Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Katavi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa fursa ili niweze kuchangia Wizara hii pia naunga mkono maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani.
Mheshimiwa Spika, katika Taifa letu asilimia 53 ya ardhi yetu ni misitu, pia asilimia 15.4 ni eneo ambalo linafaa kwa ajili ya kilimo, malisho na maeneo mengine. Sasa inashangaza kama bado tuna eneo kubwa kiasi hiki na Wizara hii ya Makazi inashindwa kutenga maeneo kwa maana ya kutenga maeneo ya makazi kwa wananchi wakapata hati zao na tukaepuka migogoro ambayo inaendelea. Hilo ni jambo la kwanza. Pia Serikali hii ikatenga maeneo kwa ajili ya malisho ili kuepuka migogoro kati ya hifadhi na Serikali.
Mheshimiwa Spika, pia kuna migogoro mingi ambayo inaendelea kwenye nchi hii inasababishwa na Wizara hii kushindwa kutatua migogoro ya ardhi, kuna masuala ya Taasisi za Serikali kukosa Hatimiliki, wananchi wanapewa hati kwa mfano kwenye Manispaa ya Mpanda kwenye Kata ya Misunkumilo, ukija Mpanda Hoteli, Milala na maeneo mengine wananchi wale wamepewa hati na wamepelekewa huduma za kijamii kwa maana ya masanduku ya kupiga kura, umeme, maji pamoja na barabara .(Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa watu hawa wanakwenda kuwaondoa, ni Serikali hii moja ya Awamu ya Tano, imepeleka huduma hizo, pia Jeshi liko pale pia nao hawana hati. Sasa mazingira haya yanapelekea wananchi wetu kupata shida, wananchi wanajenga nyumba katika mazingira magumu sana na wananchi wetu wengi ni maskini. Kwa hiyo Wizara hii ione namna ya kuharakisha jambo hili la kutoa hati kwa wananchi haraka iwezekanavyo hususani katika maeneo ambayo wananchi wanajenga katika makazi mapya.
Mheshimiwa Spika, vile vile niongele suala la Shirika la Nyumba la Taifa, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, tumeweza kuzungukia maeneo mbalimbali kwa maana ya miradi ambayo iko chini ya shirika hili ikiwepo na mradi wa Dege Eco ambao uko Kigamboni, TBA na maeneo mengine. Ukiangalia nyumba hizi kuna maeneo mengine kweli shirika wamejitahidi, lakini tunaona namna ambavyo Serikali inatumia gharama kubwa kwa kutumia pesa za Serikali kujenga nyumba hizi na tukiangalia outcome yake ni ndogo, outcome yake ni ndogo kwa sababu watumishi wengi wanashindwa ku-afford kununua na kupangisha kwa sababu gharama ziko juu. Kwa hiyo kupitia Wizara hii niombe pia Mheshimiwa Waziri kuona namna ya kuweza kupunguza gharama za upangishaji pia gharama za ununuzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukija changamoto nyingine ni kwa nini nyumba hizi zinakosa wateja. Unakuta nyumba zimejengwa kwenye maeneo ambayo hata miundombinu hakuna, barabara nyumba inajengwa porini, sasa unategemea mtumishi gani anaweza kwenda kupanga au kwenda kununua eneo hilo. Kwa hiyo Serikali ione namna ya kuweza kuboresha miundombinu ya maji, umeme, barabara na huduma za afya na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niongelee jambo la mwisho kuhusiana na suala la mipaka; narudi palepale kwamba migogoro mingi na Mheshimiwa Waziri amesema Mkoa wetu wa Katavi pia umekuwa wa mwisho kwa kukusanya hayo makusanyo ya mapato kwenye hilo eneo. Ni kweli lazima tushindwe kwa sababu hata ukiangalia halmashauri yetu bado haina uwezo, leo tutawalazimisha watu wapime na hakuna ushirikishwaji wa moja kwa moja na hizi Taasisi Binafsi bei imekuwa iko juu sana, watu wanashindwa kulipia tozo hizi zimekuwa ziko juu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba Serikali ione namna ya moja kwa moja kuweza kushirikisha hizo kampuni binafsi, halmashauri zetu na Serikali kwa ujumla wake kwa sababu wananchi wanashindwa kupima maeneo kwa sababu gharama ziko juu na leo tutaendelea kuweka uzembe kwenye eneo hili matokeo yake tuje kuwabomolea wananchi na ndiyo masuala ya bomoabomoa Serikali hii inashindwa kulipa pia masuala yao ya fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, masuala ya uwekaji wa hizi beacon; kumekuwa na migogoro hii ya muda mrefu ambayo Mheshimiwa Waziri amesema na Mheshimiwa Rais ametamka kwamba kwenye eneo ambalo linahusisha mgogoro kati ya hifadhi na wananchi maana yake wananchi wapewe kipaumbele. Sasa katika maeneo hayo ninayozungumzia katika Kata ya Sitalike ambayo iko katika Jimbo la Nsimbo Lyamgoloka, Kasekese na maeneo mengine ambayo yana migogoro hii, ni kwamba Serikali hii imeshindwa kuwashirikisha wananchi moja kwa moja kwa maana ya kuonesha hiyo mipaka. Sasa ni lengo la Serikali hii kuhakikisha linatatua migogoro hiiā¦
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Spika, kwa kuweka mipaka. Ahsante.