (dinosaur) na mifupa yake ipo Ujerumani, tunapata nini ndani ya yule mjusi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetaka kufunga ukurasa leo, Wizara ya Maliasili, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ishirikiane na nchi ya Ujerumani tuweze kujua katika Halmashauri ya Lindi inapata nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji ambavyo vimezunguka pale palitoka yule mjusi wamesema it’s a lost science, hapana it’s a life science. Naomba Ubalozi wa Ujerumani wawatoe wawakilishi, nifuatane nao mimi nikiwa na kundi langu maalum twende mpaka Tendeguru lilipotoka lile jusi ili wakajionee kuwa jusi lile limetoka Tanzania katika Wilaya ya Lindi Vijijini, katika Kijiji cha Mipingo na Wanamipingo waweze kufaidika na mjusi yule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili nalizungumza kwa mapana yake; utalii mkubwa utakaopatikana ndani ya Tendeguru utakuwa ni uchumi mkubwa katika uchumi wetu wa Tanzania. Tulikaa kwa muda mrefu toka mwaka 1905, mvumbuzi ambaye alikuwa mchimbaji wa madini akishirikiana na Wolf Henrick pamoja na Martin Abald, wao walikwenda Tendeguru kuchukua ile mifupa kwa ajili ya uchimbaji, wamepeleka Ujerumani, kunafanyika exhibition. Katika miaka yote mpaka leo katika vijiji vile hatujafaidika hata kwa kujengewa shule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni matumaini yangu Balozi na wawakilishi kutoka Ujerumani wananisikia, tukitoka hapa moja tu kuwa tunataka maendeleo katika Wilaya ya Lindi katika kupitia eneo lile lililotoka mjusi hata angalau wakatuonyeshe kumbukumbu iko wapi. Tunataka ushirikiano kati ya Ujerumani na Lindi Vijijini ili angalau Lindi Vijijini wajue pato linalopatikana na wao wanafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu; naomba tupate shule katika eneo la Mipingo na vijiji vinavyozunguka, tunataka maji maana yake maeneo yale hayana maji, tupate maji katika maeneo yale, tupate vituo vya afya ili kujenga uhusiano bora uliokuwepo kati ya Tanzania na Ujerumani kwa kupitia dinosaur. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la mwisho, wanazungumza halijulikani it’s a lost science, it’s not a lost science, it’s a life science come to Tanzania and visit Tendeguru na mtaona kila kitu kipo pale. Ni matumaini yangu kuwa leo naitangaza Tendeguru ndani ya Bunge, naitangaza Tendeguru ndani ya Ujerumani, Wajerumani tukutane baada ya Bunge, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Waziri wa Maliasili na Waziri wa Fedha tukutane kwa pamoja na mimi mwenyewe kama mdau mwanaharakati kwa muda wa miaka 15, naomba nami niwepo nithibitishe hili ili mapato yapatikane na nchi yangu iweze kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia fursa zilizopo ndani ya Balozi zetu. Nchi hii tuna Balozi ambayo inataka kutupa uwakilishi, wale Mabalozi wasikae ubalozini kule wamekaa wanatumia pesa nyingi, matumizi makubwa. Je, wana-deliver nini katika nchi yangu ya Tanzania? Tunataka fursa tulizokuwa nazo Tanzania za kilimo, madini waje watuonyeshe tunafanya hivi. Tumekwama tunataka soko la Euro, wale wa Europe wanatupa soko gani sisi Watanzania ili angalau tutoke na mazao yetu, haiwezekani Tanzania soko letu mpaka twende Uganda, Rwanda; imekuwaje Mabalozi wetu wanafanya nini kutushirikisha kama nchi kuiingiza katika uchumi bora wenye maendeleo. Tanzania yenye maendeleo kwa kupitia Balozi zetu inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)