Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante. Labda kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia afya njema, tukaweza kukutana na kuendelea na shughuli za Bunge letu. Pia niungane na wenzangu katika kuipongeza Wizara, pamoja na kwamba upo upungufu mchache, lakini wanapofanya vizuri lazima tuseme wamefanya vizuri, lakini pale kwenye matatizo basi hatuna budi kushauriana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kusema tu kwamba, ardhi ni mali, lakini kwa bahati mbaya ardhi sasa haiongezeki, lakini sisi binadamu na shughuli zetu tumekuwa tukiongezeka. Sasa tatizo linalokuja ni kwamba kwa kuwa ardhi haiongezeki na kila mmoja sasa hivi amekwishajua kwamba ardhi ni mali ndiyo pale panapotokea migogoro ya mara kwa mara. Sasa nishauri tu kwamba Mheshimiwa Waziri aendelee kufanya kazi, lakini asiwe anafanya kazi yeye na Naibu Waziri tu, pamoja na watumishi wa Wizarani, lakini hata wale Maafisa Ardhi wa kwenye Halmashauri, Maafisa Mipango Miji na Maafisa wengine nao waige mfano wa Mawaziri wetu hawa wawili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Kwenye Jimbo letu la Tanga pamekuwa na migogoro ya hapa na pale, kwa mfano ipo migogoro ambayo Mheshimiwa Waziri amekwishajaribu kuishughulikia, lakini bado haijakaa vizuri sana. Nitoe mfano, labda kuna mgogoro huu wa JWTZ na maeneo ya Mwahako pamoja na wananchi. JWTZ waliwalipa pale wananchi kumi tu, lakini baada ya kulipa wananchi kumi wanasema eneo lote lililobaki ni eneo la Jeshi.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya sasa, wakati mwingine majeshi nayo yanakuwa na sheria ngumu, baada ya kuchukua umiliki wa lile eneo basi imekuwa hakuna ruhusa hata kupita kwa miguu katika maeneo hayo. Ikumbukwe baadhi ya maeneo hata kama tuna majiji lakini bado kuna vitongoji au kuna maeneo ambayo ni ukiyatazama ni maeneo ya vijiji kwa sababu kuna mashamba, kuna wafugaji na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa namwomba kwanza Mheshimiwa Waziri, pale ambapo Jeshi liko karibu na wananchi pawe na mahusiano mazuri. Kwanza, ukilitazama jina lenyewe la Jeshi ni Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Sasa linapokuwa jeshi hapatani na mwananchi, hapo napata tabu kidogo kuelewa. Kwa hiyo naomba awaelekeze washirikiane na wananchi.
SPIKA: Haya Taarifa Mheshimiwa Laizer.
TAARIFA
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa, kwamba ni Jeshi la Wananchi...
SPIKA: Ngoja zima kwanza, Mheshimiwa Mbarouk, endelea…
MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Spika, taarifa ninayotaka kumpa ni kwamba tulichofanya sisi Monduli, kwa sababu ni Jeshi la Wananchi tuliwapa ardhi bure, tukawa na ujirani mwema; tatizo la wananchi wengi wanataka walipwe fidia, lakini warudi kutumia ardhi hiyo hiyo ambayo alishalipwa fidia. Kwa hiyo tujenge utaratibu wa mashirikiano na jeshi.
SPIKA: Anakushaurini tu kwamba, ukilipwa fidia maana yake uondoke jumla.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, sasa baadhi ya watu hawajalipwa, kuna wananchi 112 hawajalipwa na wamekuwa wakifuatilia malipo yao wamekuwa wanahangaishwa na wao kikubwa wanasema kwa nini wanadai fidia? Ni kwa sababu hata kama eneo hilo limechukuliwa na Jeshi, wanasema Sheria Na.4 ya mwaka 1999 nafikiri Waziri anaijua vizuri ile inayosema: “whether you have tittle deed or not so long you have been there for a long time, customary law recognize you as the owner of the land.” Sasa wananchi wanapoitumia sheria hii ndiyo wanapoona kwamba ni haki yao.
SPIKA: Nani alikuwa anasema Mussa Mbarouk hajui Kiingereza? Si mnaona ameteremka vizuri kabisa jamani? Endelea Mheshimiwa Bwana. (Kicheko)
MHE. MUSSA B. MBAROUK: …inaeleza kwamba hata kama kuna mradi wa maendeleo lakini lazima kwanza akae mwekezaji, ikae Serikali kwa maana ya Wizara ya Ardhi na wananchi; sasa wakati mwingine wananchi wanakuwa wanasumbuliwa kulipa malipo ambayo wanastahili na ni haki yao; na siyo hapo tu; kwa mfano; nashukuru kwamba Serikali Waziri Kamwelwe hapo amesema Uwanja wetu wa Ndege Tanga umepatiwa fedha takribani bilioni 36 ili ufanyiwe upanuzi na uwe wa kisasa zaidi; hususani kutokana na uwekezaji mkubwa unaokuja. Hata hivyo kuna nyumba zimefanyiwa evaluation tangu mwaka 2008, wananchi wale hawajalipwa, nyumba 38. Sasa hivi ili uwanja uwe mkubwa zaidi pana nyumba 802 maeneo ya Masiwani Shamba ambayo ni kata mpya zinahitajika kuondoka. Sasa wananchi wanasema hatukatai kuondoka lakini kwa Sheria ile Namba Nne tulipwe kwanza fidia hatukatai maendeleo.
Mheshimiwa Spika, mimi nashauri, Mheshimiwa Waziri, wananchi wale wa mwaka 2008 wa maeneo ya Masiwani Shamba walipwe fidia zao, lakini hata hizi nyumba 802 ambazo ni za kisasa ziondoke lakini wananchi wakabidhiwe fidia zao. Kwa sababu, mtu wa kawaida anaweza akajenga nyumba labda miaka mitatu mpaka miaka 10 lakini inapokuja shughuli za maendeleo likitolewa tu tamko ujue utaondoka; sasa hawa nao ni Watanzania wakimbilie wapi? Kwahiyo mimi naishauri, Serikali pamoja na maendeleo, maendeleo nayo yana gharama zake Wananchi wetu lazima wafidiwe.
Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshgi, kuna mgogoro wa eneo pia la kwa Ramsing, nafikiri Mheshimiwa Waziri hili ulilisikia. Wapo wazee ambao ni wenyeji wa maeneo hayo, lakini kuna huyo Ramsing ambaye alikuwa ni Singasinga alikuwa analima miwa na kutengeneza sukari wakati huo. Baada ya kuondoka na shamba lile kutaifishwa na Serikali, kwa bahati mbaya sana lile eneo lilirudishwa kwenye Halmashauri. Sasa baada ya Halmashauri nayo kushindwa kulisimamia vizuri pakatokea UVCCM wakasema lile eneo ni la kwao.
Mheshimiwa Spika, wale wazee hawakatai, wanasema kuna eneo la UVCCM lakini kuna eneo la wenyeji. Sasa limechukuliwa eneo lote limekuwa la UVCCM, wazee wale wanasema sisi tutakwenda kulima wapi na sisi tuna warithi wetu ambao ni watoto wetu? Kwahiyo naomba pia Mheshimiwa suala hili ulishughulikie ili tuondoe migogoro isiyokuwa ya lazima; na kama wachangiaji wengi wanavyokusifu, kwamba ni kinara wa kutatua migogoro, basi nakuomba na migogoro hii iliyoko Tanga nayo uitatatue.
Mheshimiwa Spika, lakini kama hili halitoshi kuna suala la EPZ maeneo ya Mwahako vilevile; jambo hili lina karibu miaka nane watu wa maeneo ya mbugani; miaka nane imeanzishwa EPZ lakini watu bado hawajalipwa na wamezuiwa kuendeleza majengo yao. Wanasema tunavyojua sisi sheria na taratibu za evaluation ikipita miezi sita lazima ifanyike upya kwa bei ya soko iliyokuwepo ya ardhi ya wakati huo; sasa hawa wananchi mpaka leo hawajui waende wapi. Nakuomba nalo Mheshimiwa Waziri hili ulishughulikie lipate ufafanuzi.
Mheshimiwa Spika, lakini lingine nikija kwenye gharama za upimaji; vifaa vya kupimia umetuambia na kupongeza kwa hili, kwamba Halmashauri zetu zikachukue vifa vya kupimia kwenye Kanda, lakini sasa kupitia Bunge hili uwatamkie wananchi kwamba gharama za kupima kiwanja kimoja ni shilingi ngapi. Kwasababu wenzetu wa kwenye Halmashauri wanatoza gharama kubwa utafikiri kile kifaa labda ni chaki kwamba ukiandikia inakwisha, kumbe kifaa kile ni kuweka battery kwenye charge ukaenda ukakitumia kinakuwa kinaendelea kudumu.
Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na hilo, eneo la Ngamiani Kati, Ngamiani Kaskazini na Ngamiani Kusini ambayo ndiyo kioo cha Mji wa Tanga; eneo lile lilipimwa zamani enzi za wakoloni watu wakapewa offer lakini hawana hizi hati kubwa za kisasa. Sasa nilikuwa naishauri serikali, kwa gharama zake, kwasababu pale asilimia kubwa nyumba zile ni za mirathi, wengine wameuza, wengine hawaelewi taratibu; kwahiyo napo Serikali ingepima eneo la kuanzia barabara ya kwanza mpaka barabara ya 21 ili na wananchi wale wapatiwe hatu ambazo zitawasaidia katika matumizi yao ya kila siku.
Mheshimiwa Spika, kama hili halitoshi, kuna mgogoro mkubwa sana sasa hivi kati ya Halmashauri na wananchi wa maeneo ya Mabokweni na Kirare na maeneo ya Amboni Cross Z. Tunajua kuna Kampuni ya Amboni ilikuwepo. Kamouni ya Amboni wakati huo, Waziri wa Kilimo na Mifugo…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Spika, ahsante.